HOTUBA YA UZINDUZI WA MRADI “DAI PESA”

 KWA MKOA WA RUVUMA ILIYOTOLEWA NA

 MHE. PIUS P. MBAWALA (MB) NAIBU WAZIRI KILIMO NA CHAKULA ILIYOFANYIKA UKUMBI WA DON BOSCO MJINI SONGEA

TAREHE 11 MACHI, 2004

 

 

-         Ndugu Mwenyekiti Maj. Gen. S.S. Kalembo,

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma;

-         Bwana Joe Burke Mkurugenzi Mkuu wa Mradi wa DAI PESA;

-         Ndugu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma;

-         Ndugu Wakuu wa Wilaya Mbinga, Songea na Namtumbo;

-         Wakurugenzi wa Wilaya Songea, na Mbinga;

-         Wakuu wa Idara za Serikali na Halmashauri;

-         Wawakilishi wa Mashirika na Miradi mbalimbali Mkoani Ruvuma;

-         Wawakilishi wa sekta binafsi;

-         Wawakilishi wa vikundi vya wakulima;

-         Wanaushirika;

-         Wasimamizi wa Mradi wa DAI PESA;

-         Mabibi na Mabwana.

 

Kwanza napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru sana viongozi wa “DAI PESA” kwa kuwaalika mhudhurie hafla hii ya uzinduzi wa mradi huu.  Aidha, nawashukuru viongozi wa “DAI PESA” kwa kunipa mimi heshima ya uzinduzi wa mradi huu mkoani Ruvuma siku ya leo.  Aksante sana kwa kunialika.

 

Mimi binafsi ninaufahamu sana mradi huu wa “DAI PESA” kwa sababu mimi ndiye niliyeuzindua rasmi kitaifa kule Dar es Salaam, mwaka jana tarehe 27 Februari, 2003.  Siku hiyo nilishirikiana na Balozi wa Marekani wa wakati ule Bwana Robert Royall.  Ila nasikitika tu kwamba mradi huu umecheleweshwa kuanza shughuli hapa kwetu mkoani Ruvuma.  Hata hivyo ingawa umechelewa kutufikia lakini leo hii mradi unaingia mkoani mwetu tujipongeze kwa hilo na nimshukuru sana Bwana Joe Burke, Mkurugenzi Mkuu wa Mradi wa “DAI PESA” kwa kutujumuisha nasi Ruvuma katika mradi huu muhimu kwa  sekta ya kilimo.

 

            Awali ya yote napenda kwanza nifafanue nini maana ya “DAI PESA”? Neno “DAI” kirefu chake kwa kiingereza ni “Development Alternatives Incorporated” ikiwa na tafsiri ya “Asasi ya Maendeleo” ambayo ndiyo inasimamia mradi wa “PESA”. Kirefu cha neno “PESA” kwa kiingereza ni “Private Enterprise Support Activities” tafsiri yake ni “Usaidiaji wa uendeshaji wa shughuli za biashara binafsi”.  Uzinduzi wa “DAI PESA” Ruvuma unafanyika leo hapa Don Bosco na sisi sote tuliokusanyika hapa ni mashahidi wa tukio hilo.

 

Mradi wenyewe unahisaniwa na Shirika la Maendeleo la Marekani yaani USAID. Utekelezwaji wa mradi DAI PESA umefanyika katika mikoa sita ikijumuisha mikoa ya Tanga, Morogoro, Iringa, Rukwa, Mbeya na kuanzia leo mkoani kwetu Ruvuma.  Mradi umeanza mwaka 2003 na utakoma mwaka 2006.  DAI PESA ni mradi wenye baraka za Serikali yetu kupitia Wizara ya Fedha ambayo iliyotia sahihi kwa niaba ya Serikali, na DAI PESA inahusisha Wizara nyingine tano.

 

Lengo la mradi wa DAI PESA ni kuunga mkono juhudi za shughuli za sekta binafsi nchini lakini lengo la Mradi SIYO KUTOA PESA kwa washiriki shughuli za mradi huu.  Kwa maneno mengine DAI PESA ni mradi wa kuwahamasisha na kuwapa maarifa washiriki mradi jinsi ya kuboresha shughuli halali za kilimo kibiashara kwa kutumia mbinu za kisasa.

 

Hivyo madhumuni ya uzinduzi wa mradi huu na WARSHA hii ni kutuelezea sisi wadau/washiriki kuhusu DAI PESA:-

1.            Jinsi mradi utakavyotekelezwa.

2.            Kujua mahitaji ya walengwa wa mradi wa DAI PESA hasa kuhusiana na mafunzo ya uwezo wa kuimudu biashara (Training needs assessment).  Vipengele vya mradi huu vitafafanuliwa na wataalam wa mradi katika warsha hii leo.

 

Hapa kwetu mkoani Ruvuma, DAI PESA itajihusisha na sekta binafsi kwenye sekta ya kilimo hususan wakulima wadogo wadogo na wale kutoka sekta ya Mali Asili yaani shughuli za uvuvi.  Hivyo katika mkoa wa Ruvuma mradi wa DAI PESA utaunga mkono sekta ya kilimo kwa kuanzia na uendelezaji bora wa biashara ya Pilipili kichaa, Korosho, Paprika, pamoja na uvuvi na uuzaji wa samaki kutoka ziwa Nyasa.  Mafanikio ya mradi wa DAI PESA unategemea sana ushirikiano wa wadau wote wakiwemo viongozi wa Serikali Kuu, Halmashauri za wilaya, pamoja na sekta zilizochaguliwa.

 

Ndugu Mwenyekiti, kama nilivyokwisha kueleza hafla hii ya leo ina lengo la kuzindua Mradi wa DAI PESA ambao utaelekeza nguvu zote katika kuendeleza shughuli za kilimo ambao sisi sote tuliomo hapa ni wadau wakubwa.  Kwa Tanzania kilimo ni ndicho uti wa mgongo wa uchumi wetu.  Katika serikali ya awamu ya tatu pamekuwepo na mageuzi makubwa sana ya shughuli za uchumi katika sekta nyingi ikijumuisha ile ya kilimo, utalii, madini, viwanda na biashara shughuli sekta ambazo zimeongeza sana mapato kwa taifa pia zimetoa ajira kwa watu wengi.  Aidha mageuzi hayo makubwa ya uchumi yameteremsha sana mfumuko wa bei asilimia 30 hadi kufikia asilimia 4 tu.

 

Aidha Serikali yetu inahimiza sana kuendeleza uzalishaji katika kilimo kama mkakati wa kukuza uchumi miongoni mwa wakulima, pia katika sekta binafsi kwa kuwa kukuza kilimo ni kunawanufaisha wananchi ambao kwa asilimia 85 huishi vijijini.  Kilimo pia huchangia asilimia 50 ya pato la Taifa (GDP).  Vile vile, kilimo ni chanzo kikuu cha ajira nchini kwa asilimia 80 kutokana na shughuli za uzalishaji na usindikaji wa mazao ya kilimo, shughuli ambazo kwa kiasi kikubwa hutupatia fedha za kigeni pia kutulisha.  Nchini kilimo sasa kinatoa mazingira mazuri kwa wawekezaji ambao shughuli zao husaidia sana kukuza uchumi wetu, hasa katika mkakati wa kuondoa umaskini (PRSP) na kuboresha maisha ya wananchi wetu kulingana na Dira ya Maendeleo (Tanzania Development vision 2025).  Dira hiyo imeweka wazi lengo la ukuaji wa sekta ya kilimo kwa asilimia 8 kwa mwaka.

 

DAI PESA ina nafasi yake katika kuunga mkono shughuli za uzalishaji unaolenga upatikanaji masoko ambayo yatakuza biashara ya mazao katika sekta ya kilimo na hivyo kuboresha maisha ya wananchi vijijini.  Ikizingatia kuwa wananchi vijijini hawana ujuzi wa kisasa katika mbinu bora za kilimo wala utaalam wa kisasa wa biashara. Wakulima pia wanahitaji aina mbalimbali za mbegu bora, upatikanaji wa pembejeo, mikopo na masoko. Aidha kilimo kinahitaji ujuzi katika uwekezaji, uzalishaji, usindikaji na hatimaye uongezaji thamani wa mazao, hasa tukikumbuka kuwa uuzaji nje wa mazao yetu yasiyosindikwa kunaudhuru uchumi wa Tanzania.  Kwa kushirikiana na DAI PESA,  serikali, vile vile sekta binafsi, pamoja na wahisani tutaleta mabadiliko makubwa ya uchumi vijijini. DAI ina mkakati wa kuleta mabadiliko hayo kwa kuwapa wakulima mafunzo katika mbinu za kisasa na kwa kuwahamasisha wakulima kupitia kujiunga katika vikundi na hivyo wanufaike na faida ya umoja katika upatikanaji wa bei nzuri kwa mazao yao watakayozalisha.

 

DAI, kwa kuwaunganisha wakulima na masoko inalenga pia kusaidia kuleta ushindani katika masoko ili kuwapatia wakulima bei nzuri zaidi.  Taarifa za masoko ni muhimu kwa wakulima kwani huwawezesha kuchagua lini na wapi, wauze kwa faida kubwa, Aidha huwasaidia wakulima kujua wapi mikopo na mitaji inapatikana, na namna ya kujitafutia pembejeo kwa wakati ili iwanufaishe wao wakulima badala ya wanunuzi wa mazao yao.

 

DAI pia itawaelimsha watumishi wa Serikali vijijini, katani, tarafani, wilayani na mkoani na hivyo kusaidia katika kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi. Washiriki wengine katika huduma za biashara ndogo ndogo, na asasi za biashara kama CCIA nao wataimarishwa.  Lengo ni kushirikisha wadau wote kusudi pasiwepo na upotevu wa rasilimali.  Tegemeo la DAI ni kuwa ifikapo mwaka 2006 mradi uwe umewaandaa wakulima kunufaika na malengo yaliyokusudiwa.  Kwa kufanya hivyo DAI itakuwa imetekeleza malengo ya USAID, DAI PESA na Ilani ya uchaguzi ya CCM (2000) inayosema, “Kilimo cha kisasa ndio ufunguo wa maendeleo ya uchumi wote wa nchi yetu.  Kilimo cha kisasa kitaongeza tija na kutoa ziada kubwa.  Kutokana na hali hiyo, CCM, katika kipindi cha miaka mitano ijayo itaendeleza juhudi zake zilizoanza miaka ya nyuma za kukienzi na kukiendeleza kilimo kwa kuhakikisha kuwa kanuni za kilimo zinafuatwa, zikiwemo zile za matumizi ya zana za kisasa na pembejeo” ……(2000:11).

 

Hata hivyo pamoja na malengo mazuri ya DAI PESA ningependa kuwashauri wahisani wa mradi wetu kwamba ni vizuri wakazielewa kiusahihi sera zetu za biashara nchini na mikakati mbalimbali ikijumuisha: Mkakati wa sekta ya kilimo au “Agricultural Sector Development Strategy (ASDS)” na Mkakati wa programu ya sekta ya kilimo au “Agricultural Sector Development Programme (ASDP)” na Sera ya kuondoa umaskini nchini, mambo ambayo pia yangeweza kuwa chanzo cha mitaji ya uwekezaji katika baadhi ya  shughuli za DAI PESA.

 

Aidha, utekelezaji wa Mradi wa DAI PESA ufanyike kupitia viongozi na watumishi mbalimbali wa kilimo (yaani DALDO na wenzake) waliopo katika wilaya husika ili kukwepa kuunda vyombo au taasisi mbadala.  DAI PESA iwatumie kikamilifu maafisa wetu wote wa ugani katika ngazi zote za uongozi husika vijijini na wilayani. Pia DAI PESA isaidie kuimarisha uwezo sio wa wataalam pekee yake bali  wawakilishi wote wa wakulima ikijumuisha madiwani na viongozi katika ngazi za kijiji na mamlaka zilizoko katika Halmashauri husika na kwa kufanya hivyo mradi wa DAI PESA utakapoisha hapo 2006 wakulima, maafisa Ugani na Mamlaka mbalimbali husika vijijini hadi wilayani watakuwa tayari wamekwisha jengewa uwezo wa kujiendeleza wenyewe.

 

Mwisho, naomba nisisitize tena kuwa “DAI PESA” ni kifupi cha maneno ya kiingereza niliyokwisha yataja hapo awali hivyo isimaanishe kuwa wakulima wetu “WATAKE AU WADAI PESA” (Demand money) kutoka kwa mradi, au USAID au Mbunge au Serikali, bali DAI PESA ni mradi wa utaratibu wa kuwapa wakulima maarifa na mbinu za  biashara pia kupewa fursa ya masoko. Aidha, ninashukuru sana DAI PESA kwa heshima niliyopewa ya kuzindua mradi huu. Tena niwapongeze sana wote mnaoshiriki katika warsha hii, na hasa viongozi na wahisani wa DAI PESA waliogharimia warsha hii ambayo naitakia mafanikio.

 

Mwenyekiti, baada ya kusema yote haya, sasa napenda kutamka rasmi kuwa, warsha hii ya DAI PESA imezinduliwa RASMI.  Aksante sana kwa kunisikiliza.