DKT. BITEKO ASEMA TANZANIA INA USALAMA WA CHAKULA, AWAPONGEZA WAKULIMA
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewapongeza wakulima nchini kwa jitihada zao za kuzalisha mazao kwa wingi na hivyo kusaidia nchi kuwa na usalama wa chakula ikiwa ni pamoja na kuwezesha sekta ya kilimo kuwa na mchango mkubwa katika Pato la Taifa.
Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo Julai 5, 2025 jijini Dodoma wakati akifunga Kongamano la Siku ya Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani.
“Leo sekta ya kilimo ina mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi yetu, tunazungumza mchango wa GDP wa asilimia 26, tunazungumza mazao ambayo yanatupa usalama wa chakula katika nchi yetu, nchi zingine zinahangaika kupata chakula sisi watu wetu wana uhakikia wa kupata chakula mitaani kwa sababu wakulima wamewezeshwa kufanya biashara ya kilimo, ” amesema Dkt. Biteko
Amebainisha kuwa takwimu zinaonesha utendaji wa vyama vya ushirika umeendelea kuimarika kila wakati mauzo ya nje yameongezeka. Ambapo kwa mwaka 2024/2025 jumla ya vyama vya ushirika 1,084 viliuza kahawa na tumbaku moja kwa moja nje ya nchi kiasi cha Dola za Marekani 344,800,000 ikilinganishwa na Dola za Marekani 325,500,000 kwa mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la Dola za Marekani 19,300,000.
Dkt. Biteko amefafanua kuwa Vyama vilivyopata Hati safi ya Ukaguzi kutoka Shirika la Ukaguzi la Vyama vya Ushirika (COASCO) vimeongezeka kutoka vyama 339 mwaka 2021/2022 hadi kufikia vyama 631 mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la vyama 292 ambayo ni asilimia 86.13
Aidha, Vyama vilivyopata Hati isiyoridhisha vimepungua kutoka Vyama 1,198 mwaka 2021/2022 hadi kufikia Vyama 263 mwaka 2023/2024 sawa na upungufu wa vyama 935 ambayo ni asilimia 78.
Ametoa rai kwa Vyama kuwawezesha wanawake kwa kuweka mikakati mbalimbali ili idadi ya Vyama vya Ushirika vya Wanawake iongezeke kutoka Vyama 50 vilivyopo sasa.
Licha ya mafanikio hayo katika sekta ya kilimo, Dkt. Biteko ameziagiza Wizara za Fedha na Kilimo kupatia ufumbuzi masuala ya bei ya mazao ya wakulima, pembejeo na mahitaji ya msingi ya wakulima ili kuendelea kufanya kilimo chenye tija.