HOTUBA YA WAZIRI WA KILIMO NA CHAKULA, MHESHIMIWA CHARLES N. KEENJA (MB.), ALIYOITOA WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA MWAKA WA WIZARA YA KILIMO NA CHAKULA, ULIOFANYIKA UYOLE,

MBEYA, TAREHE 09 HADI

10 MACHI, 2003

 

Mhe. Matheo Qares, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,

Mhe. Pius Mbawala, Naibu Waziri wa Kilimo na Chakula,

Ndugu Katibu Mkuu,

Ndugu Wafanyakazi,

Wageni Waalikwa,

Mabibi na Mabwana.

 

           

Ndugu Mwenyekiti, awali ya yote, ninapenda nichukue nafasi hii kukushukuru Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa pamoja na Uongozi wote wa Mkoa kwa kutupokea vizuri.  Ninakushukuru pia kwa kushiriki katika mkutano huu. Ninapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru nyote kwa kuitikia wito wa kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Chakula. Aidha, ninapenda niwashukuru wale wote walioshiriki katika kuandaa mkutano huu kwa kazi nzuri waliyofanya.

 

2.         Ndugu Mwenyekiti, kama mnavyofahamu tumejiwekea utaratibu wa kukutana kila mwaka ili kutathmini maendeleo ya kilimo nchini na kutoa mapendekezo ya kuboresha utekelezaji.  Hivyo, ni matarajio yangu kuwa  mkutano huu ni fursa nyingine ya kutafakari, kujadili na kutathmini maazimio ya mkutano wa mwezi wa Machi, 2002 uliofanyika Morogoro ili kubaini yametekelezwa kwa kiwango gani.

 

3.         Ndugu Mwenyekiti, sababu nyingine ya kukutana kila mwaka ni kutathmini mtazamo wetu kuhusu kilimo na kuona kama mtazamo huo unatuelekeza kwenye  mapinduzi ya kilimo tunayokusudia kuyafanya. Wote tunafahamu kwamba nchi hii ina raslimali nyingi za kuwafanya wananchi wake kuwa na maisha mazuri.  Mojawapo ya raslimali hizo ni ardhi nzuri inayofaa kwa kilimo. Hata hivyo, raslimali hiyo haijatumika ipasavyo kuzalisha mazao ya kutosha, kutoa uhakika wa chakula na  kuondoa umaskini.  Kwa mfano, kati ya hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo ni karibu hekta milioni 10 tu zinatumika kwa shughuli za kilimo. Aidha, kati ya hekta milioni 29.2 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ni hekta 191,000 tu ambazo zimeendelezwa. Hata katika eneo ambalo limeendelezwa, bado uzalishaji kwa eneo ni mdogo sana. Kwa hiyo, changamoto iliyo mbele yetu ni kuleta mapinduzi katika kilimo ili kuhakikisha ardhi inayofaa kwa kilimo inatumika ipasavyo. Kwa kuwa sisi kama wafanyakazi wa kilimo inatubidi kuonyesha njia, ni vizuri sisi tukawa na mtazamo sahihi kuhusu kilimo na mwelekeo wa pamoja kuhusu mbinu na mapinduzi ya kilimo  tunayokusudia kuyaleta.

 

4.         Ndugu Mwenyekiti, karibu asilimia 80 ya Watanzania wanaishi vijijini ambako wanategemea kilimo kwa maisha yao.  Aidha, sekta nyingine za uchumi zinategemea kukua kwa kilimo ili nazo zikue.  Pamoja na ukweli huu, umaskini umeendelea kujikita vijijini ambako wananchi wengi wanajishughulisha na kilimo kama shughuli yao kuu ya uchumi.  Hivyo, ni dhahiri kuwa mkakati wowote wa kuondoa umaskini na ambao utajenga msingi wa uchumi imara ni lazima ulenge katika kuendeleza kilimo.  Na kwa maana hiyo, kila tunapopata nafasi ya kukutana ni lazima tutathmini hali ya kilimo na kuona kama kinachangia ipasavyo katika kuondoa umaskini.

 

5.         Ndugu Mwenyekiti, katika miaka minne iliyopita, kilimo kimeanza kuonyesha dalili za kuongeza kasi ya kukua.  Kasi hiyo imeongezeka kutoka asilimia 4.1 mwaka wa 1999 na kufikia asilimia 5.5 mwaka wa 2003.  Inatarajiwa kwamba ukuaji huo utafikia asilimia sita mwaka wa 2003.  Hata hivyo, kiasi hiki cha ukuaji bado ni kidogo kuondoa umaskini na kuwezesha uchumi kukua kwa kasi ya kuridhisha.  Changamoto iliyo mbele yetu ni kukifanya kikue kwa kasi ya asilimia 10 au zaidi kwa mwaka.  Kazi iliyo mbele yetu ni kubaini njia zitakazokifikisha kilimo kwenye kiwango hicho cha ukuaji.

 

6.         Katika hutoba yangu ya mwaka jana, niliainisha matatizo mbalimbali yanayokikabili kilimo.  Aidha, katika mkutano huo mlipata fursa ya kujadili matatizo hayo na mengine mengi yanayokwamisha kilimo na kupendekeza njia za kuchukua kuyatatua.  Mkutano huu ni fursa nyingine ya kutathmini jinsi tulivyokabiliana na matatizo hayo, mafanikio tuliyoyapata na hatua za kuchukua kwa matatizo ambayo yanaendelea kuathiri maendeleo ya kilimo.  Itakuwa vizuri kama tutaainisha matatizo hayo, ili tujiridhishe kwamba tunakubaliana kwamba ndiyo yanaendelea kuathiri ukuaji wa sekta ya kilimo na ndipo tuanze kuyachambua moja moja na kupendekeza njia za kuchukua kuyaondoa.

 

7.                  Ndugu Mwenyekiti, pamoja na kwamba mwaka jana nilitaja matatizo yanayokikabili kilimo, ningependa hata mwaka huu nichangie katika mkutano huu kwa kuyataja tena kwani bado yapo. Tatizo moja wapo ambalo itabidi tupambane nalo ni tabia potofu ya kubeza na kudharau kilimo.  Kutokana na tabia hiyo, kilimo kimekuwa hakipewi umuhimu katika mipango ya maendeleo na hivyo kutokutengewa raslimali za kutosha. Kwa mfano, Halmashauri nyingi za Mitaa hupata mapato yao kutokana na kilimo, lakini ni Halmashauri chache hutenga fedha kwa ajili ya kuendeleza kilimo.

 

8.                  Mchango mdogo wa kilimo cha umwagiliaji maji mashambani kwa kulinganisha na eneo linalofaa kuendelezwa kwa ajili ya umwagiliaji. Kama nilivyo sema hapo awali, kuna hekta 29.4  sawa na asilimia 66.33 ya ardhi inayofaa kwa kilimo, zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji maji mashambani.  Hata hivyo ni hekta 191,000 tu sawa na asilimia 0.65 ya eneo linalopaswa kuendelezwa kwa kilimo cha aina hiyo.

 

9.                  Teknolojia nyingi ambazo zimekuwa zikitolewa na Vituo Vyetu vya utafiti zimekuwa haziwafikii wakulima. Aidha, unganisho hafifu kati ya utafiti, mafunzo, huduma za ugani  na wakulima limesababisha teknolojia hizo na mbinu bora za uzalishaji na usindikaji kutowafikia wakulima wengi. Aidha, kutokuwapo kwa mbinu sahihi ya kutoa mbinu za ugani kumechangia kwa kiwango katika tatizo hilo.

 

10.              Upotevu wa mazo kabla na baada ya mavuno ni tatizo ambalo halijapatiwa ufumbuzi wa kutosha. Visumbufu vya mimea na mazao vimeendelea kusababisha upotevu mkubwa kutokana na wakulima kutozifahamu mbinu mbalimbali za kudhibiti visumbufu hao.  Aidha, uhaba wa miundombinu ya kutosha kwa ajili ya kuzindika mazao ni tatizo linalochangia kwa kiasi kikubwa katika upotevu wa mazao, husani yale yanayoharibika haraka kama matunda na mbogamboga.

 

11.              Kilimo cha kutumia zana duni na matumizi madogo ya pembejeo ni kikwazo kikubwa katika kuongeza tija na uzalishaji katika kilimo.    Matumizi ya matrekta, majembe ya kukokotwa na wanyama na mashine bora za kurahisisha kazi bado ni madogo. Kutokana na tatizo hili, wakulima wengi wana mashamba madogo ya kati ya hekta 0.2 hadi 2.0.  Hivyo, wakulima wa aina hii hawawezi kupanua eneo wanalolima na uzalishaji katika vishamba hivyo ni wa kujikimu.

 

12.       Pamoja na matatizo niliyoyataja na mengine mengi ambayo mmekuwa mkipambana nayo, yapo pia mafanikio ambayo yamepatikana.  Mafanikio hayo yametokana na juhudi zenu kwa kushirikiana na wafanyakazi wengine na wadau mbalimbali katika sekta ya kilimo.  Ninapenda kuchua fursa hii kuwapongeza wote waliowezesha mafanikio hayo kupatikana.

 

13.       Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni;

 

(i)                  Kukamilika kwa maandalizi ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo, kwa ngazi ya Taifa, ambayo iliandaliwa na Wizara ya Kilimo na Chakula kwa kushirikiana na Wizara za Maji na Maendeleo ya Mifugo na Ushirika na Masoko, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na washirika wa maendeleo ambao wamekuwa wakishirikiana au wanakusudia kushirikiana na Wizara katika kutekeleza majukumu yake.

 

(ii)                Kukamilika kwa maandalizi ya sehemu ya kwanza ya Mpango Kabambe wa Umwagiliaji Maji Mashambani.  Mafanikio ya awali ya maandalizi hayo yamekamilika na sasa tnajua kuwa Taifa lina hekta milioni 29.2 zinazofaa kuendelezwa kwa kilimo cha umwagiliaji maji mashambani  na siyo hekta milioni moja kama ambavyo tulikuwa tukijua kabla ya maandalizi ya Mpango huo.

 

(iii)               Wizara kwa kushirikiana na walengwa katika maeneo mbalimbali ya nchi imekamilisha miradi 28 ya umwagiliaji maji mashambani na mingine inaendelea kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa.

 

(iv)              Katika kukabiliana na kero ya watumishi kutopandishwa vyeo kwa muda mrefu, wizara imeweka utaratibu mzuri wa kupata takwimu na taarifa za utendaji kazi za watumishi kwa kila mwaka na tayari watumishi wengi wamepandishwa vyeo kwa mserereko na wale ambao hawajapandishwa vyeo tunatarajia wapate stahili zao kabla ya mwisho wa Juni, 2003.  Wizara inakusudia kuendelea kurekebisha na kuboresha maslahi ya watumishi wake ili yaende sambamba na watumishi wenye sifa kama za walioko kwenye wizara nyingine za Serikali.

 

(v)                Vituo vya Utafiti vimekuwa vikitoa teknolojia bora ambazo zikiwafikia wakulima zitachangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta mapinduzi ya kilimo.  Kwa mfano, vituo vimezalisha mbegu bora za mazao mbalimbali ambazo zikizalishwa kwa wingi zitaongeza uzalishaji katika kilimo kwa kiasi kikubwa.  Kwa kutumia mbinu shirikishi jamii, tutahakikisha teknolojia hizo zinawafikia wakulima. 

 

(vi)              Wizara kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa na wakulima imeimarisha uwezo wa kupambana na visumbufu vya mimea na mazao na kudhibiti milipuko ya visumbufu hivyo ili ilipojitokeza. Aidha, wizara imeendelea kueneza matumizi ya mbinu ya udhibiti husishi na itaendelea kufanya hivyo.

 

(vii)             Kuweka mfumo wa huduma za ugani wenye ufanisi. Wizara inakusudia kuhakikisha matumizi ya mbinu shirikishi jamii na shamba darasa yanaenezwa nchi nzima. Mafanikio makubwa yaliyotokana na matumizi ya mbinu hizi katika maeneo nchini, yamedhihirisha kuwa mbinu hizo zinafaa kutumika nchi nzima. 

 

14.       Ndugu mwenyekiti, kilimo chetu kimeanza kuonyesha dalili za kukua japokuwa kinaendelea kuathiriwa vibaya na matatizo mbalimbali yakiwemo ya hali mbaya ya hewa. Ili kupata mafanikio makubwa katika kilimo ni sharti tufanye juhudi za makusudi za  kuandaanda mipango na kuimarisha usimamizi wa kilimo kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa.  Ni lazima mipango hiyo ihakikishe kwamba;

 

(i)                  Kila mkulima au kaya ya wakulima inakuwa na shamba lenye ukubwa wa kutosha

 

(ii)                Kuweka utaratibu shirikishi jamii wa kuandaa mipango ya kilimo na usimamizi wake katika ngazi zote ili kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika utekelezaji na kumiliki mipango hiyo.

 

(iii)               Kuweka mfumo utakaohakikisha upatikanaji wa mahitaji ya kilimo ikiwa ni pamoja na mikopo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kilimo.

 

(iv)              Kuhimiza matumizi ya wanyama kazi na zana za kisasa katika uzalishaji na usindikaji wa mazao.

 

(v)                Kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa, hususan sayansi ya bioteknolojia.  Ili tusibakie nyuma kwenye ulimwengu wa sasa wa sayansi na teknolojia, inatubidi kuzidisha kasi ya kujenga na kupanua maabara za teknolojia hii pamoja na kupeleka wataalam nchi za nje kujifunza jinsi ya kendeleza teknolojia hizo.  Aidha, inabidi kujenga uwezo wa kubaini matokeo ya teknolojia hizo ili wananchi wajue manufaa na madhara yake .

 

(vi)              Kupunguza upotevu wa mazao kabla na baada ya mavuno kwa kutumia mbinu husishi na teknolojia bora za kudhibiti visumbufu vya mimea na mazao.

 

(vii)             Kuunganisha na kuimarisha huduma za utafiti, ugani na mafunzo ili kuondoa udhaifu uliokuwapo katika unganisho (linkage) la huduma hizo.

 

(viii)           Kuboresha na kuweka mfumo imara wa uapatikanaji na usambazaji wa pembeo za kilimo. Wizara itaendelea kuwasiliana na mamlaka husika ili kuharakisha uanzishwaji wa Wakala wa mbegu.

 

(ix)              Kuhimiza uzalishaji, kwa wingi na kwa ubora unaotakiwa na soko, wa mazao ya biashara yasiyokuwa ya asili kama vile mazao ya viungo, maua na matunda ambayo yana bei nzuri.

 

(x)                Kuhimiza na kufundisha kilimo cha kibiashara ili wakulima waendeshe shughuli za kilimo kwa faida na kwa kuzingatia gharama halisi za uzalishaji.

 

14.       Ndugu Mwenyekiti, hayo niliyoyataja ni baadhi tu ya matatizo na mafanikio yaliyojitokeza miaka ya hivi karibuni.  Wakati mnajadili mada mbalimbali mtapata fursa ya kuchangia mawazo yanu katika maeneo niliyogusia na mengine yatakayojitokeza katika mada hizo.  Ningependa wahiriki wote wa Mkutano huu watoe mawazo yao bila woga wowote.  Mchango wa mawazo yao ndio utakaosaidia katika kuboresha utekelezaji na kuweka mikakati endelevu ya kutekeleza mtakayo azimiwa katika Mkutano huu.

 

15.       Ndugu Mwenyekeiti, kabla sijamaliza hotuba yangu ninapenda kutumia fursa hii kutoa taadhari kwa wananchi kutumia vizuri chakula walichojiwekea. Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa mwaka huu inawezekana tusipate mvua ya kutosha.  Kuna dalili kwamba baadhi ya sehemu za nchi zitapata ukame au mvua zitanyesha kwa mtawanyiko mbaya. Hivyo, wakulima  washauriwe kulima mazao kwa kuzingatia ushauri wa kitaalam utakaotolewa na watalaam wa kilimo kwenye maeneo yao. Wizara yangu inafuatilia suala hili kwa karibu na itatoa taarifa na maelekezo zaidi kama mvua hazitaanza kunyesha kwa kufuata majira.

 

16.       Ndugu Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninapenda kuwashukuru maandalizi  na mapokezi mazuri tuliyoyapata. Aidha, ninawatakia majadiliano yenye manufaaa.  Sasa natangaza kuwa Mkutano  Mkuu wa mwaka wa wafanyakazi wa Kilimo  umefunguliwa rasmi.