HOTUBA YA KUKABIDHI MATREKTA KWA TANZANIA COTTON ASSOCIATION ILIYOTOLEWA NA WAZIRI WA  KILIMO NA CHAKULA, MHE. CHARLES N. KEENJA, MWANZA, TAREHE

28 SEPTEMBA, 2004

 

 

Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza

 

Ndugu Christopher Gachuma     -        Mwenyekiti Tanzania

Cotton Association

 

Ndugu Wageni Waalikwa,

Mabibi na Mabwana

 

          Napenda kuchukua fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi wa Mkoa na wa Tanzania Cotton association kwa Mapokezi tuliyopata tangu tulipowasili katika Mkoa wa Mwanza.  Ninapenda kutoa shukrani za pekee kwa Tanzania Cotton Association kwa kunialika kuwa mgeni rasmi katika sherehe hii ya kukabidhi matrekta kwa wanachama wenu.   Nawapongeza kwa kazi hii nzuri mliyofanya.

 

2.      Ndugu Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kutoa pongeza kwa Tanzania Cotton Assosication, kwa juhudi mnazofanya za kuendeleza kilimo cha kutumia zana bora za kisasa.  Nina taarifa kuwa baadhi yenu mmekuwa mkitoa pembejeo na kuwalimia mashamba wakulima wanaozunguka vinu vyenu vya kuchambua pamba.  Hii ni hatua nzuri ambayo itahakikisha upatikanaji wa pamba kwa vinu vya kuchambua pamba na soko la uhakika kwa wakulima.  Natoa wito kwa Ginneries zote kuiga kujenga uhusiano wa aina hii ambao siyo tu una manufaa kwa Ginneries bali pia wakulima.

 

3.      Ndugu Mwenyekiti, katika kukabiliana na matatizo yanayoikabili sekta ya kilimo na kupunguza umaskini, Wizara inaendelea kutekeleza Makakati wa Kendeleza Sekta ya Kilimo.  Dira ya Mkakati huu ni kuwa ifikapo mwaka wa 2025, kilimo chetu kiwe cha kisasa, cha kibiashara, chenye tija na chenye faida na kinachohakikisha matumizi endelevu ya maliasili zilizopo.  Lengo ni kuweka mazingira mazuri ya kuendeleza kilimo chenye faida kama msingi wa kuongeza mapato kwa wakulima na kupunguza umaskini nchini.  Uamuzi wa Tanzania Cotton Association wa kununua matrekta kwa ajili ya kuwalimia wakulima wanaozunguka Ginneries zao ni hatua muhimu sana katika kupanua maeneo wanayolima wakulima wa pamba ili kuwawezesha kuzalisha kwa wingi na kwa hiyo mnashiriki katika kutekeleza Mkakati wa Kuendeleza Kilimo.  Nawapongeza kwa hatua hiyo.

 

4.      Upanuzi wa mashamba utawawezesha wakulima kuzalisha kwa wingi na kupata mapato makubwa zaidi kwa eneo kwa kulinganisha na kilimo cha jembe la mkono.  Wakulima sasa wataweza kulima eneo kubwa kwa muda mfupi na kutumia muda utakaobaki kufanya shughuli nyingine za kuwaongezea kipato.

 

5.      Ndugu Mwenyekiti, karibu asilimia 70 ya eneo linalolimwa nchini linalimwa kwa jembe la mkono, asilimia 20 kwa jembe la kukokotwa na ng’ombe na asilimia 10 tu kwa trekta.  Serikali inahimiza matumizi ya zana bora za kilimo, hususan matrekta, ili sehemu kubwa ya shughuli za kilimo ifanyike kwa kutumia mashine badala ya nguvu ya mwanadamu.  Kutokana na umuhimu wa kutumia zana bora za kilimo, natoa wito kwa wafanyabiashara kuiga mfano wa Tanzania Cotton Association na kuagiza kwa wingi matrekta na zana nyingine za kilimo.

 

6.      Serikali tayari imeweka vivutio kwa waagizaji wa zana za kilimo kwa kuwaondolea kodi zote.  Serikali itaendelea kuwahamasisha wafanyabiashara kuagiza matrekta na zana zingine za kilimo.  Aidha, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuwavutia wafanyabiashara kuagiza zana hizo kadri haja ya kufanya hivyo itakavyojitokeza.

 

7.      Ndugu Mwenyekiti, wastani wa eneo linalolimwa mazao bado ni kati ya hekta 0.2 hadi 2 kwa mkulima.  Hili ni eneo dogo sana, na kwa hiyo halimwezeshi mkulima kuzalisha mazao ya kutosha yatakayompatia kipato cha kukidhi mahitaji yake.  Njia mojawapo ya kumuongezea kipato mkulima ni kupanua eneo analolima ili azalishe kwa wingi.  Kama wakulima wengi watapanua maeneo wanayolima na kufuata kanuni za kilimo bora cha mazao wanayolima, nina hakika tutapunguza umaskini kwa kasi kubwa kuliko ilivyo sasa.

 

8.      Kwa mfano, maeneo yanayolimwa pamba kwa sasa ni wastani wa kati ya hekta 0.5 na 2.5 na mavuno kwa hekta ni wastani wa kilo 625 hadi 750 badala ya kilo 3,000 hadi 3,500 kwa hekta zinazowezekana.  Ni lazima tubadilishe hali hii haraka, kwa kupanua maeneo yanayolimwa na kwa kufuata kanuni za kilimo bora cha pamba.  Wizara yangu itaendelea kushirikiana na wenye vinu vya kuchambua pamba (Ginners) kuhakikisha kilimo cha pamba nchini kinapanuka na kinakuwa cha tija kubwa kuliko ilivyo sasa.

 

9.      Ninapenda kuchukua fursa hii kuwahakikishia wakulima upatikanaji wa pembejeo wakulima kwa wakati na kwa kiasi cha kutosha ili juhudi za kupanua mashamba ziende sambamba na upatikanaji wa pembejeo za kilimo.  Kwa kufanya hivyo, tunatarajia tutapanua maeneo na kuongeza uzalishaji kwa eneo.  Wizara yangu itaendelea kuratibu na kusimamia upatikanaji wa mmbolea na madawa ya kilimo ili yapatikane kwa wakati na kwa bei nafuu.  Kwa mfano, Serikali imeweka ruzuku kwenye mbolea ili ipatikane kwa bei nafuu ili kuwawezesha wakulima kuitumia kwa wingi na kupata mazao mengi kwa eneo.  Wizara itaendelea kusimamia na kuimarisha utaratibu huo ili uwanufaishe wakulima wote.

 

10.    Ndugu Mwenyekiti, suala la ubora wa pamba ni muhimu ili wakulima wapate bei nzuri kwa pamba wanayolima.  Bei za mazao kama pamba, zinabadilika badilika kwenye soko la dunia.  Hata hivyo, pamba yenye ubora wa juu bado itapata bei nzuri kwa kulinganisha na pamba ya ubora wa chini pale inapotokea bei zikashuka.  Ili Mkulima apate kipato kizuri ni lazima azalishe kwa wingi na azalishe pamba yenye ubora wa juu.  Serikali itaendelea kuhamasisha wafanyabiashara ili wawekeze kwenye usindikaji wa pamba, hususan usokotaji wa nyuzi, kama njia mojawapo ya kuongeza thamani na kupunguza athari zinazosababishwa na kushuka kwa bei ya pamba kwenye soko la dunia.

 

11.    Ndugu Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, ninapenda kuwashukuru tena viongozi wa Tanzania Cotton Association kwa kunikaribisha kuwa mgeni rasmi katika sherehe ya kuwakabidhi matrekta kutoka kwa Noble Motors.  Napenda kuwahakikishia ushirikiano wangu na wa Wizara ya Kilimo na Chakula katika kupanua kilimo cha kutumia zana bora za kilimo.  Msisite kuwasiliana na Wizara yangu kila mtakapouhitaji.

 

          Nawashukuru sana.