Minister's Statement
The Web Kilimo web
Home | Budget Speeches | Publications | Agricultural Statistics | Legislations and Regulations | Web Links
 

 

HON. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE (MP)

MINISTER FOR AGRICULTURE FOOD SECURITY AND CO-OPERATIVES

 

 

 

HOTUBA YA UZINDUZI WA BODI YA WAKURUGENZI YA BODI YA NAFAKA NA MAZAO MCHANGANYIKO ILIYOTOLEWA NA MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE(MB) WAZIRI WA KILIMO CHAKULA NA USHIRIKA UKUMBI WA WIZARA YA KILIMO CHAKULA NA USHIRIKA MANISPAA YA DODOMA TAREHE 14 FEBRUARI 2011.

 

Ndugu Mwenyekiti wa Bodi, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko
Wakurugenzi wa Bodi, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko
Wakurugenzi wa Idara, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika,
Washiriki Waalikwa wote,
Mabibi na Mabwana.

Ndugu Mwenyekiti,
Nachukua fursa hii kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha sote kuwa hapa na kwa kuwasafirisha salama kushiriki katika Uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko. Vile vile nashukuru kwa kupewa Heshima ya kuwa Mgeni rasmi katika kuizindua Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko.

Aidha, nawapongeza Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kwa kuteuliwa kwenu kuiongoza Bodi hii muhimu katika kuendeleza sekta ya kilimo hapa nchini.
Kuteuliwa kwenu konaonyesha imani tuliyonayo kuhusu uwezo wenu katika kusaidia kutekeleza jukumu la kuendeleza mazao mchanganyiko nchini.
Ndugu Mwenyekiti,
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugezi hii kwa sehemu kubwa imetokana na mchakato ulioanzia katika ngazi ya mikutano ya Kanda za Kilimo iliyofanyika kote nchini. Wengi wenu ni mashahidi wa jinsi mikutano hiyo ilivyofanyika na jinsi mlivyoteuliwa kuwa wawakilishi wa Kanda hizo kwenye Bodi.

Bodi ya Wakurugenzi imewashirikisha wajumbe kutoka katika makundi yafuatayo kama yalivyoainishwa katika sheria;

 • Mjumbe mmoja mmoja kutoka Kanda za Kilimo za Mashariki, Kaskazini, Ziwa, Magharibi, Kati, Kusini na Nyanda za Juu Kusini.
 • Mjumbe mmoja mmoja toka Wizara za Kilimo Chakula na Ushirika, TAMISEMI na Biashara Viwanda na Masoko.
 • Wajumbe wenye ufahamu na uzoefu katika mazao aina ya nafaka na mazao mchanganyiko.

Ni dhahiri muundo wa Bodi umewashirikisha wajumbe wenye taaluma tofauti ili kuunganisha nguvu ya taaluma na uzoefu kuweza kukabiliana na matarajio ya Serikali na Wananchi na changamoto zitakazojitokeza wakati wa kutekeleza majukumu ya Bodi.
Ndugu Mwenyekiti,
Chimbuko la Bodi linatokana na mabadiliko ya kiuchumi yaliyojitokeza nchini, hususan katika sekta ya kilimo yaliyosababishwa na uamuzi wa serikali wa kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa kutegemea nguvu ya soko.
Utekelezaji wa sera ya soko huria ulilazimisha ubinafsishaji wa mashirika ya umma yaliyokuwa  yanatoa huduma za masoko ya mazao ya nafaka na mengineyo. Ilitarajiwa kuwa sekta binafsi ingeweza kutekeleza majukumu hayo kwa ufanisi. Hata hivyo uzoefu unaonyesha matokeo tofauti yakiwemo ya viwango kushuka; kutozingatia vipimo kuliongezeka. Aidha masoko ya nafaka na mazao mengine hayakuwa ya ushindani kama ilivyotarajiwa.

Ndugu Mwenyekiti,
Kama mnavyofahamu Serikali imeanzisha Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kwa Sheria namba 19 ya mwaka 2009 (The Cereals and Other Produce Act 2009). Kulingana na Sheria iliyoianzisha Bodi hii, malengo ya kuanzishwa kwa Bodi ya Nafaka ni kuhamasisha na kuendeleza mazao ya nafaka na mazao mengineyo na kutoa huduma zinginezo zikiwemo za  uzalishaji, usindikaji, ugani, utafiti na masoko.
Aidha Serikali ilitoa mambo ya kuzingatiwa wakati wa mchakato wa uanzishaji wa Bodi hii. Mambo hayo ni pamoja na;

 • Maghala na majengo ya NMC ambayo bado hayajabinafsishwa yaliyoko Mwanza, Iringa, Arusha na Dodoma yakabidhiwe Bodi
 • Changamoto zilizojitokeza wakati wa NMC na GAPEX lazima ziangaliwe kwa makini na kufanyiwa kazi ili zisijitokeze tena.
 • Bodi ijihusishe pia na usambazaji pembejeo za kilimo, usindikaji ili kuondoa matatizo ya upatikanaji wa pembejeo na kuongeza thamani mazao ya wakulima.

 

 

Ndugu Mwenyekiti,

Sheria ya uanzishwaji wa Bodi hii imelenga;-

  • Kuongeza kipato cha wakulima wa mazao mbali mbali kwani sheria imeipa Bodi jukumu la kufanya biashara. Jukumu hili linalenga kuongeza ushindani baina ya wafanyabiashara na Bodi kwa lengo la kumuongezea mkulima bei ya mazao yake na kumpatia soko la uhakika.

Aidha, kuongeza uzalishaji kwa tija (kiwango na kiasi) kutokana  na kuwepo kwa vyombo vya kuendeleza na kusimamia mazao hayo na wakulima kufanya maamuzi sahihi kutokana na upatikanaji wa taarifa na takwimu sahihi kuhusiana na uzalishaji, soko na bei ya mazao.

  • Kuwezesha Wadau wote wa mazao husika kushiriki kikamilifu katika kujadiliana kupanga na kushiriki katika kuchangia maendeleo ya pamoja;
  • Kuwezesha Halmashauri za Wilaya zilizoko katika maeneo ya mazao husika zishiriki katika utekelezaji wa Mikakati na Program za kuendeleza zao husika kupitia Mipango yao ya Kuendeleza Kilimo Wilayani (DADPs). Aidha, Halmashauri hizo zitawezeshwa na sheria kuandaa sheria ndogo za kusimamia utekelezaji katika ngazi za Wilaya;
  • Kuimarisha masoko, viwango, ubora na kusisimua sekta binafsi katika kumpatia mkulima bei nzuri ya ushindani.

 

Ndugu Mwenyekiti,
Ili kuweza kuyatekeleza majukumu hayo ambayo Taifa linatarajia kutoka kwenu, ni muhimu kuzingatia mambo yafuatayo;

 • Kuhakikisha Bodi inajishughulisha na uendelezaji wa mazao nchini na biashara kwa lengo la kumuwezesha mkulima kupata bei nzuri yenye ushindani na soko la uhakika kwa mazao yake;
 • Kushirikiana na Mabaraza ya Kanda saba za kilimo ambayo yameanzishwa ili kupitia mikutano ya wadau ya kikanda na uwakilishi wa kikanda katika Bodi ya Wakurugenzi, mipango mikakati ya kuendeleza mazao ya nafaka na mchanganyiko iandaliwe na kutekelezwa.

 

 • Kutambua Mkutano wa Kanda wa wadau kuwa ndio chombo kinachotambulika kisheria cha kutoa maamuzi kwa niaba ya wadau wote wa mazao katika Kanda husika katika kuamua muundo wa kitaasisi wa kusimamia utekelezaji wa majukumu ya pamoja  (shared functions) na utaratibu wa kugharamia muundo huo kwa hiari;
 • Kuandaa mpangomkakati na mpangobiashara ya Bodi ambayo itakuwa ndiyo dira yenu katika kutekeleza majukumu mliyokabidhiwa kwa ufanisi.

 

 •   Kusimamia mali za Bodi kwa umakini mkubwa ili kuiwezesha    

      Bodi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kukidhi haja na   
      matarajio ya wananchi.

Ndugu Mwenyekiti,
Pamoja na matarajio ambayo wananchi wanatarajia kutoka kwenu, ufumbuzi wa changamoto zifuatazo zinazokabili mazao ya nafaka na mazao mengine unahitajika;

 • Kushindana na kuishinda sekta binafsi;
 • Kuhamasisha uzalishaji wa mazao husika katika Kanda;

 

 • Kutumia njia za kisasa kuanzisha masoko ya mazao kitaifa, ki-kanda na kimataifa (Commidity Exchange);
 • Kutumia fursa/sera zilizopo za kuendeleza kilimo kwa manufaa ya wananchi kama vile Kilimo Kwanza, Comprehesive Africa Agricultural Development Programme (CAADP) na Southern Agriculture Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT);

 

 • Kuweka mfumo wa uzalishaji na uendelezaji kilimo katika mazao husika kwa kutumia sera/sheria ya Ushirikiano wa kibia kati ya sekta ya umma na binafsi (Public – Private Partnership).

Ndugu Mwenyekiti,
Nachukua fursa hii tena kwa heshima kubwa mliyonipa ya kuizindua Bodi ya Wakurugenzi. Aidha ninawapongeza kwa kuteuliwa kwenu na nawatakia kazi njema ya kuleta ufanisi mkubwa katika Bodi na kwa taifa zima kwa ujumla.

Baada ya kueleza haya, sasa natamka kwamba Uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko imezinduliwa rasmi.

 

AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA.

 

 
Speeches| Publications | Agricultural Statistics | Legislation and Regulations | About us|Contact us
Copyright 2008, Ministry of Agriculture Food Security and Cooperatives All rights reserved.