HOTUBA YA MHE. CHARLES N. KEENJA (MB.) YA KUMKARIBISHA MGENI RASMI KUHITIMISHA MAADHIMISHO YA NANENANE, 2002 MOROGORO, 08 AGOSTI, 2002

 

            Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kuchukua muda huu kukushukuru sana kwa kukubali kutenga muda wako kuja hapa Morogoro kuwa mgeni wetu rasmi katika maadhimisho ya Nane Nane 2002.  Nakushukuru pia kwa hatua mbalimbali unazochukua kuhimiza kilimo na upatikanaji wa mahitaji ya kilimo.  Tunathamini sana mchango wako na ule wa viongozi Wakuu wa Taifa.  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Benjamin William Mkapa na Makamu wa Rais, Mhe. Ali Mohamed Shein.

 

2.         Mheshimiwa Mgeni Rasmi, maadhimisho ya Nane Nane yanafanyika kwenye viwanja hivi kwa mara ya tatu mfululizo kutokana na uamuzi uliofanywa na TASO wa kujenga eneo hili, ili liwe kituo cha Kanda ya Mashariki cha Maadhimisho ya Nane Nane.  Kama ulivyojionea mwenyewe, hatua kubwa imepigwa katika kuelekea kwenye lengo la kuvijenga viwanja hivi:

 

  • Hati ya kumiliki eneo hili imepatikana na namshukuru Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Alhaj Mussa Nkhangaa, kwa juhudi zake zilizowezesha kupatikana kwa hati hiyo.

 

  • Idadi ya washiriki imeongezeka kutoka 120 mwaka jana hadi 158 mwaka huu.

 

  • Washiriki wengi wamejenga mabanda imara na ya kudumu na ningependa kuwapongeza Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Maji na Maendeleo ya Mifugo, Bodi ya Chai Tanzania na wadau wao na Wizara ya Kilimo na Chakula kwa kazi nzuri na kubwa ya kujenga majengo ya kudumu na huduma nyingine za kuboresha maonyesho.

 

  • Maadhimisho ya Nane Nane yanaambatana na maonyesho ya kilimo.  Wizara ya Kilimo na Chakula, Wizara ya Maji na Maendeleo ya Mifugo, Jeshi la Kujenga Taifa na baadhi ya Bodi za Mazao wameanzisha mashamba ya maonyesho na malisho ya mifugo.  Baadhi ni mazuri sana.  Aidha, baadhi ya makampuni, hususan Balton Tanzania Ltd. wametumia nafasi hii kuonyesha bidhaa wanazouza na teknolojia mbalimbali za umwagiliaji maji mashambani.  Nawapongeza sana Balton (T) Ltd. na nawaomba wafanyabiashara wengine washiriki katika maadhimisho ya Nane Nane yajayo.

 

 

  • Ukuta wa kuzunguka eneo hili unaendelea kujengwa kwa kasi ndogo lakini ya uhakika.

 

3.         Pamoja na mafanikio mazuri yaliyopatikana, bado iko kazi kubwa ya kuendelea kujenga majengo ya kudumu na kuweka utaratibu wa kuyatumia mwaka mzima.  Baadhi ya washiriki wanasita kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha kwa hofu kwamba mwakani watatakiwa kuhamia kwenye kituo kingine.

 

4.         Namshukuru sana Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo, Mheshimiwa Edward Lowassa (Mb.) kwa ushirikiano na juhudi zake za kutatua tatizo la maji kwenye viwanja hivi na Wizara yake kwa kuboresha sana maonyesho ya ufugaji mwaka huu.  Kati ya sasa na maadhimisho ya Nane Nane 2003, itabidi tulipatie tatizo la maji kwenye viwanja hivi ufumbuzi wa kudumu.

 

5.         Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Maonyesho ya kilimo yanaonyesha dhahiri kwamba tunao ujuzi unaotakiwa wa kumwezesha mkulima kupata tija kubwa zaidi katika kilimo.  Vituo vyetu vya Utafiti na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, vimezalisha mbegu nyingi zenye sifa bora za kutoa mazao mengi kwa eneo, ukinzani wa magonjwa, uvumilivu wa ukame na viini vya lishe bora.  Kazi iliyo mbele yetu ni kuzalisha mbegu hizo kwa wingi na kuzifikisha kwa mkulima mapema iwezekanavyo.  Nachukua nafasi hii kuyashauri makampuni ambayo yamekuwa yakiagiza mbegu kutoka nje kuchukua hatua za haraka za kuzalisha mbegu hizo humu nchini kama yangependa kuendelea na biashara hiyo.

 

6.         Kazi nyingine ambayo itafanyika katika mwaka ujao ni kusambaza mbinu za ugani na utafiti shirikishi na mbinu nyingine zilizojaribiwa kwa mafanikio za kufundisha kilimo bora, kwa mfano, shamba darasa.  Mfumo wa kuoanisha utafiti na huduma za ugani utaangaliwa upya na kuimarishwa.

 

7.         Kazi ya tatu itakuwa ni kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo na zana za kilimo za kutosha na kwa wakati.  Tunatambua kwamba tatizo kubwa ni uwezo mdogo wa mkulima wa kununua pembejeo na zana hizo bila mkopo.  Katika hotuba yako ya kuahirisha Mkutano wa Bunge la Bajeti tarehe 31 Julai, 2002, uligusia suala la vyombo vya fedha kutenga sehemu ya fedha zao kukopesha kilimo.  Tunakushukuru kwa maelekezo hayo na tutashirikiana na Wizara ya Fedha na Benki Kuu ya Tanzania kuzungumza na wahusika ili kuona uwezekano wa kuyatekeleza.  Visingizio mbalimbali vinavyotolewa vya kutokutoa mikopo kwa sekta ya kilimo, havina msingi lakini madhara yake kwa uchumi ni makubwa sana.  Katika mwaka huu wa fedha tutaweka utaratibu wa kugharamia kilimo ambao utajumuisha kumwezesha mkulima kupata mikopo.

8.         Kazi ya nne ni kuhakikisha kwamba mazao yanayozalishwa yatakuwa ya ubora wa kimataifa ili yaweze kupata bei nzuri katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

 

9.         Kazi ya tano ni kuendeleza juhudi za kufufua na kuongeza sana uzalishaji wa mazao muhimu ya biashara, hususan kilimo cha chai cha wakulima wadogo wadogo, mkonge, korosho na kahawa.  Ukuaji wa mazao mengine ni wa viwango vya kuridhisha.

 

10.       Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Watanzania wengi hawana imani kwamba kilimo chetu kinaweza kukua kwa viwango vya kuridhisha.  Sisi katika Sekta ya Kilimo tumeandaa mipango na utaratibu ambao unatupa matumaini kwamba kasi ya kukua kwa uzalishaji katika kilimo itaendelea kuongezeka kutoka asilimia 5.5 ya mwaka jana kuelekea kwenye asilimia zaidi ya 10 katika miaka michache ijayo.

 

11.       Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza wakulima kwa mchango wao mkubwa katika maisha na uchumi wa Taifa hili.

 

12.       Baada ya maneno hayo machache, sasa nina heshima kukukaribisha kuzungumza na wakulima, wafanyabiashara, walaji n.k. na kuhitimisha maadhimisho ya Nane Nane 2002.

 

 

 

Karibu Sana!