SALAAM ZA WAZIRI WA KILIMO NA CHAKULA MHESHIMIWA CHARLES N. KEENJA (MB.) WAKATI

WA UFUNGUZI WA MKUTANO WA NNE WA

SEKTA YA PAMBA JIJINI MWANZA

 TAREHE 18 – 19 MACHI, 2003

 

Mheshimiwa George Kahama (Mb.), Waziri wa Ushirika na      Masoko,

 

Mheshimiwa Daniel Ole Njoolay, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,

 

Mheshimiwa Raphael N. Mlolwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Pamba,

 

Mheshimiwa Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza,

 

Waheshimiwa Mawaziri,

 

Waheshimiwa Wabunge,

 

Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa,

 

Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,

 

Waheshimiwa Viongozi wa Serikali,

 

Waheshimiwa Wageni Waalikwa,

 

Mabibi na Mabwana.

Mhe. Waziri wa Ushirika na Masoko, napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru kwa kukubali kuwa mgeni rasmi wa mkutano huu wa nne wa Sekta ya Pamba.  Wewe ni Mdau na Kiongozi muhimu katika sekta hii na tunaamini kwamba uongozi wako katika mkutano huu, utatuwezesha kufanya maamuzi ambayo yataiwezesha sekta hii muhimu kukua na kuchangia katika kuondoa umaskini miongoni mwa wakulima wa pamba na kuongeza pato la Taifa.  Tunakushukuru sana kwa kukubali kuwa Mwenyekiti wetu.

 

2.         Ndugu Mgeni Rasmi, tulipokutana mwaka wa 2002 uzalishaji wa pamba ulikuwa marobota 282,000.  Katika mwaka huu, uzalishaji umefikia marobota 354,000 sawa na ongezeko la asilimia 29.  Ninapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wakulima, wafanyabiashara na wadau wengine wa zao la pamba kwa mafanikio yaliyopatikana.  Wizara yangu kupitia Bodi ya Pamba na kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa, itaendelea kuhimiza kilimo cha pamba ili kifikie lengo la marobota 750,000 ifikapo mwaka wa 2006/2007.

 

3.         Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tukiwapongeza wakulima kwa kuongeza uzalishaji wa pamba, inatubidi tutambue na kukubali kwamba uzalishaji wa pamba kwa eka moja bado ni mdogo sana.  Kwa wastani, wakulima wanavuna kilo 250 hadi 300 kwa eka.  Kama wakitumia samadi, wanapata mavuno mara dufu na wakipanda kwa vipimo sahihi na kutumia mbolea za chumvi chumvi wanaweza kupata kilo 1,200 kwa eneo lile lile la eka moja.  Hii ina maana kwamba kwa kutumia mbinu za kilimo bora, wakulima wetu wanaweza kuongeza uzalishaji wa pamba mara nne bila ya kupanua eneo wanalolima na kwa kufanya hivyo, kuongeza sana mapato ya mkulima.

 

4.         Kuongeza tija katika kilimo cha pamba ni njia sahihi ya kupunguza umaskini na kuwatajirisha wakulima.  Katika msimu wa 2004/2005 Wizara za Kilimo na Chakula na Ushirika na Masoko na Bodi ya Pamba, tutafanya kampeni kubwa ya kuongeza uzalishaji kwa eneo kwenye maeneo yote yanayolima pamba.  Bodi ya Pamba itaandaa kampeni hiyo kwa kushirikisha Halmashauri zote za Wilaya zinazohusika.

 

5.         Bei za Pamba kwenye soko la dunia ziko chini sana.  Kwa upande wa Tanzania, pamba yetu iliwahi kuwa na sifa kubwa ya ubora na sifa hiyo iliiwezesha kupata bei nzuri sana katika soko.  Tumepoteza sifa hiyo kwa kutokuzingatia masharti rahisi ya kuchambua pamba na kuiweka kwenye madaraja na wengine wamediriki kuitilia pamba maji au kuichanganya na mchanga ili kuiongezea uzito.  Vitendo vyovyote vinavyoharibu ubora wa pamba vinafanya pamba yetu isipate bei zuri katika soko.  Tumeamua kuchukua hatua za makusudi za kuhakikisha kwamba pamba yetu inarudia kuwa na sifa nzuri ya ubora duniani.  Huenda baadhi ya watu wasifurahishwe na hatua zitakazochukuliwa.  Kwa vyovyote vile, pamba yoyote itakayochanganywa na vitu visivyohusika itapewa daraja la chini au haitanunuliwa kabisa.

 

6.         Bei ndogo ya pamba inatokana pia na kuuzwa kwa pamba bila ya kuongezewa thamani kwa kusindikwa.  Baadhi ya viwanda vyetu vya nguo vimekwisha binafsishwa.  Tunawaomba wale waliovinunua wavikarabati haraka ili vianze uzalishaji wa nyuzi na nguo.  Kiwanda cha MWATEX kiliwahi kuwa na sifa ya kuzalisha nguo zilizopendwa sana.  Tunatarajia kwamba kitarudia umaarufu wake baada ya muda sio mrefu.  Baada ya viwanda vyetu kuanza kuzalisha kikamilifu ndipo Serikali itakapoangalia uwezekano wa kuvilinda na ushindani wa nguo za ubora wa chini au mitumba inayoingizwa nchini kwa wingi hivi sasa.

 

7.         Kilimo chetu cha pamba kinakabiliwa na tatizo la matumizi ya jembe la mkono kulimia.  Tunawaomba Serikali za Mitaa na Vyama vya Ushirika kuhimiza sana kilimo cha kutumia wanyamakazi na kuanzisha vituo vya matrekta ya kukodishwa kwa wakulima.  Mikoa inayolima pamba ina utajiri mkubwa wa mifugo na iko katika nafasi nzuri sana ya kutumia wanyamakazi na mashine nyingine katika kilimo.  Mfuko wa Pembejeo umeagizwa kutoa mikopo ya kununulia majembe ya kukokotwa na ng’ombe na matrekta na pia kuyafanyia matrekta matengenezo.  Tumieni nafasi hii.

 

8.         Kuanzia msimu wa 2004/2005 ukanda wote wa Magharibi utatumia aina moja ya mbegu inayojulikana kama UK91.  Ukanda wa Mashariki nao utatumia aina moja tu ya mbegu IL85. Utaratibu wa kupata mbegu zitakazosambazwa kwa wakulima utabadilishwa ili kuhakikisha kwamba mkulima anapata mbegu ya ubora unaotakiwa.  Chini ya utaratibu huu, mbegu zote zinazotokana na pamba itakayonunuliwa kutoka kwa wakulima zitakamuliwa ili kupata mafuta.  Wakulima maalum watateuliwa kulima pamba itakayochambuliwa kupata mbegu za kusambaza kwa wakulima.  Utaratibu huu unatarajiwa kuondoa tatizo la kusambaza mbegu zilizoota kutokana na pamba kutiliwa maji.  Aidha, utaratibu huu utahakikisha kwamba ni mbegu ile tu inayopendekezwa ndiyo itakayolimwa.

 

9.         Kwa kifupi, mipango ya uzalishaji wa pamba katika miaka ijayo inapaswa kulenga:

 

(a)                Kuongeza uzalisha kwa eneo kwa kufuata masharti ya kilimo bora.

 

(b)               Kushirikiana na Serikali za Mitaa Vyama vya Ushirika, Vikundi vya Wananchi na wananchi wenye uwezo, kuongeza matumizi ya wanyamakazi na matrekta kupunguza uzito wa kazi za kilimo na usafirishaji wa pembejeo na mazao.

 

(c)                Kuhakikisha kwamba pamba yetu inarudia ubora wa hali ya juu, kama ilivyokuwa zamani.

 

(d)               Kuhimiza usindikaji wa pamba ili kuiongezea thamani na kuongeza ajira.

 

(e)                Kuweka utaratibu wa kupata mbegu bora na ya aina inayopendekezwa na kuifikisha kwa wakulima.

 

10.       Ili tufanikiwe katika kutekeleza malengo haya, itabidi viongozi na wakulima tushirikiane kuhimiza utekelezaji wa malengo haya na kutatua matatizo yoyote yatakayotokea mara yatakapojitokeza.  Huu ni wajibu wetu sote na hatupaswi kuwaachia watu fulani fulani tu.

 

11.       Mheshimiwa Waziri, baada ya maelezo haya mafupi, sasa nakuomba utufungulie mkutano huu wa wadau wa pamba na kisha uuongoze kwa kuwa Mwenyekiti wetu.

 

Asanteni kwa kunisikiliza.