HOTUBA YA WAZIRI WA KILIMO NA CHAKULA,

MHE. CHARLES N. KEENJA (MB.) WAKATI AKIFUNGUA MKUTANO WA BARAZA LA WAFANYAKAZI, MJINI MOROGORO, TAREHE 19 MACHI, 2004

 

 

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Waheshimiwa Viongozi wa Wizara ya Kilimo na Chakula,

Waheshimiwa Washiriki wa Baraza

 

1.         Awali ya yote, ninapenda kuwashukuru kwa kunialika kuja kufungua Mkutano wa Baraza lenu la Wafanyakazi wa Kilimo.  Hii ni fursa nzuri kwangu kutoa mchango wangu wa mawazo na ni nafasi nzuri ya kupata taarifa, kuelekezana kukumbushana na kuchangia mawazo kuhusu majukumu ya Wizara na ushiriki kwa wafanyakazi katika kuyatekeleza na kuyasimamia.

 

2.         Mwenyekiti, Baraza la Wafanyakazi ni chombo kinachowawezesha wafanyakazi kushiriki katika mipango na utekelezaji wake.  Mabaraza ya wafanyakazi hutoa fursa kwa wafanyakazi kushiriki katika maamuzi mbalimbali na kuboresha uhusiano baina ya wafanyakazi mahali pa kazi.  Kwa maneno rahisi ni chombo cha kuimarisha na kuboresha demokrasia mahali pa kazi.  Hata hivyo inatubidi kuwa na tafsiri sahihi ya demokrasia mahali pa kazi.

3.         Demokrasia ninayoizungumzia ni mfumo unaowawezesha wafanyakazi kushiriki katika kufanya maamuzi halali na kutekeleza maamuzi hayo kwa wakati uliopangwa, kwa uadilifu na kwa nidhamu ya hali ya juu ya kazi.  Ni mfumo unaoweka mizania sawa kati ya maslahi ya mwajiri na mwajiriwa.  Kwa maneno mengine ni mfumo unaoweka wajibu na haki za kila mwajiri na mwajiriwa katika kufanikisha malengo ya kiuchumi na kijamii.

 

4.         Ndugu Mwenyekiti, nchi yetu imepitia mfumo wa uchumi hodhi na sasa wanuchumi huru na utandawazi.  Misingi na mahitaji ya mifumo hii yanatofautiana kwa baadhi ya mambo.  Hivyo, kuna haja ya kuifahamu vizuri na kubadili fikira zetu na utaratibu wa utendaji kazi ili kazi zetu ziwe za ufanisi.  Kubadilika kutoka mfumo mmoja kwenda mfumo mwingine, mara nyingi husababisha woga na wasiwasi kuhusu matokeo ya mfumo mpya.  Mfumo wa sasa wa soko huru haukwepeki kama ulivyo utandawazi.  Kwa hiyo inatubidi kujizatiti kuweka mikakati, mipango, taratibu, sheria na kanuni za kazi zitakazotuwezesha kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa katika mfumo huu.  Hii siyo kazi rahisi lakini ni kazi ya lazima kama inatubidi kuishi kama Taifa.

 

5.         Ndugu Mwenyekiti, Taifa letu liko katika mabadiliko na linafanya mabadiliko katika sera, miundo ya taasisi zetu na sheria mbalimbali zinazosimamia utekelezaji wa sera zetu.  Kwa mfano, tunao Mpango wa Kurekebisha Utumishi wa Umma (Civil Service Reform).   Mipango ya Kurekebisha Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma, Mipango hii inatutaka tubadilishe utendaji wetu wa kazi na hata fikra zetu kuhusu kazi.  Baraza la Wafanyakazi linabidi kuwa mstari wa mbele kuelewa na kuwaelimisha wafanyakazi wengine juu ya umuhimu na matokeo ya mipango hii, ili wafanyakazi washiriki kikamilifu katika kuifanikisha.

 

6.         Ni wazi katika kutekeleza mipango hii, kutakuwa na vikwazo na matatizo yatakayojitokeza.  Hata hivyo, vikwazo hivyo na matatizo yatakayojitokeza inabidi kuwa changamoto katika uendeshaji wa shughuli za Serikali.  Baraza linabidi liwe mshiriki mkubwa katika kubuni mbinu mpya za uendeshaji wa shughuli za Serikali, na siyo kusubiri tu Serikali kubuni mbinu za uendeshaji wa shughuli zake na Baraza kufanya kazi ya kupokea malalamiko tu kutoka kwa wafanyakazi.

 

7.         Ndugu Mwenyekiti, nchi yetu inaendesha mfumo wa Vyama vingi vya Siasa.  Wafanyakazi inabidi wafahamu vizuri mfumo wa vyama avingi vya siasa na jinsi ya kautekeleza majukumu yao katika mfumo huo.  Kwa mfano, wafanyakazi inawabidi kuifahamu Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala na kuitekeleza, hata kama ni mashabiki wa itikadi za vyama vingine vya Siasa.

           

8.         Baraza la Wafanyakazi linabidi kuelewa kwa ufasaa mipango mbalimbali ya Serikali na kuwaelimisha watumishi wengine kuhusu mipango hiyo.  Kwa mfano, Baraza la Wafanyakazi wa Kilimo linabidi kuelewa Sera ya Kilimo, Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo, Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo, na jinsi Wizara inavyotelekeza majukumu yake kwa kufuata sera, mkakati na Mipango iliyopo.

 

9.         Ndugu Mwenyekiti, hizi ni zama za utandawazi.  Inatubidi kuuelewa utandawazi na kuandaa mikakati itakayohakikisha nchi yetu inanufaika na utandawazi.  Utandawazi unatutaka tufanye kazi tofauti na mazoea tuliyokuwa nayo huko nyuma.  Inatubidi kufanya kazi kwa ufanisi zaidi, kwa nidhamu ya kazi ya hali ya juu na kwa kusimamiana.  Mazingira ya kazi yamebadilika sana ulimwenguni kutokana na maendeleo ya teknolojia za kufanyia kazi na za mawasiliano.  Kazi ambazo huko nyuma zilihitaji muda mwingi kuzifanya, sasa zinaweza kufanyika kwa muda mfupi na kwa ufanisi mkubwa.  Wizara ya Kilimo inabidi kubaini na kutumia teknolojia bora ambazo zitarahisisha utendaji wa kazi.

 

10.       Ndugu Mwenyekiti, teknolojia bora ni nyenzo nzuri ya kuongeza ufanisi sehemu za kazi na motisha kwa wanaozitumia.  Hata hivyo, teknolojia hizo zitakuwa za manufaa kama zitatumika kufanikisha majukumu ya Wizara ya Kilimo na Chakula.  Jukumu kubwa ni kuhakikisha tija na uzalishaji unaongezeka katika sekta ya kilimo.  Hii ina maana kwamba, teknolojia zitakazotumika nchini lazima zituwezeshe kuzalisha kwa wingi na mazao bora.  Hili haliwezi kutokea isipokuwa kama tutapanga mipango sahihi na kuweka vipaumbele ambavyo kwa kutumia teknolojia hizo yataleta matokeo makubwa, hususan kwa wakulima.

 

11.       Ndugu Mwenyekiti, nimekuwa nikikutana na wafanyakazi wengi ambao wamekuwa wakijitambulisha kuwa ni wafanyakazi wa Kilimo.  Lakini nimekuwa nikijiuliza kama kila mmoja wao anajua wajibu, mchango wake na jinsi anavyopaswa kushiriki katika kuendeleza kilimo.  Sina uhakika kama kila mfanyakazi wa kilimo ana hadidu za rejea za kazi yake na mpango wa kazi kulingana na hadidu hizo.  Kuna ulazima wa kuhakikisha kila mfanyakazi katika ngazi mbalimbali anafanya kazi ambazo  zinatanikisha mwelekeo na madhumuni ya Wizara.  Kila kiongozi kwa ngazi yake inambidi kusimamia kikamilifu waliochini yake na kubaini watu wanaofanya kazi zao vizuri, wanaohitaji msaada ili wafanye kazi zao vizuri, walio na udhaifu kiasi cha kutomudu majukumu yao na hatua za kuchukua kuboresha utendaji wa kazi.

 

12.       Ndugu Mwenyekiti, ninafahamu kuwa moja ya mambo mtakayojadili ni makadirio ya bajeti ya Wizara ya Kilimo na Chakula.  Hii ni fursa nzuri kwenu kutathmini shughuli zilizotekelezwa mwaka huu na matokeo ya shughuli hizo.  Aidha, ni wakati mzuri wa kuainisha maeneo muhimu ya kupewa kipaumbele katika mwaka wa 2004/2005.  Maeneo hayo yawe ni yale ambayo kama serikali itawekeza fedha zake, ukuaji wa tija na uzalishaji utakuwa kwa haraka sana.  Sambamba na kuainisha maeneo hayo, ni lazima kuonyesha jinsi ya kutekeleza shughuli zitakazopangwa kuendeleza maeneo hayo na jinsi kila mfanyakazi wa kilimo atakavyoshiriki katika kuzifanikisha.

 

13.       Eneo lingine ninalopenda kutiliwa mkazo ni kuboresha mazingira ya kazi ya watumishi wa kilimo.  Hii ni pamoja na kukamilisha zoezi la kuwapandisha vyeo watumishi wa kilimo na kurekebisha maslahi yao kulingana na sifa walizonazo, kuwapatia vitendea kazi na kutoa miongozo mbalimbali itakayowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.  Inatubidi kuangalia wafanyakazi kama raslimali muhimu katika kuendeleza kilimo na kwa hiyo kuna haja ya kuiendeleza na kuijengea mazingira mazuri ya kazi.

 

14.       Ndugu Mwenyekiti, kilimo chetu bado hakijakua kwa kasi itakayotuwezesha kujitosheleza kwa chakula na kuhimili athari zinazosababishwa na ukame, milipuko ya visumbufu vya mimea na mazao na majanga mengine.  Aidha, hakijakua kwa kasi ya kupunguza umaskini kwa wanaokitegemea kilimo kwa maisha yao.  Hii ina maana kwamba kuna mambo ambayo hatujafanya au hatujafanya sawa sawa kukifanya kilimo kikue kwa kasi inayotakiwa.  Hii ni changamoto ambayo inabidi kuijadili na kuona kama mipango iliyopo inakidhi mahitaji ya sasa ya kilimo.

 

15.       Kabla sijamaliza hotuba yangu napenda kuwakumbusha kuwa tunazo raslimali ambazo ni lazima tuziwekee mipango mizuri ili ziwezeshe kilimo kukua kwa kasi kubwa kuliko ilivyo sasa.  Tuna raslimali ya watu, ardhi, maji na mitaji kutoka vyanzo mbalimbali.  Raslimali hizi hatujazitumia kikamilifu kutuwezesha kufikia kiwango cha ukuaji wa sekta ya kilimo utakaotuwezesha kuondokana na umaskini.  Aidha, matumizi ya muda kama raslimali muhimu hatujaitilia maanani sana.  Mipango ya kutumia raslimali lazima ijumuishe matumizi ya muda.  Lazima tuandae mipango mizuri itakayotuwezesha kutumia raslimali tulizonazo kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo.  Mahali pa kuanzia ni kwenye bajeti ya kilimo na raslimali ya watu tuliyonayo.

 

16.       Mwisho, baada ya kusema hayo machache sasa natangaza kuwa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Kilimo umefunguliwa rasmi.  Nawatakia majadiliano yenye mafanikio.

 

 

Asanteni kwa kunisikiliza.