HOTUBA YA WAZIRI WA KILIMO NA CHAKULA MHE. C.N. KEENJA (MB.) KWENYE MKUTANO WA TATU WA WASHIKADAU WA ZAO LA MKONGE MJINI TANGA AGOSTI 25, 2001

 

-                     Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Benjamin W. Mkapa ambaye ndiwe Mwenyekiti wa Mkutano huu

-                     Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Waziri

-                     Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa

-                     Waheshimiwa Wabunge

-                     Prof. A.S. Kauzeni Mwenyekiti wa Bodi ya Mkonge Tanzania

-                     Ndugu S. Shamte Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Mkonge Tanzania

-                     Washikadau wa zao la mkonge

-                     Wageni Waalikwa

-                     Mabibi na Mabwana

 

Mheshimiwa Rais wetu, awali ya yote ningependa kuchukua nafasi hii kwanza, kukushukuru sana, wewe binafsi Mheshimiwa Rais, kwa kukubali mwaliko wa washikadau wa zao la mkonge na kuja hapa Tanga kushiriki nao, katika mkutano wao huu wa mwaka.  Karibu sana utufungulie mkutano huu.  Aidha, tunashukuru sana pia kwa kukubali kubaki mkutanoni, ili kushiriki majadiliano kwa lengo la kufufua zao la mkonge.  Akhsante sana.  Pili, ningependa kuchukua nafasi hii pia kuwakaribisha wageni wote na washika dau walioalikwa kuhudhuria kikao hiki, ambao pia, tunatarajia watachangia mikakati madhubuti ya kufufua zao la mkonge, hivyo tunafurahi sana kuwa na wote hapa mkutanoni Tanga.

 

Mheshimiwa Rais, tunatiwa moyo sana kuona Kiongozi wetu Mkuu na Wasaidizi wako wa uongozi wa juu wa taifa letu, kwa kujihusisha kwa karibu zaidi na sekta ya Kilimo na Mifugo.  Kwanza, wewe mwenyewe Mheshimiwa Rais, ulifungua mkutano wa washika dau, wa zao la korosho kule Masasi mwezi Juni 2000.  Mnamo Desemba 2000, pia ulifungua mkutano na kuzindua Chama cha Kilimo na Mifugo kule Arusha.  Halafu, mwezi Machi tarehe 24 na 25, 2001 ulikuwa Mwenyekiti wa mkutano wa washika dau wa sekta ya Kilimo, Dodoma.  Tunapenda kukuhakikishia kwamba, mapendekezo yaliyotokana na mikutano hiyo yameshaanza kufanyiwa kazi na Wizara ya Kilimo na Chakula, pia taasisi zinazohusika.  Pili, Makamu wa Rais Marehemu Dr. Omari Ali Juma alikuwa Mwenyekiti kwenye mkutano wa sekta ya Pamba mjini Mwanza.  Tatu, Waziri Mkuu, Mhe. Frederick T. Sumaye (Mb.) naye alifungua kikao cha sekta ya Kahawa, mjini Moshi mwaka huu.  Hii yote inaonyesha jinsi gani uongozi wa juu, umedhamiria kuwahamasisha washika dau wote katika kuendeleza kilimo ikiwa sekta kiongozi.  Sote wakulima tumefarijika sana.

 

Mheshimiwa Rais, Wizara ya Kilimo na Chakula, tayari imekwishatayarisha “Mkakati wa Kilimo” yaani “Agricultural Sector Development Strategy” ambao utatumiwa katika kutekeleza sera za kilimo.  Hapa ningewaomba washika dau wote wa zao la mkonge, kuisoma sera hii kwa makini, ili Wizara ya Kilimo na Chakula ipate maoni yao.  Sambamba na sera hiyo, Wizara yangu pia imeshaziagiza Bodi zote za mazao mbalimbali kutayarisha mipango yao ya miaka mitano toka mwaka huu hadi 2005.  Mipango hii inategemewa kuwasilishwa serikalini ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu lakini kabla yake inatakiwa ijadiliwe na washikadau pamoja na Bodi za wakurugenzi husika.

 

Aidha, wakati Wizara yangu inaendelea kuboresha programu na mikakati madhubuti yenye kubaini aina ya vivutio na sera za kodi kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje wa zao la mkonge, ninapenda kutumia nafasi hii kuwakaribisha washika dau wote kutoa maoni yao, ili Bodi ya Mkonge iyajumuishe wakati inakamilisha mpango wake.

 

Mheshimiwa Rais, Leo tumekusanyika hapa kuzungumzia zao la mkonge.  Zao la wakati wa ukoloni lilikuwa maarufu kwa jina la “White Gold” yaani “Dhahabu Nyeupe” umaarufu huo uliendelea mpaka kwenye miaka ya 1970.  Wakati huo mkonge ulilimwa katika mashamba ya hekta 475,000.  Lakini baada ya hapo zao hili limepungua sana ambapo leo tunazalisha jumla ya tani 20,000 tu yaani asilimia 2 tu katika mashamba yenye eneo la hekta 180,000.  Hiki ni kiasi kidogo mno ikilinganishwa na kiasi tulichoweza kuzalisha mwaka 1964 ambapo zao lilifikia tani 230,000.  Kushuka huko kwa uzalishaji kumeathiri nchi kwa namna mbalimbali, maana licha ya kupoteza ajira na mapato, mikoa ya Tanga na Morogoro ambayo ilikuwa imeneemeka kwa ajili ya ukulima wa mkonge, imepunguza umaarufu wao mkubwa.  Leo hii nchini, bidhaa bandia, zimechukua zaidi ya asilimia 50 ya soko la mkonge.  Zao la mkonge pia limekuwa likitegemea zaidi ya asilimia 75 soko la Ulaya Magharibi na Marekani ambapo matumizi ya katani yamepungua sana.

 

Mheshimiwa Rais, Serikali ilipoanzisha sera mpya za uchumi mwaka 1985 kwa kiasi fulani ilifanikiwa kufungua milango kwa kukaribisha wawekezaji kwa kuuza baadhi ya mashamba yaliyokuwa yanamilikiwa na Mamlaka ya Mkonge (TSA).  Mpango huu. Ilipofikia mwaka 1998, zao la mkonge limekuwa linamilikiwa na sekta binafsi kwa asilimia 100.  Hata hivyo, uzalishaji mkonge umekuwa ukipanda taratibu mno, maana hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2000 uzalishaji umeongezeka hadi tani 20,489 ukilinganisha kutoka tani 17,340 zilizozalishwa mwaka 1997.  Lakini Serikali inategemea kwamba wawekezaji wa ndani na nje, watatumia kwa kikamilifu dhamana na vivutio, ambavyo serikali itakuwa inavitoa mara kwa mara kwa kuendeleza Kilimo cha Mkonge.  Katika “Mkakati wa kuendeleza kilimo,” Kuinua ukuaji wa mazao ya biashara.  Kutoka asilimia 6.8 mwaka wa 2000 hadi asilimia 9 kwa mwaka,  ifikapo mwaka wa 2005, ni pamoja na uendelezaji wa zao hili la mkonge.

 

Mheshimiwa Rais, Hivi karibuni mimi mwenyewe na Naibu Waziri wangu, Prof. Mbawala (Mb.) tumepata nafasi ya kutembelea baadhi ya mashamba na viwanda vinavyosokota kamba.  Tumejionea wenyewe juhudi za baadhi ya wawekezaji, pia mapungufu, ambayo tutayafanyia kazi, kwa kuyarekebisha.  Nimeridhika na juhudi, ambazo zimeanza kufanywa katika upandaji na hasa kuwahusisha wakulima wadogo wadogo kwenye zao la mkonge (outgrowers). Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wadogo wadogo wanaweza kulima mkonge kwa mpango huo, kwa hiyo tunapendekeza wakulima hawa, wahusishwe kikamilifu na wawe na mkakati kamili wa kuanzisha upanuaji wa kilimo hicho.  Ili kuongeza uzalishaji wizara itaendelea na harakati za kuendeleza kuhimiza uanzishaji wa mitaji midogo (micro-finance) ya kugharamia shughuli za kilimo ubia, kati ya wakulima wakubwa na wadogo, pia kuhamasisha Benki zetu nchini, ziwe na Idara ya Mikopo kwa ajili ya Kilimo.  Lingine Mheshimiwa Rais, ni kwamba sekta hii ina uwezo mkubwa wa kutengeneza bidhaa ambazo zinaweza kutumika humuhumu nchini, na hata nchi za nje.  Bidhaa kama kamba, mazulia na magunia yanaweza kabisa kushindana na bidhaa zozote kutoka nje.

 

Hivyo basi ni muhimu tukajadili ni jinsi gani tunaweza kuongeza juhudi zetu katika kusindika malighafi ya mkonge na kuweza kuuza bidhaa zake badala ya singa za mkonge peke yake, kama ilivyo leo hii, ambayo ni asilimia 2 tu ya matumizi ya zao zima la mkonge.  Kwa kuuza bidhaa za aina nyingi zaidi mkonge utaweza kuchangia zaidi katika pato la Taifa pia kupiga vita umaskini.

 

Mwisho Mheshimiwa Rais, naomba tena kutoa shukrani zangu kwako, kwa kukubali kuwa Mwenyekiti wa mkutano wa leo na ninapenda kuchukua fursa hii, kwa heshima na taadhima, kukukaribisha ili uweze kutufungulia kikao chetu hiki.