RASIMU YA SALAAM ZA WAZIRI WA KILIMO NA CHAKULA MHESHIMIWA CHARLES KEENJA WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO WA TATU WA SEKTA YA PAMBA JIJINI MWANZA TAREHE

2 MEI 2002

 

Mheshimiwa Fredrick T. Sumaye (Mb.),

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Mheshimiwa Balozi George Kahama (Mb.), Waziri wa

Ushirika na Masoko,

Mheshimiwa Stephen J. Mashishanga, Mkuu wa Mkoa

wa Mwanza,

Mheshimiwa Raphael N. Mlolwa (Mb.) Mwenyekiti wa Bodi ya Pamba,

Mheshimiwa Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza,

Waheshimiwa Mawaziri,

Waheshimiwa Makatibu Wakuu,

Waheshimiwa Wabunge,

Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa,

Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,

Waheshimiwa Viongozi wa Serikali,

Waheshimiwa Wageni waalikwa,

Mabibi na Mabwana.

 

 

1.         Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa niaba ya Wizara ya Kilimo na Chakula, kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya wajumbe wote wa mkutano huu nina furaha sana kukukaribisha kwenye Mkutano huu wa Tatu wa Sekta ya Pamba.  Aidha, napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru sana kwa kutenga muda katika shughuli zako nyingi kuja Mwanza kushiriki na kuongoza mkutano huu wa tatu wa Wadau wa Pamba.  Asante sana na karibu sana Mwanza na kwenye Mkutano huu.

 

2.         Mheshimiwa Waziri Mkuu, tulipokutana hapa mwaka jana, uzalishaji wa pamba nchini ulikuwa umeshuka kutoka marobota 532,000 yaliyopatikana katika msimu wa 1992/93 hadi kufikia marobota 196,000 katika msimu wa 1999/00.  Katika msimu wa 2000/01 uzalishaji ulipanda kidogo kufikia marobota 225,000.  Kwa msimu wa ununuzi wa 2001/02, ambao ndio unamalizika, uzalishaji wa pamba nchini uliongezeka tena hadi kufikia marobota 282,000, ongezeko la silimia 25.  Hata hivyo, ongezeko hili ni chini ya matarajio yetu ambayo yalikuwa kuzalisha marobota kati ya 400,000 na 500,000.

 

3.         Mheshimiwa Waziri Mkuu, matarajio yetu hayakuweza kufikiwa kwa sababu ambazo zimetajwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Pamba hususan uhaba mkubwa wa madawa ya kuulia wadudu katika msimu uliopita, suala ambalo lilipelekea asilimia kubwa ya pamba kutonyunyiziwa madawa ya kuulia wadudu kabisa na hivyo kuathirika sana kutokana na uharibifu wa wadudu wa pamba. 

 

4.         Mheshimiwa Waziri Mkuu, pamoja na mambo mengine, madhumuni makubwa ya mkutano huu ni kutathmini maendeleo ya sekta ya pamba ya kufuatilia utekelezaji wa maazimio yaliyotolewa kwenye Mkutano wa Pili wa Sekta ya Pamba uliofanyika mwaka jana. Mkutano huu utazingatia zaidi juhudi zinazochukuliwa katika kuikwamua Sekta ya Pamba kutokana na matatizo makuu matatu yaliyoainishwa na Mheshimiwa Rais katika hotuba yake kwa mkutano huu mwaka juzi ambayo ni:- kushuka kwa uzalishaji, tija na ubora wa pamba; usimamizi hafifu wa sekta ya pamba katika hatua zote za uzalishaji, ununuzi, usindikaji na uuzaji wa pamba; na kilimo cha pamba kukosa msukumo wa kutosha kiuwekezaji.

 

5.         Katika mwaka uliopita, Bodi ya Pamba ilitekeleza kwa ufanisi, baadhi ya maagizo waliyopewa na Mkutano wa Wadau wa tarehe 17 – 18 Aprili, 2001 na Wizara.  Mambo hayo ni pamoja na:

 

(a)                           Kuzalisha kwa wingi mbegu mpya ya pamba iliyozalishwa na kituo cha Utafiti cha Ukiriguru inayofaa kwa ukanda wote wa magharibi.  Bodi ilizalisha kilo 4000 kwa kilimo cha umwagiliaji maji mashambani na msimu huu wanatarajia kuzalisha 71,150 ambazo zitakidhi nusu ya mahitaji yote ya mbegu kwa ukanda wa magharibi.  Nachukua nafasi hii kuwapongeza Watafiti wa Ukiriguru kwa kuzalisha mbegu moja mpya inayofaa kwa ukanda wote wa magharibi ambayo itaondoa tatizo lililosababishwa na soko huria la kuchanganyika kwa mbegu za pamba.  Bodi ya Pamba inapaswa kuandaa mipango mizuri ya kuzalisha mbegu hiyo kwa wingi katika muda mfupi iwezekanavyo na kuondoa mbegu zote za zamani ili zisichanganyike na mbegu hii mpya.

 

(b)                           Katika kipindi hiki Bodi iliandaa na kukamilisha Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Pamba.  Kinachotakiwa sasa ni kuandaa programu za kuutekeleza.

 

(c)                           Katika kipindi hiki Bodi ya Pamba ilifufua jinari za  Mwaya katika wilaya ya Ulanga, Mandera katika wilaya ya Bagamoyo na Kilosa na iliendesha kampeni za kuwahimiza wakulima waanzishe au wapanue kilimo cha pamba.

 

(d)                           Aidha, Bodi iliweka mipango mizuri iliyohakikisha upatikanaji wa madawa ya kuulia wadudu na kupunguza sana hasara ambayo ingeweza kupatikana.

 

(e)                           Bodi ya Pamba imeanza kutekeleza majukumu yake vizuri na inastahili pongezi kwa mafanikio yaliyopatikana.  Hata hivyo, bado yapo matatizo mengi ambayo yanahitaji kushughulikiwa haraka.

 

6.         Tatizo la uthibiti hafifu wa ubora wa pamba inayozalishwa linachangia sana kusababisha pamba yetu ipate bei ya chini.  Tatizo hili linachangiwa na wakulima wenyewe na kukuzwa sana na ununuzi holela wa pamba unaofanywa na wanunuzi binafsi.  Bodi inapaswa kuweka utaratibu wa kuthibiti mienendo ya wakulima na wanunuzi wa pamba ili kuhakikisha kwamba pamba inawekwa katika madaraja sahihi ya ubora na inakuwa katika hali ya juu ya usafi.

 

7.       Mheshimiwa Waziri Mkuu, kuna maeneo kadha ambayo hatujapata mafanikio na kwa kweli hatujayapa umuhimu yanayostahili.

 

(a)                        Uzalishaji wa pamba kwa eka (tija) bado ni mdogo sana (kg. 250 – 300 tu).   Kwa kutumia samadi na kulitunza shamba vizuri, uzalishaji kwa eka unaweza kuongezeka kufikia kg. 600 – 700 na kwa kuongeza mbolea za chumvi chumvi, uzalishaji unaweza kupanda hadi kg. 1000 – 1200 kwa eneo lile lile.  Sheria ya Pamba ya 2001, inahitaji kusajiliwa kwa wakulima wa pamba na itabidi uongozi katika ngazi zote, wakiwamo maafisa ugani, wahakikishe kwamba mbinu za kilimo bora zinafuatwa ili kuongeza uzalishaji na kupunguza uwiano wa gharama za uzalishaji na mapato.

 

(b)                        Eneo la pili ambalo halijathibitiwa ni mwenendo mzima wa kuvuna, kusafirisha na kuchambua pamba.  Wakulima wengi hawavuni au kuichambua pamba na kuiweka kwenye madaraja ya ubora.  Viwanda vya kuchambua pamba navyo vinachambua pamba bila kujali ubora wake.  Kwa kulinda usafi na ubora wa pamba na kwa kuichambua kwa ‘roller gins’, bei ya kilo moja inaweza kuongezeka kwa karibu shs. 140/= au USD 15. Ni lazima wakulima, wanunuzi na wenye viwanda vya kuchambua pamba wazingatie mbinu zote za kuifanya pamba yetu kuwa bora na wasiofanya hivyo wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.

 

(c)                        Tatizo jingine ni lile la wanunuzi kutokuwalipa wakulima kulingana na ubora wa pamba yao.  Tabia hii inawafanya wakulima wasione umuhimu wa kuichambua pamba na kuipanga kwenye madaraja ya ubora.

 

(d)                        Baadhi ya Viwanda vya nguo vimeshabinafsishwa na tunatarajia kwamba waliovinunua watachukua hatua za haraka kuvirudisha kwenye uzalishaji.  Aidha, tunahitaji wawekezaji wengi zaidi ambao watatengeneza nyuzi na nguo za pamba ili tuuze nguo na nyuzi badala ya pamba ghafi.

 

8.         Bodi ya Pamba peke yake haina watumishi wa kutosha wa kuiwezesha kutekeleza majukumu yake yote kwa ufanisi na Wizara yangu haipendekezi kuajiriwa kwa watumishi wengi zaidi.  Narudia kuhimiza Bodi zote za mazao kushirikiana na Serikali za Mitaa kuwapatia watumishi wa kilimo waliopo mafunzo maalum ya kuwawezesha kusimamia kilimo cha mazao yanayohusika na kuchangia katika kuwawezesha watumishi hao kutekeleza kazi zinazohusika.  Tuwaandae watumishi waliopo ili wawe mabingwa katika kusimamia kilimo na tuwatumie kikamilifu.

 

9.         Mheshimiwa Waziri Mkuu, pamoja na matatizo yaliyojitokeza msimu uliopita, matarajio yetu msimu huu ni mazuri.  Hali hii inatokana na mambo yafuatayo:-

 

*   Hali ya hewa kwa ujumla imekuwa nzuri na ya kuridhisha ijapokuwa katika baadhi ya maeneo kulikuwepo ukame uliochelewesha upandaji wa zao hili.

 

*   Upatikanaji na usambazaji wa mbegu za kupanda msimu huu haukuwa na matatizo na wakulima walipata mbegu wakati muafaka.

 

*   Upatikanaji na usambazaji wa madawa ya kuulia wadudu umekuwa mzuri zaidi ingawa bado kuna matatizo madogo madogo hapa na pale zaidi kuhusiana na mazoea ya wakulima ya aina fulani tu za madawa ya kuulia wadudu na vinyunyizi vyake.

 

10.       Kutokana na hali ya uzalishaji kuwa nzuri katika msimu huu, tunatarajia kwamba uzalishaji wa pamba utafikia marobota 325,000 katika msimu wa 2002/2003.

 

11.       Mheshimiwa Waziri Mkuu, baada ya kusema haya machache, kwa heshima na taadhima nakuomba sasa  utufungulie Mkutano wa Pili wa Sekta ya Pamba nchini.

 

PAMBA “DHAHABU NYEUPE”

 

KARIBU SANA.