HOTUBA YA KATIBU MKUU (BW. WILFRED NGIRWA) WA WIZARA YA KILIMO NA CHAKULA  KATIKA SHEREHE YA UZINDUZI WA MBEGU MPYA  TAREHE 8 JANUARI, 2002

Mhe. Waziri wa Kilimo na Chakula, C.N. Keenja, (Mb),

Mhe. Naibu Waziri, Prof. Pius Mbawala, (Mb),

Waheshimiwa Wageni Waalikwa,

Wafanyakazi wenzagu,

Mabibi na Mabwana.

 

1.            Napenda niwakaribishe wageni wetu wote  mliofika hapa kujumuika nasi katika sherehe yetu hii fupi ya uzinduzi rasmi wa mbegu mpya zilizotafitiwa na wataalam wa Wizara hii.  Kama wengi wenu   mnavyofahamu, Wizara hii, kwa kupitia vituo vyake vya utafiti, imekuwa ikitoa aina mbalimbali za mbegu bora kwa lengo la kuboresha kilimo cha wananchi wa Tanzania. 

2.     Wote tunatambua umuhimu wa mbegu kama pembejeo yenye kipaumbele  katika kilimo.  Hivyo basi  kwa mara ya kwanza Wizara sasa imeamua kuwa na sherehe maalum ya uzinduzi wa mbegu mpya kila zitakapokuwa zimetolewa rasmi. 

3.         Lengo kuu la sherehe  yetu ya leo ni kuwatangazia wakulima wa Tanzania kuhusu kuwepo  kwa mbegu mpya bora na pia kuwatambua na kuwaenzi watafiti waliofanikisha upatikanaji mbegu hizo.  Kwa kuwa hii ni mara ya kwanza kuwa na shughuli ya aina hii vile vile tunawapongeza na kuwatambua watafiti wote waliovumbua teknolojia bora hapo miaka ya nyuma.  

4.         Mhe. Waziri nafurahi kutamka hapa kwamba mbegu utakazozizindua rasmi leo zina sifa ambazo zitawezesha kuleta mapinduzi ya kilimo nchini na pia kuboresha hali ya lishe, miongoni mwa wananchi wetu wengi hususani watoto.           

 5.         Mbegu mpya ya mahindi aina ya Uyole Hybird 615 (UH 615) inastahimili ugonjwa hatari  wa ukungu wa mahindi yaani "Grey Leaf Spot" ambao umekuwa tishio kwa kilimo cha mahindi hasa Nyanda za Juu Kusini.  Mbegu hii yenye uwezo wa kutoa tani 8-10 kwa hekta itawezesha tena kilimo cha mahindi chenye faida na tija.  

6.         Mbegu mpya za mahindi za LISHE 1 na 2 zina virutubisho bora zaidi vya protein ambavyo vitapunguza hali ya utapiamlo kwa watoto na pia kuweza kupunguza gharama za utengenezaji vyakula vya mifugo.    Mbegu hii ina uwezo wa kutoa tani 8-10 kwa hekta. 

7.         Mbegu ya mahindi aina ya SITUKA 1 na 2 zitaweza kuleta mageuzi makubwa katika kilimo nchini.  Mbegu hizi, siyo tu zinavumilia ukame kwa kiasi kikubwa sana, bali pia zinastawi kwenye udongo wenye rutuba ndogo na kuweza kutoa mavuno ya tani 3 hadi 4 kwa hekta.  Hii ni habari njema sana kwa wakulima wetu.  

8.                 Aidha mbegu mpya za mpunga za TXD 85 na TXD 88, zina sifa ya kuwa na ladha nzuri na pia kutoa mavuno mengi ya tani 6-8 kwa hekta. 

9.                 Mheshimiwa Waziri na Wageni waalikwa kazi kubwa iliyo mbele yetu ni kuhakikisha mbegu hizi zinazalishwa kwa wingi ili ziweze kuwafikia wakulima katika muda mfupi ujao. 

10.               Sote tunafahamu kuwa shughuli za utafiti wa kilimo huchukua muda mrefu na hugharimu fedha nyingi.  Kwa kuwa utafiti ni mojawapo ya majukumu muhimu sana ya Wizara, basi tutahakikisha tunatenga fedha za kutosha kuendesha utafiti na vile vile tutashirikisha kikamilifu wadau wote na wahisani katika suala hili.  

11.                 Mkakati wa kuendeleza kilimo nchini (ASDS) unaainisha maeneo yatakayopewa kipaumbele katika utafiti  na jinsi wadau mbalimbali watakavyohusishwa katika uchangiaji wa gharama za utafiti.  Miradi na programu mbalimbali zinazoandaliwa kati ya Wizara na Wahisani  zinaweka mkazo kwenye kuboresha huduma zetu ikiwemo utafiti. 

12.                Kwa kumalizia ningependa nitoe pongezi zangu binafsi na pia kwa niaba ya uongozi wa Wizara kwa wataalam wetu kwa kazi zao nzuri za kubuni teknolojia bora za kuendeleza kilimo nchini.  Tunatambua jinsi kazi hizo zinavyofanyika katika mazingira magumu.  Nawaomba waendeleze moyo huo wa uzalendo wakati Wizara inaendelea  na jitihada mbalimbali za kuboresha mazingira yao ya kazi pamoja na maslahi yao. 

13.            Zawadi wanazopewa baadhi yao leo ni kielelezo cha Wizara kutambua  na kuenzi jitihada hizo.  Aidha ieleweke kuwa zawadi hizo watakaozipokea ni kwa niaba ya wote waliohusika.  Wizara vile vile inatambua michango ya Idara na Taasisi zake.

14.            Ningependa pia niwashukuru wote wale wanaoshirikiana na Wizara hii kwa hali na mali kuendeleza kilimo chetu.  Napenda kutambua michango ya mashirika, Taasisi na nchi zifuatazo:- FAO, Benki ya Dunia, JICA, NORAD, DANIDA, DFID, Netherlands, USAID, GTZ, Ireland AID, EU, SACCAR, ASARECA, CIAT, CIMMYT, ICRISAT, ICRAF na IRRI.

15.            Nategemea kuwa kufanyika kwa sherehe hii leo pamoja na utoaji wa vyeti na zawadi itakuwa ni changamoto kubwa kwa watafiti wote nchini kuongeza bidii katika kazi zao.  Sambamba na hili nategemea wakulima wetu watazitumia mbegu hizi mpya ili wanufaike na zile sifa nzuri nilizozitaja hapo awali.

            Nawashukuru kwa kunisikiliza.