HOTUBA YA WAZIRI WA KILIMO NA CHAKULA MHE. CHARLES N. KEENJA (MB.) WAKATI WA UZINDUZI WA BODI YA WAKURUGENZI WA BODI YA PARETO, KATIKA UKUMBI WA BODI YA CHAI, TAREHE 24 AGOSTI, 2002,

DAR ES SALAAM

 

Mwenyekiti wa Bodi, Mhe. Hassy Kitine,

Ndugu Wajumbe wa Bodi,

 

            Awali ya yote napenda nichukue fursa hii kuwashukuru kwa kunialika kuja kuzindua Bodi yenu.  Napenda kuchukua nafasi hii pia kumpongeza Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Bodi kwa kuteuliwa kuunda Bodi ya Pareto. 

 

2.         Ndugu Mwenyekiti wa Bodi, napenda nichukue nafasi hii kuongelea masuala mbalimbali yanayohusiana na maendeleo ya zao la pareto nchini.  Masuala nitakayogusia ni pamoja na; upanuzi wa kilimo cha pareto nchini, usindikaji wa zao hilo, usimamizi wa maendeleo ya zao la pareto na majukumu ya Wizara katika kuhudumia na maendeleo ya zao la pareto.

 

3.         Ndugu Mwenyekiti, kabla sijaendelea na hotuba yangu naomba kwanza niwakumbushe majukumu ya Bodi ya Pareto, kulingana na sheria ya pareto ya mwaka wa 1997.  Baadhi ya majukumu hayo ni;

 

-                     Kumshauri Waziri kuhusu hatua za kuchukua kukuza, kuendeleza na kudhibiti zao la pareto (Pyrethrum industry).

 

-                     Kupokea, kuzingatia na kumshauri Waziri kuhusu mapendekezo yoyote yatakayotolewa na wazalisaji wa pareto au Umoja wao kwa maslahi ya zao la pareto.

 

-                     Kupokea na kuzingatia maombi kwa ajaili ya kuzalisha pareto.

-                     Kufanya au kugharamia utafiti na majaribio moja kwa moja au kupitia wakala katika jambo lolote linalohusiana na zao la pareto.

 

-                     Kutoa leseni na kuamua mazingira ya kutoa leseni hizo.

 

-                     Kutengeneza kanuni kwa ajili ya kudhibiti visumbufu na magonjwa.

 

-                     Kutokana na uwezo iliyopewa na sheria, kufanya yale yote ambayo Bodi inaona ni lazima kwa kuendeleza zao la pareto.

 

Nimeanza kwanza kwa kuainisha majukumu ya Bodi ili tuelewane vizuri katika mambo tunayokusudia kuyafanya.  Kama mtakavyoona, sheria inatoa nafasi kubwa kwa Bodi kuweza kusimamia kikamilifu maendeleo ya zao la pareto.  Sheria inaipa Bodi uwezo kamili wa kudhibiti uzalishaji, usindikaji na biashara ya pareto nchini na kuishauri Serikali katika masuala mbalimbali yanayohusiana na zao hili.  Imani kubwa tuliyonayo katika Bodi hii itathibitika katika utekelezaji wa majukumu yake.

 

3.         Ndugu Mwenyekiti, kazi ya kwanza ya Bodi ambayo itabidi muifanye mara moja ni, kuangalia upya muundo wa Bodi ya Pareto katika ngazi zake zote ili kuona kama ina uwezo wa kusimamia majukumu yake ipasavyo.  Itabidi kuangalia kila idara na kila kitengo kuona kama kuna watumishi wenye sifa zinazotakiwa.  Kwa kufanya hivyo, mtahakiki uwezo wa Bodi na pengine kubaini udhaifu unaotakiwa kuondolewa. Aidha, itabidi kuhakikisha utendaji kazi katika Bodi unaleta ufanisi na kufikia lengo la kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zinazozalisha pareto kwa wingi duniani.  Tanzania inaweza kuzalisha pareto kwa wingi na kuchukua zaidi ya asilimia 25 ya soko la dunia.

 

4.         Eneo jingine ambalo linabidi kutiliwa mkazo ni kuhakikisha kilimo cha pareto kinapanuka na tija inaongezeka kuliko ilivyo sasa.  Kwa sasa uzalishaji kwa eneo ni wastani wa kilo 300 kwa hekta wakati tija inayowezekana ni wastani wa kilo 600 kwa hekta.  Kwa hiyo, kazi iliyo mbele yenu ni kuhakikisha watendaji katika ngazi zote wanasimamia uzalishaji kwa kufuata kanuni za kilimo bora cha pareto.  Mabwana shamba itabidi wapewe mafunzo ya kutosha kuhakikisha wanakielewa na kukisimamia ipasavyo kilimo cha pareto.

 

5.         Ndugu Mwenyekiti, changamoto iliyo mbele yenu ni kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo za kilimo kwa wakati.  Itabidi Bodi ifanye kazi kwa karibu sana na sekta binafsi ili kufanikisha lengo hilo.  Itabidi Bodi iweke utaratibu wa kuhakikisha sekta binafsi inashiriki kikamilifu katika kuendeleza zao hili.

 

6.         Eneo jingine muhimu ni soko la uhakika la maua ya pareto.  Kuongeza uzalishaji peke yake hakutoshi kumletea mkulima mafanikio na kuongeza kipato chake.  Inabidi kuhakikisha pareto inayozalishwa inanunuliwa yote na kwa bei nzuri.  Bodi inatakiwa kuhakikisha inatafuta na kuvutia wawekezaji katika viwanda vya kusindika pareto.  Viwanda hivi vitawahakikishia wakulima soko la maua yao.  Nina taarifa kuwa katika msimu wa 2001/2002 wakulima wengi walishindwa kuuza pareto yao kutokana na kukosa soko la zao hilo.  Aidha, wakulima waliouza, walikopwa pareto yao.  Napenda Bodi Mpya ya Wakurugenzi isimamie ulipaji wa madeni ya wakulima haraka iwezekanavyo. Bodi ihakikishe hakuna wakulima wanaokopwa pareto yao  msimu unaokuja.  Wanunuzi wa zao la pareto wahakikishe walipa fedha taslimu kwa wakulima na si vinginevyo.

 

7.         Ndugu Mwenyekiti, kuna taarifa pia kuwa pareto ya msimu uliopita bado iko mikononi mwa wakulima.  Ni lazima Bodi ihakikishe pareto yote ya msimu uliopita inaondoka mikononi mwa wakulima ili isichanganywe na pareto ya msimu huu na kusababisha kushuka kwa ubora wake.  Ni matarajio yangu kuwa katika mkutano wenu wa leo mtaweka mkakati wa kushughulikia jambo hili na kuhakikisha tatizo hili halitokei tena.

 

8.         Ndugu Mwenyekiti, kuna tatizo la uwezo mdogo wa kiwanda kilichopo cha kuengua pareto.  Hili ni eneo linalohitaji kupewa kipaumbele katika mipango yenu ya kuendeleza zao la pareto.  Kuwepo kwa viwanda vya kuengua na kuchuja pareto kutasaidia kuimarisha soko la pareto nchini.  Aidha, pareto iliyochunjwa ina soko la uhakika nje ya nchi.  Bodi hii itabidi kubuni mbinu mbalimbali za kuvutia wawekezaji katika viwanda vya aina hii.

 

9.         Mhe. Mwenyekiti, kama mnavyojua serikali imekamilisha maandalizi ya Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo ni kuhakikisha kilimo kinakua kufikia asilimia 11% au zaidi kwa mwaka ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.5 mwaka 2001.  Mambo muhimu yaliyopewa kipaumbele katika mkakati huo ni pamoja na utafiti, huduma za ugani, kilimo cha umwagiliaji maji mashambani, usindikaji wa mazao, matumizi ya pembejeo na zana bora, mikopo kwa wakulima, uimarishaji wa miundo mbinu, n.k.

 

10.       Ndugu Mwenyekiti, Wizara yangu mwaka huu imeanza kutekeleza Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo.  Programu za Kutekeleza Mkakati huu tayari zimeandaliwa.  Bodi ya Pareto inabidi iwe na mpango wake ambao utakuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati.  Kwa mfano, katika msimu wa 2002/2003 uzalishaji wa zao la pareto unatakiwa kuongezeka kwa asilimia 14.  Ili kufikia lengo hili, unahitajika mpango thabiti na usimamizi wa hali ya juu.  Ni matarajio yangu kuwa Bodi hii ya Wakurugenzi itasimamia ipasavyo suala hili.

 

11.       Jambo jingine la kupewa uzito wa juu ni matumizi ya fedha za Bodi.  Lazima Bodi ya Wakurugenzi ihakikishe sehemu kubwa ya Bajeti inatumika katika shughuli zinazomnufaisha mkulima moja kwa moja.  Aidha, fedha inabidi zitumike kwa kufuata mpango maalum na kwa shughuli iliyokusudiwa.  Wizara yangu itasaidia kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya ukosefu wa fedha pale yanapojitokeza, lakini kwa Bodi ambazo zinafuata kanuni za matumizi ya fedha na zile zenye mipango mizuri ya utekelezaji.

 

12.       Mwisho, napenda kuwahakikishia ushirikiano wa Wizara yangu katika autekelezaji wa shughuli mbalimbali za kuendeleza zao la pareto.  Nitapenda Bodi hii iwe mfano mzuri wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo badala ya kuyaainisha tu.  Ni matarajio yetu kuwa Bodi ya Pareto itatekeleza majukumu yake kulingana na sheria na kanuni zilizopo za kuendeleza zao la pareto nchini.  Pale mtakapokwama tafadhali tuwasiliane mara moja bila kuchelewa.

 

13.       Baada ya kusema hayo, sasa natangaza kwamba Bodi Mpya ya Pareto imezinduliwa rasmi.  Nawatakia kazi njema ya kuendeleza zao la pareto.

 

Asanteni Sana kwa Kunisikiliza