CROP TRUST YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUIMARISHA BIOANUWAI NA UHAULISHAJI WA TEKNOLOJIA ZA KILIMO NCHINI
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Stephen J. Nindi, amekutana na ujumbe kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Crop Trust ukiongozwa na Dkt. Benjamin Kilian na Bi. Joanna Purcell tarehe 01 Desemba 2025, jijini Dodoma.
Ujumbe huo umeeleza kazi mbalimbali za taasisi hiyo nchini Tanzania na katika mataifa mengine, ikiwemo kuhifadhi bioanuwai ya mazao, kuboresha mifumo ya uzalishaji wa mbegu, pamoja na kuimarisha utafiti wa kilimo kwa ajili ya kuongeza tija na ustahimilivu wa mazao.
Washiriki wengine katika majadiliano hayo ni wataalam kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), World Vegetable Center, pamoja na wawakilishi kutoka Idara ya Mafunzo na Utafiti; na Idara ya Maendeleo ya Mazao za Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo.
Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Nindi amesisitiza umuhimu wa kuimarisha juhudi za kulinda bioanuwai ya kilimo kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali. Aidha, ameomba kuongezewa nguvu katika kujengea uwezo maafisa ugani, kuimarisha vituo vya uhaulishaji teknolojia, na kuendeleza Benki ya Mbegu (Gene Bank) ili kuhakikisha upatikanaji wa vizazi bora vya mazao nchini.
Wawakilishi wa Crop Trust wamepongeza jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na kuahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kufikia malengo yaliyowekwa, hususan katika kuongeza uzalishaji na tija ya mazao kwa manufaa ya Taifa.