HOTUBA YA WAZIRI WA KILIMO NA CHAKULA, MHE. CHARLES N. KEENJA (MB.), AKIZINDUA BODI YA WAKURUGENZI YA BODI YA KAHAWA, MOSHI, TAREHE 18 AGOSTI, 2003.

 

 

Ndugu Mwenyekiti, Dr. Hussein Mongi,

Ndugu Wajumbe wa Bodi

 

            Awali ya yote, ninapenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru kwa kunialika kuja kuzindua Bodi yenu.  Ninapenda kuchukua nafasi hii kukupongeza wewe Dr. Hussein Mongi kwa kuteuliwa na Rais kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Kahawa.  Aidha, ninawapongeza Wakurugenzi wote wa Bodi kwa kuteuliwa kuwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi.

 

2.         Ndugu Mwenyekiti, Bodi ya Kahawa ni chombo muhimu ambacho Serikali imekasimu madaraka kwake ili kisimamie maendeleo ya zao la kahawa.  Jukumu kubwa la Bodi ni kufanya shughuli zote za lazima na za manufaa kwa zao la kahawa.  Majukumu hayo yanajumuisha;

 

(i)                              Kuishauri Serikali kuhusu sera na mikakati ya kuendeleza zao la kahawa ili kuongeza ubora, uzalishaji na ushindani kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi;

 

(ii)                            Kuhimiza uendelezaji wa uzalishaji, usindikaji na soko la kahawa.

 

(iii)                           Kuandaa kanuni za kusimamia taratibu za upandaji na biashara ya kahawa ikiwa ni pamoja na kufuatilia bei ya zao hilo.

 

(iv)                          Kutoa fedha kwa ajili ya utafiti na Maendeleo ya Kahawa kuhamasisha uuzaji wa kahawa ndani na nje ya nchi.

 

(v)                            Kuweka kanuni na kudhibiti ubora wa kahawa na mazao ya kahawa.

 

(vi)                          Kukusanya, kuchambua, kutunza, kutumia au kusambaza taarifa na takwimu zinazohusiana na zao la kahawa.

 

(vii)                         Kufuatilia uzalishaji na uuzaji nje wa kahawa.

 

(viii)                       Kuhimiza uendelezaji wa teknolojia katika sekta ya pamba.

 

(ix)                          Kuandaa kanuni kwa ajili ya usindikaji, uuzaji nje na hifadhi ya kahawa na mazao yake.

 

(x)                            Kusaidia katika uanzishwaji wa vyama au vyombo vingine vinavyohusiana au kujihusisha na zao la kahawa.

 

(xi)                          Kulinda maslahi ya wakulima dhidi ya umoja wa wanunuzi ambao unaweza kufanywa kupitia katika uundwaji wa vyama.

 

(xii)                         Kuhakikisha uendeshaji sahihi wa Mfuko wowote ulioanzishwa chini ya sheria ya kahawa.

 

Chombo hiki kina wajibu mkubwa wa kusimamia shughuli zote za lazima na za manufaa kwa zao la kahawa.  Majukumu ya Bodi ya Kahawa yameainishwa vizuri katika sheria Na. 23 ya mwaka wa 2001.  Baadhi ya majukumu hayo ni;

 

Ninashauri kuwa kila mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi apatiwe nakala ya sheria hiyo na aisome kwa makini kwa kuwa inatoa mwongozo wa kufuatwa na Bodi Mpya ya Wakurugenzi katika kuendeleza zao la kahawa.

 

3.         Ndugu Mwenyekiti, zao la kahawa linakabiliwa na matatizo mengi ambayo Bodi yako itabidi iyawekee utaratibu wa kuyatafutia ufumbuzi wa haraka.  Baadhi ya matatizo hayo ni;

 

(i)                              Tija ndogo.  Uzalishaji kwa eneo ni wastani wa kilo 170 kwa hekta, wakati tija inayowezekana ni kilo 600 kwa hekta.  Tija hii ndogo inatokana na kutofuata kikamilifu kanuni za kilimo bora cha kahawa.  Katika baadhi ya maeneo nchini mibuni imezeeka sana na hakuna hatua za makusudi zilizochukuliwa kung’oa mibuni hiyo na kupanda mipya.  Katika maeneo mengine, mibuni haitunzwi vizuri kutokana na bei ya kahawa kuwa ndogo au huduma duni za ugani.

 

(ii)                            Matumizi madogo ya pembejeo za kilimo.  Kutokana na gharama kubwa za pembejeo, hususan mbolea na madawa, wakulima wengi wamekuwa wakitumia pembejeo kidogo au kutotumia pembejeo hizo.

(iii)                           Bei ndogo ya kahawa.  Bei ya kahawa katika soko la dunia zimekuwa za chini sana katika miaka ya hivi karibuni.  Bei ndogo zimewakatisha tamaa wakulima kutunza mikahawa yao na kuwekeza katika kilimo cha zao hilo.

 

(iv)                          Ubora hafifu wa kahawa.  Katika miaka ya nyuma, kahawa ya Tanzania ilikuwa na ubora wa juu na sifa ya kahawa ya Tanzania ilijulikana katika soko la Dunia.  Lakini sasa, ubora wa kahawa ya Tanzania umeshuka sana kutokana na kutokuwepo usimamizi na kanuni za kuendeleza zao la kahawa.  Wakulima wengi hawapangi kahawa yao katika madaraja ya ubora na hata wanunuzi hawajali tena kununua kahawa kulingana na ubora wake.

 

(v)                            Udhaifu katika usimamizi wa soko huru.  Kukosekana kwa mfumo wa kusimamia uendelezaji wa zao la kahawa kuanzia shambani hadi kahawa inapopelekwa mnadani au kwa ununuzi wa mwisho kumesababisha wafanyabiashara na hata wakulima  kuchanganya kahawa ya ubora wa juu na ile ya ubora wa chini na hivyo kuifanya sehemu kubwa ya kahawa inayozalishwa nchini kuwa ya ubora wa chini.

 

(vi)                          Huduma duni za ugani.  Kutokana na udhaifu katika kutoa huduma hiyo, mbinu bora za uzalishaji wa kahawa zimekuwa haziwafikii wakulima.  Aidha, usimamizi mbaya wa kutoa huduma za ugani umechangia sana katika kudumaza kilimo cha kahawa.

 

(vii)                         Kutokuwapo kwa vinu vya kutosha vya kukoboa kahawa.  Katika baadhi ya maeneo wakulima wamekuwa wakisafirisha kahawa ya maganda umbali mrefu, jambo ambalo linaongeza gharama za usafirishaji na kumpunguzia kipato mkulima.

 

(viii)                       Mfumo mbaya wa ununuzi wa kahawa.  Wafanyabiashara binafsi wamekuwa wakishirikiana kula njama za kumpa bei ndogo mkulima.  Kutokana na njama hizo, mnunuzi mmoja hununua kahawa, huikoboa na kwenda kuinunua mwenyewe mnadani.  Njama za namna hiyo zimekuwa zikikwamisha juhudi za kumpatia mkulima bei nzuri kwa kahawa yake. Kuna taarifa kuwa hata baada ya kubadilisha utaratibu wa utoaji leseni na kuweka Electronic Auction Machine kwenye mnada, bado kuna wafanyabiashara wanafanya njama na baadhi ya wafanyakazi wa Bodi wasiokuwa waaminifu kununua  kahawa yao wenyewe kwenye mnada.

 

(ix)                          Magonjwa ya Chulebuni, kutu ya majani na Mnyauko Fuzari wa Kahawa.  Magonjwa hayo yamekuwa yakiathiri sana uzalishaji wa kahawa nchini.  Kwa mfano, katika Mkoa wa Kagera, kuna ugonjwa wa Mnyauko Fuzari ambao umesababisha mikahawa mingi kukauka.

 

(x)                            Kodi nyingi kwenye zao la kahawa.  Zao hili limekuwa likitozwa kodi nyingi na hivyo kupunguza sehemu kubwa ya mapato anayopata mkulima.

 

(xi)                          Kutokuwepo mpango maalum wa kupanua kilimo cha kahawa katika maeneo ambako uzalishaji wa zao hilo unawezekana.  Kwa mfano, kuna maeneo katika mkoa wa Kagera, Mbeya, Ruvuma, Mara na Kigoma ambako upanuzi huo unawezekana, lakini hatua za kupanua maeneo hayo zinatekelezwa kwa kasi ndogo.

 

4.         Ndugu Mwenyekiti, haya ni baadhi tu ya matatizo yanayolikabili zao la kahawa.  Ninafurahi kuona kuwa baadhi ya matatizo yameanza kushughulikiwa kikamilifu na Vituo vya Utafiti wa Kilimo na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TACRI).  Kwa mfano, nina taarifa kuwa, uzalishaji wa kahawa ya vikonyo yenye ukinzani dhidi ya ugonjwa Mnyauko Fuzari imeanza kuzalishwa kwa wingi ili kukabiliana na tatizo hilo.  Aidha, nimefahamishwa kuwa TACRI imeainisha aina 31 za mbegu chotara za kahawa ambazo zina sifa ya kustahimili mashambulizi ya ugonjwa wa chulebuni na kutu ya majani.  Ninafikiri kuna haja ya kuongeza juhudi za kupambana na magonjwa hayo ili magonjwa hayo yasienee nchi nzima.

 

5.         Ndugu Mwenyekiti, kuna baadhi ya wazalishaji ambao wanazalisha kahawa yenye ubora wa juu na hivyo kupata abei nzuri.  Nimefahamishwa kuwa katika msimu wa 2002/2003, kahawa yenye ubora wa juu ilifikia dola za Kimarekani 2.63 kwa kilo.  Hii inaonyesha kuwa, tukizalisha kahawa yenye ubora wa juu itapata bei nzuri na wakulima watanufaika.  Ni dhahiri kuwa jambo hilo linawezekana.  Nitapenda Bodi iandae mkakati wa uzalishaji wa kahawa Bora.  Kuna haja ya kuhakikisha yafuatayo yanatekelezwa;

 

-                     Kutoa elimu ya kuwawezesha Maafisa ugani kumudu kazi yao vizuri zaidi.

 

-                     Kuweka utaratibu mzuri zaidi wa kusimamia maafisa ugani.

 

-                     Kusajili wakulima wote wa kahawa, ili kuhakikisha wanafuata kanuni za kilimo bora cha kahawa.   Kuwasajili wakulima wa kahawa kutarahisisha kuwafikishia utaalam, kusikiliza matatizo yao na kutafuta huduma za ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili.

 

-                     Kuhimiza wakulima wa kahawa kujiunga katika vikundi ambavyo vitasajiliwa kuzalisha kahawa ya ubora maalum (specialty coffee).

 

-                     Kuweka mfumo wa wakulima kupata utaalam kutoka kwa wataalam wa kilimo kwa mfano, kwa kutumia Mbinu Shirikishi Jamii na Shamba Darasa, nakadhalika.

 

6.         Ndugu Mwenyekiti, sambamba na mpango wa kuongeza tija na uzalishaji wa kahawa, Bodi inatakiwa kuandaa mkakati wa kutambua na kupenyeza masoko ya kahawa ambayo yatakuwa na soko zuri kwa kahawa tunayozalisha.  Inawezekana kuna masoko katika nchi za Afrika ambazo zinaweza kuwa soko zuri la kahawa tunayozalisha na yasiyokuwa na vikwazo vingi.  Lakini kwa kuwa hatujafanya juhudi ya kutosha kuyatambua na kuandaa mkakati wa kupenyeza katika masoko hayo, tunabakia kutegemea masoko ya ulaya Amerika na Japan ambayo yana vikwazo vingi.

 

7.         Ndugu Mwenyekiti, nimefahamishwa kuwa Taasisi ya Utafiti wa kahawa imekwisha kuandaa Mpango wa Kuendeleza zao la kahawa.  Itakuwa vizuri kama mpango huo utahusisha wakulima wa kahawa na kufanya utafiti utakaoleta mapinduzi katika uzalishaji wa kahawa nchini.  Kwa muda mrefu uzalishaji wa kahawa umekuwa wastani wa karibu tani 50,000 kwa mwaka.  Kuna haja ya kuongeza uzalishaji mara mbili ya uzalishaji wa sasa.

 

8.         Ndugu Mwenyekiti, soko la ndani la kahawa yetu bado ni dogo sana.  Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa, tunakunywa asilimia moja tu ya kahawa inayozalishwa hapa nchini.  Nchi kama Ethiopia wanakunywa zaidi ya asilimia hamsini ya kahawa wanayozalisha.  Kuna haja ya kuanza kuhamasisha wananchi kunywa kahawa na hususan kahawa ya Tanzania.  Itakuwa busara kama bodi itaandaa mpango maalum wa kuhamasisha wananchi kujenga tabia ya kunywa kahawa.

 

9.         Ndugu Mwenyekiti, tarehe 2 Julai, 2003, nilipokutana na viongozi mbalimbali wa Wizara na Taasisi zilizo chini ya Wizara ziliagiza kila Taasisi kuangalia upya muundo wake na kuona kama unaiwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo.  Kama Bodi ya Kahawa ilikuwa haijaanza kutekeleza agizo hilo, ningependa kazi ya kwanza ya Bodi hii mpya ya Wakurugenzi iwe kuangalia majukumu ya Bodi na Muundo wake na kuona kama muundo huo unaiwezesha kutekeleza na kupata matokeo yanayokidhi matarajio ya Serikali.  Kuna haja ya kuangalia upya ikama ya kila idara na kuhakikisha wote walioajiriwa ni wale tu wenye sifa zinazotakiwa kwa mujibu wa majukumu ya Bodi.  Nitapenda baada ya zoezi hili kukamilika, Bodi kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya itafute utaratibu wa kuwatumia wataalam wa kilimo walio chini ya Halmashauri badala ya kuajiri watumishi wapya.

 

10.       Mwisho, baada ya kusema hayo, ninatangaza kuwa Bodi ya Kahawa imezinduliwa rasmi.