HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA, YA KUFUNGUA MKUTANO WA TATU WA WASHIKA DAU WA ZAO LA KOROSHO, SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA, PWANI, 29 SEPTEMBA 2001.

 

Mhe. Nicodemus Banduka, Mkuu wa Mkoa wa Pwani,

Mhe. Charles Keenja, (Mb), Waziri wa Kilimo na Chakula,

Mhe. George C. Kahama, (Mb), Waziri wa Ushirika na Masoko,

Waheshimiwa Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wabunge

Mheshimiwa Kitwana Kondo, Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania,

Washika Dau wa zao la Korosho,

Mabibi na Mabwana.

 

Nachukua nafasi hii kuwakaribisheni nyote katika mkutano huu. Kwa kuwa mkutano ni wa siku moja na unajumuisha Washikadau wengi ni vyema tukajiwekea nafasi ya kutosha kusikiliza na kujadili kwa kina mada, zilizoandaliwa.

 

Mkutano huu wa leo ni muhimu sana siyo tu kwa Washikadau mliojumuika hapa, bali ni kwa wananchi wote wa Tanzania.  Hii inatokana na ukweli kwamba katika miaka ya karibuni zao la korosho limechangia kipato kwa maelfu ya wananchi hususani wa Mikoa ya Kusini na Pwani na pia kuliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni. 

 

Katika mazao ya biashara zao la Korosho linachuana na zao la kahawa ambalo liliongoza kwa muda mrefu katika kulipatia taifa mapato.  Katika mwaka wa 1997/98 zao la kahawa liliingiza kiasi cha dola za Kimarekani 108.7 milioni na korosho iliingiza dola 80.94 milioni, Mwaka wa 1999/2000 zao la korosho limeongoza usukani kwa kuliingizia Taifa fedha za kigeni dola 123.8 milioni ukilinganisha na dola 73.6 milioni tu kwa zao la kahawa.  Bei ya kahawa kwenye soko la dunia imeshuka sana, na ni vyema tukajizatiti kuongeza uzalishaji wa korosho ambapo kwa sasa soko lake ni nzuri.

 

          Pamoja na mafanikio ambayo yamejionyesha katika zao la korosho miaka ya karibuni, kuna matatizo ambayo yameendelea kutishia maendeleo ya sekta ya korosho. Matatizo haya ni pamoja na kutokuwepo na uhakika wa soko, bei isiyotabirika, mfumo mbovu wa upatikanaji pembejeo na uwezo mdogo wa ubanguaji nchini.  Hivyo basi kuyumba katika ufanisi wa sekta ya korosho kutaleta madhara makubwa katika vita yetu ya kuondoa umasikini nchini na pia kuathiri uchumi wa nchi yetu.

 

          Aidha licha ya kwamba tuna viwanda 12 vyenye uwezo wa kubangua tani 113,000 viwanda hivi havifanyi kazi.  Vile vile wawekezaji wa sekta binafsi katika kubangua korosho bado ni wachache.  Hadi sasa tunao wawili tu ambao viwanda vyao vina uwezo wa kubangua tani 9,500 tu.  Kwa kuwa zao la korosho linaongoza katika kuliingizia nchi yetu fedha za kigeni ni dhahiri kwamba iwapo matatizo haya hayatapatiwa ufumbuzi mapema yatasababisha ufanisi katika sekta ya korosho kuyumba na kuathiri uchumi wa nchi yetu na jitihada zetu za kuondoa umaskini.

 

Ni mategemeo yangu kuwa baada ya mkutano huu matatizo mengi  ambayo yamekuwa yanakwamisha maendeleo ya zao la Korosho hususan katika msimu unaokwisha yatapatiwa ufumbuzi kwani mengi ya majibu ya matatizo hayo yako ndani ya uwezo wenu nyinyi kama Washikadau.

 

Hata hivyo mikutano na warsha nyingi kuhusu kilimo zimefanyika nchini bila kuleta mafanikio ya kutosha.  Napenda kuona mkutano huu uwe tofauti.  Hivyo basi ningependa baada ya kusikiliza mada zitakazotolewa majadiliano yatakayofuata yalenge katika maeneo yafuatayo ambayo ni ya msingi na lazima yawekewe mikakati thabiti ya kuendeleza sekta ndogo ya korosho.

 

Kwanza, kuna umuhimu kwa washika dau wote tuliopo hapa kufanya tathmini ya kina kuhusu matatizo ya zao la korosho nchini na kupendekeza hatua za msingi za kuchukuliwa. Hatua hizo ziainishwe na kujulikana zichukuliwe na nani, na kwa muda gani.  Katika mchanganuo wa nani anapaswa kufanya nini, itabidi majukumu ya vyombo mbalimbali vinavyoshughulikia zao la korosho yawekwe bayana, kwa lengo la kila chombo kuelewa mipaka yake.   Vyombo hivyo ni pamoja na Bodi ya Korosho, Bodi yake ya Wakurugenzi, Mfuko wa Uendelezaji Zao la Korosho (CIDEF), Vyama vya Ushirika, Umoja wa Wafanyabiashara wa Korosho –“Cashewnut Association of Tanzania CAT”, Wauzaji Korosho Nje (Exporters), Watafiti na pia Halmashauri za wilaya/Miji zinazolima korosho.   Majukumu na wajibu wa Serikali Kuu nayo ni vyema yakaeleweka wazi kwa washikadau wote.

 

Pili, takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa kiwango cha juu cha korosho kilichowahi kuzalishwa nchini ni tani 145,000 katika msimu wa mwaka 1973/74.  Uzalishaji huu ulishuka kwa kasi kubwa hadi kufikia tani 16,500 katika msimu wa 1986/87.  Juhudi na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali kwa lengo la kufufua uzalishaji wa zalo hili katika miaka ya tisini, zimezaa matunda mazuri ambapo uzalishaji wa korosho umepanda mwaka hadi mwaka na kufikia kiwango cha tani 135,000 msimu wa 2000/2001.  Kama tutajizatiti kikamilifu upo uwezekano wa uzalishaji wa korosho nchini kufikia tani 400,000 ifikapo mwaka wa 2008.  Kwa hiyo pamoja na dalili hizi nzuri za kuongezeka kwa uzalishaji wa zao hili hadi msimu uliopita, bado kuna sababu za msingi mkutano huu kuangalia na kujadili hatua za kuchukua ili uzalishaji uendelee kuongezeka na wakulima wetu wanufaike zaidi.  Hii ni pamoja na kuweka mifumo endelevu ya kutathmini mahitaji ya pembejeo kwa kila msimu na mitandao ya uhakika ya uagizaji na usambazaji wake.  Hali iliyojitokeza msimu huu ya kuyumba bei na korosho kubakia mikononi mwa wakulima kwa muda mrefu bila kuuzwa ni tishio kubwa kwa ukuaji wa zao hili, na ni vizuri tukaijadili pamoja kwa makini na kujiwekea malengo ya muda mfupi na mrefu ya jinsi ya kukabiliana na hali ya namna hiyo inapotokea, pamoja na kuondoa vikwazo vinginevyo vya uzaliashaji

Tatu, ikumbukwe kwamba nchi zinazozalisha korosho kwa wingi, mfano, India, Brazil na Vietnam hubangua korosho zenyewe kabla ya kuuza nje.  Kwa hiyo ni lazima mkutano huu ujadili na kutoa ufumbuzi ili wakulima wetu na taifa letu liweze kufaidika kwa: 

 

·       Kuuza nje korosho zilizobanguliwa ambazo soko lake ni kubwa zaidi na bei inayopatikana ni nzuri kulinganisha na korosho ghafi.

·       Ongezeko zaidi la thamani ya korosho, na kuwapatia ajira vijana wetu, hivyo kuongeza vipato na kuchangia katika jitihada zetu za kupambana na umaskini.

·       Kutuwezesha pia kupata bidhaa nyingine zitokanazo na korosho.

 

Katika jambo hili ni vizuri tukawa na mikakati ya muda mfupi na mrefu ambayo itatuhakikishia kuwa siku za usoni korosho zote zinazozalishwa nchini zitakuwa zinauzwa nje zikiwa zimebanguliwa.   Ubanguaji ulenge kutumia viwanda vikubwa,  vya kati na vidogo.

 

Nne, kuongezeka kwa uzalishaji wa korosho ni lazima kuende sambamba na kupatikana kwa soko la uhakika kwa zao hili. Soko la zao hili ni pamoja na kuhamasisha soko la ndani kwa matumizi ya zao hili pamoja na bidhaa zake. Kwa mfano, iwapo nusu ya idadi ya Watanzania wote watakula angalau kilo moja tuu ya korosho iliyobanguliwa kwa mwaka, karibu nusu ya korosho ghafi inayozalishwa nchini itakuwa imetumika humu humu nchini.   Aidha, korosho zitumike kwa wingi zaidi katika mahoteli ya kitalii, tafrija na sehemu mbalimbali za vinywaji.  Inabidi pawe na juhudi za makusudi za kuhamasisha upanuzi wa soko la ndani la zao hili.  Aidha ni muhimu tuainishe masoko mengine ya nje badala ya kutegemea masoko machache kwa korosho ghafi tunazouza sasa. Ni mategemeo yangu kuwa mkutano huu utajadili suala la soko la korosho zetu kwa mapana na marefu yake kwani matatizo ya soko yaliyojitokeza msimu wa 2000/2001 yametufungua macho na kutuonyesha ukubwa wa matatizo ambayo yako mbele yetu.

 

Tano, kwa vile wote tunaelewa kuwa upo uwezekano wa kutumia bidhaa nyingine zinazotokana na zao la korosho kuliko tunavyofanya hivi sasa, itakuwa ni jukumu la mkutano huu kutoa na kujadili mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa mara moja ili bidhaa hizo ziweze kutumika kwa ajili ya soko la ndani na la nje.  Lazima watafiti wetu wachunguze zaidi matumizi mbalimbali ya zao hili.

 

Sita, kwa zao lolote kuwa na mafanikio ni lazima kuwepo na utafiti wa kina ambao utasaidia kupata mbegu bora, miche bora na mbinu mbalimbali za kupambana na magonjwa na wadudu. Kwa hiyo ni muhimu kwa Mkutano wetu kutafuta njia endelevu za kupanua, kueneza na kugharamia utafiti wa kilimo cha korosho na bidhaa zinazoweza kutengenezwa kutokana na korosho, pamoja na shughuli za ugani katika zao hili.

 

Saba, katika jitihada za kuhamasisha uzalishaji, ubanguaji na biashara ya zao la korosho kwa ujumla ni muhimu kwa mkutano huu kutoa mapendekezo ya aina ya vivutio na mazingira yatakayowavutia wakulima na wawekezaji wa ndani na nje katika kilimo na ubanguaji wa korosho. Hata hivyo ni vyema pia mkapendekeza jinsi ambavyo wawekezaji hao wataweza kusimamiwa ili watimize masharti ya mikataba na taratibu zilizowekwa.

 

Mwisho, ingawa yapo mambo mengi ambayo yanatakiwa kuzungumzwa kuhusu zao la korosho, lakini ningependa haya niliyoyataja tuyazungumze na kuhakikisha tunayatolea majibu na tunapotoka hapa kila mmoja wetu awe ameelewa njia iliyo sahihi ya kuyashughulikia na wajibu wake.

Baada ya kusema haya machache, sasa napenda kutamka kuwa mkutano wa tatu wa washika dau wa zao la korosho umefunguliwa rasmi.

 

 

AHSANTENI SANA