Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

WASHIRIKI 1163 WATHIBITISHA KUSHIRIKI NANENANE 2025

Imewekwa: 01 Aug, 2025
WASHIRIKI 1163 WATHIBITISHA KUSHIRIKI NANENANE 2025

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli amesema kuwa washiriki wapatao 1163 wamethibitisha kushiriki katika Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa Nanenane 2025 ambayo Kitaifa yanafanyika katika Viwanja vya Nzuguni, mkoani Dodoma.

 "Kutakuwa na teknolojia za huduma za kisekta ambapo waoneshaji 753 wanatoka katika Sekta za Umma na Binafsi; washirika kutoka katika taasisi za nje ya nchi wapato 26; wajasiliamali 334; Vyama vya Ushirika 90 vikijumuisha wanachama wao pamoja na Vyama Vikuu vya Ushirika nchi nzima,” amefafanua Katibu Mkuu Mweli wakati akiongea na waandishi wa habari tarehe 30 Julai 2025, nzuguni - Dodoma. 

Maonesho ya Nanenane 2025 yanafanyika pia katika kanda saba 7 nchi nzima ambapo yatahusisha washiriki mbalimbali wakiwemo wakulima, waongezaji thamani ambao ni Viwanda, wafanyabiashara; vile vile watafiti, washirika wa maendeleo; taasisi za fedha, kampuni mbalimbali za pembejeo na zana za kilimo na wale wanaohusika na usindikaji, ufungashaji na usafirishaji.

Katika tukio lingine, Katibu Mkuu Mweli amepokea hundi yenye thamani ya shilingi millioni 50 iliyotolewa kwa udhamini wa maonesho hayo kutoka Benki ya CRDB.  Ameipongeza Benki hiyo kwa kuwa mdau muhimu wa kuchangia maendeleo katika Sekta ya Kilimo.

Wageni rasmi katika Maonesho ni Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 8 Agosti 2025  katika kusherehekea Siku ya Nanenane; ambapo ufunguzi wake wa tarehe 1 Agosti 2025 mgeni rasmi ni Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kauli mbiu ni "Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025.