HOTUBA YA MHESHIMIWA PROF. P.P. MBAWALA (MB), NAIBU WAZIRI WA WIZARA YA KILIMO NA CHAKULA,

WAKATI WA KUFUNGUA WARSHA YA VIONGOZI WA VYAMA VYA AKIBA NA MIKOPO (SACCOS) MJINI NAMTUMBO MKOANI RUVUMA TAREHE 10 MACHI, 2004

 

 

 

-         Ndugu Mwenyekiti, wa Warsha,

-         Maafisa Ushirika

-         Viongozi wa Chama Tawala cha CCM

-         Viongozi wa SACCOS Washiriki Warsha

-         Wageni Waalikwa

-         Mabibi na Mabwana

 

 

Awali ya yote napenda kuwapongeza na kuwakaribisha viongozi wote wa vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo kwa kuchaguliwa kushiriki warsha hii muhimu hapa Namtumbo ambako ni Makao Makuu ya Wilaya yetu mpya.

 

Aidha, nami nitoe shukrani zangu za dhati kabisa kwa Waandalizi wa Warsha kwa kunialika mimi binafsi nikiwa Mbunge wa Wilaya ya Namtumbo kuifungua Warsha hii. Nasema aksante sana kwa heshima hii.

 

Ndugu Mwenyekiti, warsha hii ina umuhimu wake katika masuala ya uendeshaji makini wa shughuli za Vyama vya Akiba na Mikopo au SACCOS. Ujenzi wa Ushirika katika uchumi wa soko nchini mwetu unatiliwa maanani sana hata katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2000 (UK.36) inayotamka:-

 

Chama cha Mapinduzi kinatambua kuwa Ushirika ndicho chombo cha uhakika cha ukombozi kwa wakulima, wafugaji na wavuvi wadogo wadogo. Ushirika wa kuweka na kukopa uliwekewa mkazo kwa sababu ndicho chombo mwafaka katika kutatua matatizo ya maendeleo ya wanachama wake. Kwa mfano upatikanaji wa pembejeo na mikopo.

 

Hivyo warsha hii ni moja ya mikakati ya mafunzo ya kuuimarisha ushirika. Kwa kupitia mafunzo ya warsha hii, tunaimarisha Elimu ya Ushirika kuhusu kuboresha fani ya menejimenti, uchumi na udhibiti wa fedha kwa Halmashauri, watumishi na wanachama juu ya vyama vyao. Uendeshaji wa SACCOs kwa umakini sio tu mipango wa kupanua idadi na wanachama wa vyama bali pia kwa usimamizi bora wa vyama hivyo.

 

Taarifa zilizoko kitaifa zinabaini kuwa matatizo mengi ndani ya ushirika yanafanana. Ingawa juhudi za kukabiliana nayo yanategemea na mwamko na uelewa wa wanaushirika wenyewe mahali walipo. Kwa kifupi baadhi ya matatizo ni kama ifuatavyo:-

 

(1)               Vyama kushindwa kutoa huduma kwa wanachama wao za madawa na pembejeo kwa wakati, na kwa viwango vinavyotosheleza mahitaji kitaalam.

 

(2)               Vyama vikuu haviwajibiki ipasavyo kwa kuvilipa ushuru wake mapema vyama vya msingi. Matokeo vinatumia malipo ya fedha za mkulima kugharimia uendeshaji wake.

 

 

(3)               Wanachama, wahalmashauri na watendaji wa Vyama vya ushirika hawapati elimu ya kutosha kuhusu ushirika na shughuli zao kama ilivyo katika moja ya nguzo za ushirika.

 

(4)               Halmashauri kushindwa kusimamia watendaji kuandika na kufunga vitabu vya mahesabu kwa wakati kisha kuviwasilisha kwa wakaguzi kwa muda unaotakiwa kwa mujibu wa sheria. Aidha, wanachama hawasomewi mahesabu yao yaliyokaguliwa kwa wakati.

 

(5)               Wizi na udanganyifu ambao unafanywa na watendaji wasio waaminifu ndani ya ushirika umedhohofisha sana nguvu za ushirika katika mikoa na nchi kwa ujumla.

 

(6)               Vyama vya ushirika havikaguliwi mara kwa mara hivyo kukosa usimamizi wa karibu wa sheria na kanuni za ushirika katika vyama hivyo.

 

(7)               Wanachama na viongozi wa vyama kutoheshimu misingi ya kidemokrasia wakati wanachagua/kubadilisha viongozi katika vyama vyao.

 

(8)               Vyama havina mitaji ya kutosha kutokana na kuwa na wanachama wachache na kuweka viwango vya chini vya hisa zao.

 

(9)               Wananchi hukatishwa tamaa na Vyama vya Ushirika dhaifu na hivyo idadi ya wanachama wanaojiunga na vyama vya ushirika haiongezeki na hata hisa za wanachama vyamani haziongezeki.

 

(10)           Viongozi na watendaji wababaishaji hujipenyeza katika Vyama vya ushirika na kusababisha gharama kubwa za uendeshaji na usimamizi bila kujali maslahi ya wanachama.

 

Ndugu Mwenyekiti, sera ya maendeleo ya ushirika inatambua fika kuwa vyama vya ushirika ni taasisi binafsi lakini serikali haiwezi kupuuzia matatizo haya. Aidha ni jukumu la wanachama wenyewe na hasa ninyi viongozi kuhakikisha matatizo kama haya hayajirudiirudii na hasa katika asasi za fedha kama SACCOs. Baadhi ya mikakati ya kukabiliana na matatizo ni kukuza upeo wa elimu na mafunzo ya ushirika kama tutakayopata katika warsha hii. Ili kufanikisha azma hii SACCOs sherti itenge asilimia ya fungu fulani la mapato ya mwaka kwa ajili ya elimu na mafunzo. Katika SACCOS lazima wanachama waweke fedha daima, waongeze viwango vya mafungu (hisa) na kukopa ili kutunisha mapato ya SACCOs yatakayotokana na riba.

 

Mafanikio ya SACCOs yatatokea haraka ikiwa Wanachama watajenga tabia ya kuweka akiba kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya wanachama kwa wakati uliopo na siku za usoni. Uwekaji fedha katika SACCOs itasaidia wanachama kupata mikopo tena kwa masharti nafuu ukilinganishwa na upatikanaji wa fedha hizo toka Benki kwa masharti magumu yanayotolewa au asasi nyingine za fedha zinazotoa riba kati ya asilimia 12 na asilimia 24, tozo ambalo wananchi au wakulima wengi wenye kipato kidogo wanashindwa kutimiza masharti hayo.

 

Katika mkakati wa kupata mitaji zaidi ya kuwapatia wanachama wa SACCOs kwa masharti nafuu, SACCOs ziwe na uhusiano wa karibu sana na SCCULT ambako serikali imekipa fungu la fedha linalotumika kutoa mikopo kwenye SACCOs ambazo zinahitaji mikopo hiyo kwa matumizi ya wanachama wao. Kadiri ya taarifa zilizoko hadi kufikia 31 Desemba 2003, jumla ya Vyama vya Akiba na mikopo nchini ilikuwa 1,264 vyenye wanachama 163,732. Hisa shilingi bilioni 11.3 na Amana shilingi bilioni 3.1 ambapo mikopo ya shilingi 28.5 ilikuwa imetolewa. Haya ni baadhi ya mafanikio makubwa yaliyofikiwa ya kuweka Akiba mara kwa mara ili kujijengea uwezo wa kuwekeza katika shughuli za uchumi za wanachama.

 

Pamoja na mafanikio niliyoyataja vyama hivyo itabidi viendelee kuwa na sifa za kukopesheka, maana yake viweze kutumia fedha hizo kwa kukopesha wanachama wake na kurejesha mikopo kwa wakati bila ya ubabaishaji, ili fedha hizo zizunguke kwa kuwasidia wengine. Tegemeo langu warsha hii itawezesha pia kuwapa uwezo wa kuendesha na kusimamia shughuli za SACCOs kwa makini kusudi SACCOs zenu ziweze kuwa vyama vya Akiba na Mikopo ambavyo ni endelevu na zinazoelekeza rasilimali zao adimu kwenye shughuli za manufaa kwa maslahi ya wanachama. Mkitaka SACCOs zenu zizidi kushamiri inabidi kuwepo na nidhamu ya matumizi mazuri ya mikopo inayotolewa. Urejeshaji mikopo hiyo inayotolewa uwe kwa asili mia moja kusudi wengine waweze kuwa na mitaji ya kukidhi mahitaji yao, iwe katika shughuli za kilimo,biashara na shughuli zingine, mfano ujenzi wa nyumba bora au ununuzi wa pembejeo au hata kulipia ada za shule.

 

 

Mwisho, Mwenyekiti naomba nirudie tena kuwashukuru kwa kuja kuhudhuria warsha hii kwa lengo la kutoa huduma bora katika SACCOs zenu. Niwapongeze tena waandaji wa warsha hii ambayo naitakia mafanikio makubwa.

 

Baada ya kusema hayo mafupi sasa napenda kutamka rasmi kuwa warsha yenu imefunguliwa rasmi. Aksanteni kwa kunisikiliza.