RASIMU YA HOTUBA YA MAKAMU WA RAIS

MHE. DKT. ALI MOHAMED SHEIN, WAKATI WA  MAADHIMISHO YA SIKU YA CHAKULA DUNIANI MBINGA  – OKTOBA 16, 2003

 

 

 

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Meja Jenerali Mstaafu

Said Kalembo

Naibu Waziri, Wizara ya Kilimo na Chakula,

Mhe. Prof. Pius Mbawala, (Mb.)

Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO)

Mwakilishi wa Shirika la Mpango wa Chakula (WFP)

Mwenyekiti wa Kamati ya Tele - Food

Waheshimiwa Mabalozi

Waheshimiwa Wabunge

Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya

Viongozi wa Vyama vya Siasa,

Wageni waalikwa

Mabibi na Mabwana

 

 

1.         Ndugu Wananchi, leo tuko hapa kwenye kijiji cha Maguu kuadhimisha siku ya Chakula duniani.  Naushukuru uongozi wa Mkoa wa Ruvuma, Wilaya ya Mbinga na Wananchi wa Kijiji cha Maguu kwa kukubali kubeba mzigo mzito wa kuandaa sherehe hizi.  Nawapongeza sana kwa mafanikio makubwa mliyoyapata katika kufanikisha sherehe hizi.

 

2.         Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, mnamo mwaka wa 1979 nchi wanachama wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa, linalojulikana kwa kifupi kama FAO, ziliamua kuitambua tarehe 16 Oktoba ya kila mwaka kuwa Siku ya Chakula Duniani.  Tarehe hiyo ndipo FAO ilipoanzishwa katika mwaka wa 1945.  Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yalianza rasmi kwama wa 1981.  Maadhimisho ya mwaka huu, kwa hiyo, ni ya ishirini na tatu.

 

3.         Ndugu Wananchi, kwa jumla kuna chakula kingi cha kutosha duniani cha kuwezesha kila mtu kula akashiba.  Taarifa za FAO zinaonyesha kwamba wapo watu mia nane milioni katika dunia ambao hawapati chakula cha kutosha, au, kwa maneno mengine, ambao hawali wakashiba.  Kwa upande wa Tanzania, inakisiwa kwamba asilimia 40 ya Watanzania wote hawapati chakula cha kutosha kutokana na wananchi hao kutokuzalisha chakula cha kutosha au kutokuwa na uwezo wa kujinunulia chakula cha kutosha.  Kwa kutambua hali hii, Shirika la Chakula na Kilimo duniani liliweka lengo la kupunguza idadi ya watu wasiopata chakula cha kutosha kwa asilimia 50 ifikapo mwaka wa 2015.  Hili ni moja kati ya Malengo ya Milenia ya Tatu.

 

4.         Ndugu Wananchi, madhumuni ya maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani ni kuhamasisha umma na watu wote ulimwenguni kutoa kipaumbele katika kuhakikisha kwamba watu wote Dunianiwatoto, watu wazima na wazee, wanakuwa na uhakika wa kupata chakula cha kutosha na chenye viinilishe vinavyotakiwa kwa afya bora, kwa muda wote wa maisha yao.

 

5.         Kila mwaka FAO hutoa kaulimbiu maalumu ambayo huwa dira wakati wa maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani.  Kaulimbiu ya mwaka wa 2003 ni Mshikamano wa Kimataifa Dhidi ya Njaa” (International Alliance Against Hunger”).  Kaulimbiu hii inahimiza nchi zote kuungana na kushikamana katika kutokomeza njaa duniani.