HOTUBA YA WAZIRI WA KILIMO NA CHAKULA, MHESHIMIWA CHARLES N. KEENJA (MB.) WAKATI WA KUFUNGUA SEMINA YA KILIMO YA MKOA WA MOROGORO TAREHE 21 NOVEMBA, 2003

 

 

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kukupongeza sana wewe kwa uongozi wako na wa viongozi wengine wa Chama cha Mapinduzi na Serikali yake kwa juhudi mnazofanya kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya Wananchi wa Mkoa huu.  Mkoa wa Morogoro una rasilimali nyingi ambazo zikitumiwa vizuri, unaweza kuendelea kwa kasi kubwa sana.  Kwa bahati mbaya, mkoa huu umeendelea kuwa na sifa za kuwa na rasilimali nyingi na matumaini kwamba siku moja utazinduka na kuzitumia rasilimali hizo lakini hayo yamebaki kuwa matumaini au ndogo ambazo hazielekei kutimia.

 

2.         Mwaka juzi, mwaka wa 2001, niliutembelea mkoa wa Morogoro kwa siku 14.  Mkuu wa Mkoa alinitembeza akanionyesha mabonde yenye rutuba na mito zaidi ya 176 yenye maji yasiyokauka kwa mwaka mzima.  Katika baadhi ya maeneo, kwa mfano katika Wilaya ya Kilombero, utajiri huu wa maji na udongo mzuri ni kikwazo cha mawasiliano na maendeleo badala ya kuwa neema alizotupa Muumba wetu.

 

3.         Lengo langu la kutembelea mkoa wa Morogoro kwa siku 14, ambazo ni nyingi sana, lilikuwa kubaini fursa za maendeleo katika kilimo na kushirikiana na uongozi wa Mkoa kubuni mikakati ya kuzitumia kwa maendeleo ya wakazi wa mkoa wa Morogoro na Taifa kwa jumla.  Malengo yangu hayakutimia lakini naendelea kuwa na matumaini kwamba siku itakuja ambapo wakazi wa mkoa huu watatumia utajiri walionao kwa manufaa yao na ya Taifa kwa jumla.  Nisilojua ni lini siku hiyo itakapokuja na tutaitambuaje itakapofika.

 

4.         Mheshimiwa Mwenyekiti, suala moja ni la uhakika kabisa.  Haitatokea wananchi wa Mkoa huu wakazinduka ghafla wakainua majembe na kuanza kulilima eneo lote la mkoa huu.  Tukisubiri hilo litokee, tutasubiri kwa maisha yetu yote na hakuna litakalotokea.  Baadhi ya mambo ambayo sisi tunayaona kuwa matatizo, pengine wananchi hawayaoni hivyo.  Kutokana na uzuri wa ardhi, mvua za kuaminika na maji mengi kwenye mito na kwenye mabonde, mtu akitumia nguvu kidogo anaweza kabisa kujitosheleza kwa mahitaji yake ya chakula na hata kujipatia fedha kidogo.  Kama tunataka kupata mabadiliko katika maendeleo yetu, ni sharti uongozi uwe na uelewa na mtazamo utakaouwezesha kuwaongoza wananchi ili wasiridhike na mambo madogo madogo na wajenge mahitaji makubwa kuliko kula, kushiba na kulala.  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Benjamin William Mkapa aliwahi kutueleza maneno aliyoambiwa na Rais wa India, Mheshimiwa Dr. Avu Abdul Kalam kwamba, “Where nature Works, man does not work”.

 

5.         Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kwamba Mkoa wa Morogoro una rasilimali nyingi za ardhi nzuri, kubwa na inayofaa kwa kilimo.  Ili tutumie rasilimali hizo kwa maendeleo, ni sharti tuziainishe kwa usahihi zaidi kuliko kutambua tu kuwapo kwazo na kuhakikisha kwamba kila familia na vijana wanapata sehemu ya rasilimali hizo ya kukidhi mahitaji yao.  Mara nyingi tunasikitika tukisema, “Mkoa hauna shida ya ardhi” lakini msemo huu sio sawa sawa na kusema kwamba kila familia ina ardhi ya kutosha ambayo inaweza kuitumia kwa shughuli zake za Kilimo, ufugaji na shughuli nyingine.  Pengine niulize hapa, je ni kiasi gani cha ardhi ambacho familia inahitaji?  Tukishatambua kiasi hicho, lililobaki ni kuhakikisha kwamba kila familia inapata siyo chini ya kiwango hicho cha ardhi.  Ni lazima pia vijana wanaomaliza elimu ya shule za msingi na hata juu zaidi, wapatiwe ardhi ili waitumie kama nyenzo ya kuzalisha mali na kama msingi wa kujiandaa kwa maisha katika familia zao wenyewe.  Suala hili halijapewa umuhimu unaostahili.

 

6.         Tukiunda vikundi vya wananchi katika vijiji na tukavishirikisha na watumishi waliopo na kuvipa mafunzo, tutaweza kuhakikisha kwamba kila familia inapimiwa eneo la ardhi la kukidhi mahitaji yake na wala hatutakuwa tukifanya jambo jipya kwa kuwa limeshafanyika kwa mafanikio katika baadhi ya mikoa humu nchini.

 

7.         Hatua ya kuhakikisha kwamba kila mwananchi ana ardhi ya kutosha na kwamba vijana wana ardhi yao wenyewe na ya kuwatosha ni muhimu sana katika kupanga maendeleo ya mkoa kwa kuwa tutakuwa tunapanga kutumia rasilimali mbili muhimu: nguvukazi na ardhi.  Tuepuke kosa la kuamini kwamba ardhi ipo na wananchi wanaweza kuipata.  Inawezekana, kweli kwamba ardhi ipo lakini siyo kila mtu ana ardhi ya kukidhi mahitaji yake na wengine hawajui jinsi ya kuipata.  Kazi moja ya Serikali na uongozi kwa jumla ni kuondoa dosari hizi.

8.         Baada ya wananchi kupata ardhi ndipo tunapoanza kazi muhimu ya kutafsiri au kuanisha kilimo cha wananchi wa maeneo mbalimbali ya mkoa wa Morogoro.  Vision (taswira) ya mkoa ni nini?  Katika Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo tunasema kwamba, Ifikapo mwaka wa 2025 kilimo chetu kiwe cha kisasa, cha kibiashara, chenye tija, chenye faida na kinachohakikisha matumizi endelevu ya maliasili zilizopo na chenye kushirikisha sekta nyingine”.  Maana yake ni kwamba ifikapo mwaka 2025 kilimo chetu kitakuwa cha kisasa, chenye tija na faida.  Kwa kuwa Vision hii ni ya Kitaifa itabidi mkoa wa Morogoro uichukue ilivyo na kuichambua na kuifafanua ili ioane na matakwa ya wananchi wa mkoa huu na mazingira yake.

 

9.         Kilimo chetu ni sharti kitimize mambo yafuatayo:

 

Kwanza: ni lazima kituhakikishie upatikanaji wa chakula chetu na kwa Mkoa wa Morogoro ambao unapaswa kuwa “Kapu la Taifa la Nafaka”, unapaswa kuzalisha ziada kubwa ya chakula ambayo itatumiwa kulisha maeneo mengine ya nchi au kuuzwa nje ya nchi.  Hivi sivyo ilivyo hivi sasa.

 

             Pili: kilimo chetu ni sharti kitupatie malighafi za viwanda vyetu vilivyopo na vitakavyojengwa.  Kwa kawaida, nchi inapoanza kuendelea, hujenga viwanda vya kusindika mazao ya kilimo na baadaye viwanda vya aina nyingine.  Uzalishaji wetu wa mazao ya aina zote bado uko chini sana na viwanda vya kusindika mazao navyo ni vichache sana.

 

             Tatu: tunalazimika kulima mazao ambayo tutayauza nje ili tujipatie fedha za kigeni.  Kwa wastani, sekta ya kilimo huchangia theluthi mbili za mapato yetu ya fedha za kigeni.

 

-          Kilimo kingeweza kutoa mchango mkubwa zaidi kama masharti fulani fulani yangezingatiwa.

 

-          Bei za mazao mengi katika soko la dunia zimeshuka sana na inatubidi tukiangalie kilimo chetu upya ili kiendelee kuongoza katika kuchangia uchumi wa nchi na kuinua ubora wa maisha ya wananchi wetu.

 

Nne:  kwa kutekeleza hayo niliyotangulie kueleza, kilimo kitatoa ajira kwa wananchi na kuchangia kwa kiwango kikubwa katika kupunguza umaskini.

 

10.       Mkoa wa Morogoro unaongoza kwa kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari.  Hali hii itaendelea, hususan shamba jipya la Ruipa litakapoanza kuendelezwa na Mtibwa watakapoendeleza eneo kubwa waliloongezewa na Serikali.  Kilimo cha miwa kinawapa wananchi wa Mkoa wa Morogoro fursa ya kuchangia katika uzalishaji wa miwa kama “outgrowers au contract farmers” wa mashamba makubwa.  Wanaoweza kushiriki katika kilimo hiki ni wachache kutokana na vikwazo mbalimbali lakini tunapaswa kuweka utaratibu wa kufaidika na kilimo hicho kwa kiasi kinachowezekana.

 

11.       Nje ya kilimo cha miwa na usindikaji wa sukari, Mkoa wa Morogoro hauna jingine la kujivunia.  Maeneo mengine ya nchi yakilalamika juu ya upungufu wa chakula, Morogoro nao wamo na mkoa hauna mazao ya biashara ya kujivunia.  Hali hii ni lazima ibadilike na ifanyike hivyo haraka.

 

12.       Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, nakusifu sana kwa msukumo unaoweka katika kuhimiza uzalishaji katika kilimo.  Uhimizaji na usimamiaji wa kilimo ni kazi zinazopaswa kufanywa na viongozi wote, hususan Halmashauri zote za Wilaya na Miji.  Tatizo lililopo ni kwamba tusipokuwa waangalifu tunaweza kutumia muda mwingi kuhimiza jambo lisilokuwapo na pia inawezekana tukawa tunatumia utaratibu ambao hauwafikii wananchi na kuwasaidia kutatua matatizo yao ili kuwawezesha kuzalisha kwa ufanisi, kwa wingi na kwa ubora unaotakiwa.

 

13.       Tumekubaliana kwamba mahali pa kuanzia ni kuhakikisha kwamba kila mkulima ana shamba kubwa linalokidhi mahitaji yake.  Ardhi ndiyo rasilimali kuu katika kilimo na asiyekuwa nayo hawezi kuwa mkulima.  Hatua ya pili ni kuandaa mfumo wa usimamizi na utoaji elimu au ujuzi unaomshirikisha mkulima na, kwa hiyo unaomfikia.  Katika maeneo mengi nchini, wananchi wamejiunga kwenye vikundi vyao, vinavyoongozwa na vinavyoshirikisha viongozi na wataalam wa ngazi inayohusika na vikundi hivyo vimekuwa na mafanikio makubwa sana katika kupanga, kusimamia utekelezaji na matumizi ya teknolojia sahihi katika uzalishaji.  Vikundi hivi vinakuwa ‘darasa’ linalotumiwa na wakulima wenyewe kwa kuwa wanajua mambo mengi ambayo wanaweza kufundishana na pia yanatumiwa na wataalam wachache waliopo kuwaongezea wakulima ujuzi.

 

14.       Inabidi yawepo mambo yaliyopangwa kufanywa na yaliyowekewa utaratibu wa kuyatekeleza.  Mambo hayo yaamuliwe na wananchi wenyewe kupitia kwenye vikundi vyao chini ya ushauri wa uongozi na  wataalam wao.  Inabidi kuwa waangalifu ili uongozi usijichukulie madaraka ya kutoa amri na vitisho.  Lengo la uongozi ni kuelekeza, kushauri, kulea na kuwezesha.  Lakini uongozi unapaswa pia kuvisaidia vikundi kutekeleza maamuzi na maagizo yao.

 

15.       Shughuli zitakazofanywa na vikundi zitaainishwa kwa ukubwa, mahitaji na jinsi ya kuyapata na nafasi ya kila mshiriki katika kutekeleza sehemu yake ya shughuli husika.  Kwa maneno mengine, utaandalaiwa mpango wa kikundi utakaoonyesha mahitaji ya kuutekeleza lakini utakaoonyesha pia manufaa yatakayotokana na kutekelezwa kwa mpango huo kwa kikundi na kwa kila mshiriki.  Manufaa yanavyozidi kuwa makubwa kwa washiriki ndivyo watakavyovutiwa kushiriki na kuchangia katika kufanikisha shughuli za kikundi.

 

16.       Mipango ya vikundi vyote katika Kata ikiunganishwa, tutapata mpango wa kata na mipango ya kata zilizoko katika Wilaya ikiunganishwa, tutapata mpango wa wilaya au “District Agricultural Development Plan” (DADP).  Serikali imekwishaagiza kila wilaya kuandaa mpango wake wa Maendeleo ya Kilimo na mipango hiyo ndiyo itakayotengewa fedha kutoka kwenye bajeti ya Serikali na kutoka kwa Washirika wetu wa maendeleo.  Katika mwezi wa Julai, 2003 utekelezaji wa PADEP ulianza rasmi na mpango huo utashirikisha Wilaya 28.  Serikali inakusudia kuchukua mkopo wa ADB ambao utagharimia DADPs katika wilaya nyingine 28 na Benki ya Dunia, IFAD na FAO wako nchini hivi sasa wakiandaa mpango wa kufikisha utaalam wa kilimo kwa wakulima.  Kwa kifupi, fedha zitapatikana kwa watakaopanga lakini ni kweli pia kwamba kwa wale ambao hawatapanga wataachwa nyuma.

 

17.       Suala la nne muhimu linahusu mazao ya kulimwa, utaalamu wa kuyalima na kuyaandaa kwa matumizi yetu au kwa soko.  Kwa upana, tumekubaliana kwamba tutalima mazao ya chakula na ya biashara kwa sababu ambazo tumeziainisha.  Lakini haitoshi kuzungumzia mazao kwa upana huo inabidi tuangalie mazingira yetu na kuamua ni mazao gani yanayostawi katika mazingira hayo na kuchagua yale yenye manufaa makubwa zaidi ndiyo tukazanie katika kuyazalisha.  Mkoa wa Morogoro uko karibu na Bandari na Kiwanja cha Ndege cha Dar es Salaam jambo ambalo linatupa fursa ya kuandaa mipango yetu ya uzalishaji kwa kulenga masoko yaliyoko  nje ya mipaka yetu.  Mazao kama paprika, ndizi, pamba n.k. yanatajwa lakini hakuna mipango iliyoandaliwa na kubadilisha ndoto kuwa ukweli.

 

18.       Uzalishaji ni lazima ulenge mahitaji ya ndani ya nchi na masoko ya nje na ufanywe kwa makusudi na siyo kama tabia au desturi tu.  Hii ina maana kwamba inatubidi tuchague aina za mazao tunayolima kwa kuzingatia mahitaji ya masoko tuliyotafuta.  Ni lazima tuzingatie nidhamu ya uzalishaji kulingana na mahitaji ya soko na ubora unaotakiwa.  Tunakusudia kuanzisha Bodi ya Mazao Mchanganyiko ambayo itashirikiana na Wazalishaji kubaini aina na ubora wa mazao yanayotakiwa na soko na kusimamia upangaji wa mazao hayo katika madaraja ya ubora na kuhakikisha kwamba bei zinapangwa kwa kuzingatia ubora huo.

 

19.       Yapo mambo ambayo tunayajua lakini hatuandai mipango ya kuyafanya.  Tunajua, kwa mfano, kwamba tungeweza kuongeza uzalishaji kutoka eneo linalolimwa hivi sasa kwa hadi mara tano (x5).  Tunajua kwamba asilimia karibu 40 ya mazao tunayozalisha yanapotea kwa kuharibiwa na wadudu kama dumuzi, wanyama kama panya na kwamba asilimia nyingine inayokaribia 30 inaharibikia mashambani.  Tunajua kwamba tuna uwezo wa kurekebisha dosari hizi kwa gharama nafuu na kwamba ipo mipango ya kutusaidia.

 

20.       Tunalalamikia mvua zisiponyesha na zinaponyesha.  Tunatumia sehemu ndogo tu ya mwaka katika uzalishaji.  Mkoa wa Morogoro una mito mingi inayoanzia kwenye milima na tungeweza kuitumia kumwagilia maji kwenye mashamba yetu kwa gharama nafuu sana.  Mkoa huu uko nyuma sana katika kilimo cha umwagiliaji maji mashambani.  Aidha, kilimo cha umwagiliaji maji mashambani kingetuwezesha kuzalisha chakula kwa wingi na pia mazao ya kuuzwa nje ya nchi.  Haya mambo hayatatokea kwa miujiza.  Inabidi yawekwe kwenye DADPs.

 

21.       Mwisho, Mkoa wa Morogoro una mashamba mengi makubwa yaliyotelekezwa.  Tumeomba sana mkoa uyajadili mashamba hayo na kuwasilisha mapendekezo kwenye Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ili hatua zinazofaa zichukuliwe.  Hatutavumilia watu kuhodhi ardhi bila ya kuitumia kikamilifu kama ilivyokusudiwa.

 

22.       Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kusisitiza kwamba ili tupate maendeleo katika kilimo tunahitaji:

 

·        Kuweka mfumo wa usimamizi, na uhimizaji.

 

·        Tunahitaji kuandaa mipango ya uzalishaji itakayoonyesha mahitaji na manufaa yatakayopatikana.

 

·        Inatubidi kuchagua mazao kwa kuzingatia mazingira yetu, mahitaji yetu na ya soko la ndani na la nje na tunapaswa kuzalisha kwa nidhamu na kwa kuzingatia mahitaji ya soko.

 

23.       Uongozi ni muhimu sana na mfano mzuri na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Benjamin William Mkapa ambaye chini ya uongozi wake madhubuti uchumi wa nchi hii unakuwa kwa kasi ya kuridhisha.  Viongozi wa Tanzania wameacha kusimamia kilimo na kuwaacha wananchi wafanye wanavyojua na wanavyoweza.  Aidha, staili za uongozi na usimamizi mara nyingi haziwezeshi kupatikana kwa mafanikio yaliyokusudiwa.  Tujirekebishe!!  Tusimamie utekelezaji wa mipango iliyoandaliwa na tupunguze maagizo ya kwenye majukwaa.

 

24.       Inabidi tuangalie zana wanazotumia wakulima katika kilimo.  Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba “kama Adam na Mke wake Hawa wangerudi Duniani wangeona mambo mengi ya kuwashangaza lakini hawatashangazwa na kilimo chetu”.  Katika kuandaa mipango ya kilimo, tulenge kupanua sana kilimo cha wanyamakazi na matrekta ili kupanua ukubwa wa maeneo yanayolimwa na ili pia kupunguza uzito wa kazi za kilimo.

 

25.       Tunatarajia kwamba tukichukua hatua sahihi, mkulima mdogo atakua kutoka uzalishaji wa kujikimu na kuwa mzalishaji wa kibiashara – anayezalisha kwa ajili ya soko.  Aidha, tunalenga kuwawezesha watu wenye ujuzi na rasilimali kuwekeza katika kilimo cha mashamba makubwa ambayo yataingiza teknolojia za kisasa za uzalishaji na ambayo yatazalisha kwa wingi kwa ajili ya soko.

26.       Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, napenda kuchukua fursa hii kukuhakikishia wewe na Wananchi wa Mkoa wa Morogoro kwamba Serikali inatambua sana uwezo wa Mkoa wa Morogoro wa kuwa “grain basket” ya Tanzania na nawaahidi ushirikiano katika kuwapatia utaalam na rasilimali za kuwekeza.  Mkoa una Vyuo Vikuu Viwili, vituo vya Utafiti na Vyuo vya Kilimo – Mnazo rasilimali nyingi na za aina zote.  Zitumieni!  Sharti moja tu ni kwamba mnapaswa kuamua mnaelekea wapi ili wengine washirikiane nanyi kuwawezesha kuelekea huko.  Miaka iliyopita Mkoa haukuonyesha ari ya kuchukua hatua za kuharakisha maendeleo ya wananchi wenu.  Naanza kuona mabadiliko na tungependa kuwa sehemu ya mabadiliko na mafanikio hayo.  Semina hii ni kielelezo cha mabadiliko hayo.

 

27.       Baada ya maneno hayo machache, sasa natamka kwamba semina yenu imefunguliwa rasmi.