The voucher system
The Web Kilimo web
Home |Budgt Speeches | Publications | Agricultural Statistics | Legislations and Regulations | Web Links
 

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA KILIMO CHAKULA NA USHIRIKA

UTARATIBU WA KUTUMIA VOCHA KUTOA RUZUKU ZA PEMBEJEO

 

JUNI, 2008

 

1. LENGO LA UTARATIBU WA KUTUMIA VOCHA KUTOA RUZUKU ZA PEMBEJEO

Malengo makuu ya utaratibu huu wa kutumia Vocha kwa pembejeo ni:

•  Ruzuku itakwenda moja kwa moja kwa wakulima walengwa ambao kamati za pembejeo za kijiji, serikali ya kijiji na mkutano mkuu wa kijiji utakuwa umewateua. Kwa utaratibu wa zamani ruzuku ilikwenda kwa makampuni na mawakala wa pembejeo.

•  Mawakala wa pembejeo watakuwa wameunganishwa na NMB hivyo kuweza kupata mikopo ya kununulia pembejeo.

Utaratibu huu utahakikisha kwamba wakulima wanafikishiwa pembejeo mapema, pembejeo zinakuwepo kwa wakati na kwamba matumizi sahihi ya pembejeo na yenye kuongeza tija na kipato cha mkulima yanakuwepo.

Malengo mengine ni pamoja na:-

 

•  Kuhakikisha kwamba kunakuwepo na ufanisi na uwazi wa kutosha katika kusimamia usambazaji wa pembejeo za ruzuku, uteuzi wa wakulima walengwa na katika kufidia ruzuku kwa wadau.

•  Kuongeza uwezo wa wasambazaji na wauzaji wa pembejeo wilayani/kata/vijiji ili kuwaongezea ufanisi wa kuhifadhi kiasi kikubwa cha pembejeo na pia kuwapa mafunzo ya kiufundi ili kumudu kazi hii ya usambazaji pembejeo.

•  Kuhakikisha na kusimamia matumizi stahili ya pembejeo yenye lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao na tija.

 

2. UTARATIBU WA UTEKELEZAJI

 

•  Ruzuku ya pembejeo itaendelea kutengwa katika bajeti ya Serikali.

•  Ruzuku ya Serikali itatolewa moja kwa moja kwa wakulima kwa vocha badala ya kulipa kwa makampuni kama ilivyokuwa hapo awali.

•  Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika itaandaa vocha kulingana na fedha zitakazotengwa na bajeti ya serikali kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo kwa mwaka husika na itatenga kiasi cha vocha kwa mikoa kulingana na mahitaji.

•  Benki ya NMB itashirikishwa katika kufanikisha matumizi ya Vocha katika upatikanaji wa pembejeo.

•  Kutakuwepo Kamati teule ya vocha ya kijiji itakayochaguliwa na serikali ya kijiji. Kamati hii itakuwa na wajumbe sita akiwepo Afisa Mtendaji wa Serikali ya Kijiji ambaye atakuwa Katibu wa Kamati. Miongoni mwa wajumbe sita, wawili ni lazima wawe wanawake. Majukumu ya kamati hii yatakuwa ni pamoja na uteuzi wa wakulima watakaonufaika na ruzuku ya pembejeo kwa njia ya vocha, kwa kuzingatia vigezo vilivyotajwa kwenye kiambatanisho 1.

•  Wakulima watakaoteuliwa kwa ajili ya kuwemo kwenye utaratibu huu wa vocha ni lazima wathibitishwe na Baraza la Kijiji. Kwa kadri inavyowezekana, mchakato huu utamuhusisha Bwana Shamba wa Kata au kijiji.

•  Baada ya wakulima wateule kuthibitishwa na Baraza la Kijiji, orodha itapelekwa kwa Halmashauri ya Wilaya, NMB, CNFA na Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika. Orodha hii itasaidia kama rejea kwa kila hatua.

•  Vocha zitachukuliwa toka wilayani na wajumbe watatu wa kamati ya Vocha ya kijiji (Mwenyekiti, Katibu na Mjumbe mmoja). Saini za wajumbe zitakuwa tayari zipo Benki ili kusaidia utambuzi na uhalali wa wajumbe.

•  Kamati ya Vocha ya kijiji itasimamia usambazaji wa vocha na itasaidia kuelewesha mahali pa kupata pembejeo na kadri inavyowezekana kusaidia upatikanaji na ufikishaji pembejeo kijijini.

•  Takwimu na taarifa zote za ugawaji vocha na uchukuaji pembejeo zitatunzwa na Katibu wa Kamati ya vocha.

•  Katibu wa Kamati atahakikisha nyaraka zote muhimu kwa ajili ya uchukuaji wa pembejeo zinawekwa sahihi na yeye ndiye atakayeidhinisha.

•  Ili kufanikisha utaratibu huu wa kusambaza pembejeo za ruzuku kwa kutumia vocha, kutakuwa na uhamasishaji utakaofanywa na Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika kwa kushirikiana na TAMISEMI ( kupitia Halmashauri zake mbalimbali pamoja na wadau mbalimbali wa kilimo).

•  Wizara itahakikisha kwamba vocha zinatayarishwa na kusambazwa hadi wilayani kanla ya msimu wa kilimo kuanza. Mikoa kwa kuhusisha wilaya zao watahakikisha Kamati za vijiji zinafanya kazi na kugawa vocha kwa uwazi kadri ya maelekezo hapo juu.

 

3. UREJESHAJI WA FEDHA

Baada ya kutoa pembejeo kwa wakulima na kupokea vocha, wakala wa pembejeo atarejesha orodha ya wakulima waliompa vocha na namba za vocha alizopokea kwa Afisa Kilimo wa Wilaya ambaye atahakiki na kuweka kumbukumbu na ndipo wakala wa pembejeo atapeleka vocha hizo benki kwa ajili ya kurejeshewa fedha zake.

4. Utaratibu na Utekelezaji wa Mfumo wa Vocha

Mfumo wa Vocha utatekelezwa katika ngazi kuu saba (7) zenye majukumu kama ifuatavyo:-

Majukumu ya Wizara ya kilimo Chakula na Ushirika (WKCU)

 

 • Kuandaa bajeti kwa ajili ya utaratibu wa vocha;
 • Kuaanda vocha kulingana na bajeti na kuainisha pembejeo za mazao mbalimbali;
 • Kuingia mkataba na Benki teule itakayoshughulikia malipo kwa mawakala wa pembejeo watakaowasilisha vocha zilizotumika kuuzia pembejeo zailizolengwa; na
 • Kuratibu utekelezaji wa mfumo mzima wa vocha;
 • Kuhamasisha wadau wa mikoa, wilaya na vijiji kuhusu utaratibu wa kutumia vocha katika kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo.

Majukumu ya Mikoa

 

 • Itapokea kutoka WKCU na kusambaza vocha zitakazogawiwa kwa kila wilaya;
 • Itaratibu utekelezaji wa mfumo wa vocha; na
 • Itahakikisha kwamba pembejeo zenye ruzuku zinatumika ipasavyo.

 

Majukumu ya Wilaya

 

 • Itawasilisha mahitaji halisi ya pembejeo katika Kamati ya Vocha ya Mkoa ambayo itaziwasilisha WKCU;
 • Itagawa vocha katika kila kijiji kulingana na idadi ya wakulima walioteuliwa kupata pembejeo zenye ruzuku;
 • Itaratibu mfumo wa vocha katika wilaya.

 

Majukumu ya Kamati ya Kijiji

 • Kamati ya Vocha ya Kijiji kwa ushirikiano na Afisa Kilimo itaainisha idadi ya wakulima na eneo litakalonufaika na mfumo wa vocha;
 • Itateua wakulima watakaonufaika na vocha zenye ruzuku ya pembejeo;
 • Kwa ushirikiano na Afisa Ugani aliyepo itahakikisha pembejeo za kilimo zinatumiwa kama ilivyokusudiwa.

Majukumu ya Makampuni

Kupeleka na kuuza pembejeo za kilimo kwa mawakala wa pembejeo katika mikoa na vituo watakavyopanga.

Majukumu ya Wakala wa Pembejeo za Kilimo

 

 • Kuhakikisha kwamba ana pembejeo za kilimo za kutosha kila wakati;
 • Kupokea vocha na fedha taslimu kutoka kwa wakulima na kuwauzia pembejeo husika; na
 • Kuwasilisha vocha zilizotumika katika Benki teule na kufidiwa kulingana na pembejeo zilizouzwa.

 

Majukumu ya Benki Teule

  Itapokea na kuhakiki vocha zilizotumika kuuzia pembejeo za kilimo kutoka kwa mawakala na kufanya malipo.

5. UFUATILIAJI NA TATHMINI

Utaratibu wa usambazaji Pembejeo kwa vocha utaandaa namna ya usimamizi, ufuatiliaji na tathmini wenye mtiririko kutokea Wizarani, Wilayani mpaka Kijijini. Wizara itatoa utaratibu wa namna ya kutoa taarifa. Vigezo vitavyozingatiwa ni kama ifuatavyo:-

5.1 Namna wakulima walengwa walivyochaguliwa kwa kadri ya vigezo kiambatanisho Na. 1 na utaratibu utakaotumika Kiambatanisho Na. 2.

•  Umadhubuti wa utaratibu wa usambazaji pembejeo:

•  Usambazaji kwa wakati.

•  Kuthibitisha kama wakulima wamepokea vocha.

•  Kuthibitisha kama wakulima wamenunua pembejeo kwa kutumia vocha.

•  Kuthibitisha kama wakulima wametumia pembejeo.

•  Kuthibitisha mazao yaliyotiliwa mbolea kwa kulinganisha na uzalishaji.

•  Kuona matatizo yaliyojitokeza.

 

6. UTENDAJI WA WAKALA WA PEMBEJEO

•  Kupima uwezo wa wakala wa pembejeo katika kutimiza usambazaji wa pembejeo ikilinganishwa na mahitaji.

•  Kutathmini takwimu za ununuzi na uuzaji wa pembejeo.

•  Kuona mtiririko wa vocha na pembejeo zilizouzwa kwa kulinganisha na orodha ya wakulima walengwa iliyotolewa na kamati ya kijiji.

•  Kutathmini utaratibu na urahisi wa kurejesha fedha za ruzuku kutoka NMB kwenda kwa wakala wa pembejeo kwa mrejesho wa vocha zilizotolewa kwa wakulima.

•  Kuona matatizo ya kiufundi katika hatua za utekelezaji wa mfumo wa vocha kwa wakala wa pembejeo.

Kiambatanisho 1:

  Vigezo vya Kuchagua wakulima wanufaika na Vocha.

  •  Wanufaika wa Vocha watachaguliwa na kamati teule ya Kijiji na kuthibitishwa na Baraza la kijiji.

•  Ili kuchaguliwa mkulima atakuwa na sifa zifuatazo:-

•  Lazima awe mkulima na mkazi wa kijiji husika.

•  Mkulima ina maana ni kaya moja.

•  Awe mkulima mdogo muhitaji wa pembejeo. Kigezo cha mkulima mdogo kitaainishwa na walengwa wa eneo husika (kijiji).

•  Vocha zitatolewa kwa pembejeo za kutosheleza ekari moja na zitatumika katika ekari moja tu.

•  Upendeleo maalum utatolewa kwa wajane na familia zinazoongozwa na wanawake.

 

Kiambatanisho cha 2:

Utaratibu utakaofuatwa wakati wa kutumia vocha.

  1. Pamoja na kutumia vocha mkulima azalishe zao/mazao yaliyopendekezwa na serikali kwa eneo husika.

2. Vocha haziruhusiwi kuhamishiwa kwa mtu ambaye hakuchaguliwa na kamati teule.

3. Matumizi ya vocha yatakuwa kwa kituo ambacho kiliandikishwa tu eg. Mkulima wa eneo moja hawezi kutumia vocha hiyo kwa eneo lingine ambako sicho kituo alichopokelewa.

4. Vocha itakuwa halali kwa msimu mmoja tu.

 

 
Speeches| Publications | Agricultural Statistics | Legislation and Regulations | About us|Contact us
Copyright 2008, Ministry of Agriculture Food Security and Cooperatives All rights reserved.