HOTUBA YA WAZIRI WA KILIMO NA CHAKULA, MHE. CHARLES N. KEENJA (MB.)  WAKATI AKIWASILISHA MUSWADA WA SHERIA YA HAKI MILIKI ZA WAZALISHAJI WA AINA MPYA ZA MBEGU NA MIMEA  (PROTECTION OF NEW PLANT VARIETIES (PLANT BREEDERS RIGHTS) ACT, 2002) MBELE YA KAMATI YA BUNGE YA UCHUMI NA FEDHA

 __________________________________________

 

1.0              Utangulizi

 

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada wa sheria ya Haki Miliki za Wazalishaji wa Aina Mpya za Mbegu na Mimea  (Protection of New Plant Varieties (Plant Breeders Rights) Act, 2002) unakusudia kutunga sheria itakayoweka utaratibu wa kusajili haki miliki za  wazalishaji wa mbegu na mimea mipya, ili kuharakisha na kuboresha maendeleo ya kilimo kupitia kwa watafiti, wazalishaji na waendelezaji wa mbegu na mimea mipya. Utaratibu huo utahakikisha kuwa watafiti, wazalishaji na waendelezaji wa mbegu na mimea mipya  wanakuwa na haki ya kunufaika na kazi walizozifanya za utafiti, uzalishaji na uendelezaji wa mbegu na mimea mipya, kabla ya mtu mwingine yeyote.  Aidha, Muswada unakusudia kuanzisha ofisi ya Msajili wa haki miliki itakayohusika na usajili na usimamizi wa haki miliki za mbegu na mimea mipya.

 

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya kuweka utaratibu wa utoaji wa haki miliki za wazalishaji na watafiti  wa mbegu na mimea mipya ni muhimu baada ya Serikali kuruhusu sekta binafsi kujihusisha na biashara ya mbegu, kuanzia mwaka wa 1993. Mfumo wa awali uliipa Serikali haki pekee ya kumiliki utafiti, uzalishaji, uuzaji, ununuzi na usambazaji wa mbegu. Mfumo huo ulisababisha mbegu zote zilizozalishwa, ikiwa ni pamoja na mbegu mpya, kutotosheleza mahitaji ya wakulima. Aidha, watafiti na wazalishaji wa mbegu na mimea mipya hawakunufaika moja kwa moja kwa kuwa walikuwa hawapati mapato yoyote kutokana na ugunduzi wao. Shughuli za uzalishaji na uendelezaji wa mbegu na mimea mipya zilikuwa zikifanywa na vituo vya utafiti na mashamba ya Serikali na hatimaye kusambazwa na Kampuni ya mbegu ya Taifa (TANSEED).  Baada ya kuanzisha mfumo wa kuzalisha mbegu na mimea mipya na kuzisambaza kwa kuhusisha sekta binafsi, kumekuwa hakuna sheria yenye kukidhi mahitaji ya kulinda haki za wazalishaji wa mbegu za Serikali na za wazalishaji wa mbegu binafsi, pamoja na kudhibiti usambazaji wa mbegu na mimea mipya. Matokeo yake wazalishaji wa mbegu binafsi wamekuwa wakisita kuwekeza ipasavyo kwenye utafiti wa mbegu. Aidha, kuna hatari ya mbegu mpya zinazozalishwa na Serikali kuibiwa kabla Serikali haijafaidika  nazo ipasavyo.

 

2.0              Madhumuni ya Muswada

 

Mheshmiwa Mwenyekiti, Madhumuni ya Muswada huu ni kutunga sheria mpya itakayoitwa “Protection of New Plant Varieties (Plant Breeders Rights) Act, 2002”,  itakayotambua haki miliki za wazalishaji wa mbegu na mimea mipya na itakayokidhi mabadiliko ya kijamii na kiuchumi kulingana na soko huria la uzalishaji na usambazaji wa mbegu nchini.  Haki hizo zitawawezesha wazalishaji wa mimea na mbegu mpya kunufaika na utafiti wao kutokana na malipo watakayopata kwa kutoa leseni au kuruhusu mbegu zao zitumiwe na wazalishaji wengine kwa ajili ya biashara (“seed multiplication”).

 

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbegu zilizozalishwa na taasisi za Serikali za utafiti zitalindwa chini ya Sheria hii na kuiwezesha Serikali kupata mapato kutoka kwa wazalishaji wa kibiashara watakaoomba na kupewa leseni za kuzalisha au kuuza mbegu na mimea mipya iliyogunduliwa na watafiti wa Serikali. Aidha, kwa kutumia njia ya kuwasajili wazalishaji wa mbegu na mimea mipya Serikali itaweza kudhibiti ubora wa mbegu mpya, ikiwa ni pamoja na kuwadhibiti wazalishaji holela.

 

3.0              Muundo wa Muswada

 

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu umegawanyika katika sehemu kuu kumi na mbili: -

 

Sehemu ya kwanza inaeleza mambo ya kiutangulizi yaani:-

 

·        Jina fupi la sheria na tarehe ya kuanza kutumika kwa sheria;

 

·        Tafsiri ya baadhi ya maneno yaliyotumiwa katika Muswada pia imetolewa. 

 

4.0              Sehemu ya Pili

 

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu ya pili inaanzisha ofisi ya Msajili wa haki miliki za watafiti na waendelezaji wa mbegu na mimea mipya. Aidha, sehemu hii inabainisha kazi za Msajili na utaratibu wa kusajili mbegu na mimea hiyo. Sehemu hii vilevile inaanzisha Kamati ya Ushauri wa utoaji wa haki miliki. Kamati hii itaundwa na wawakilishi kutoka taasisi zifuatazo:

 

(i)                              Chama cha wazalishaji wa mbegu na mimea mipya;

(ii)                            Chama cha wakulima wa mbegu;

(iii)                           Chama cha wafanyabiashara wa mbegu;

(iv)                          Mwakilishi wa wakulima;

(v)                            Chuo Kikuu au taasisi inayohusika na utafiti wa kuzalisha mbegu na mimea mipya;

(vi)                         Wakala wa utoaji wa haki miliki za gunduzi mbalimbali (intellectual property rights); na,

(vii)                         Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

 

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi za Kamati hii zitakuwa ni pamoja na zifuatazo:

§         Kumshauri Waziri kuhusu utekelezaji wa sheria;

§         Kupokea kutoka kwa Msajili na kutoa maoni ya kitaalam kuhusu uhakiki wa hati za maombi ya haki miliki, kabla hazijasajiliwa;

§         Kumshauri Msajili kuhusu utoaji wa haki miliki.

 

5.0              Sehemu ya Tatu

 

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu ya tatu inaainisha sifa za mbegu za mazao ambazo zinastahili kusajiliwa na kupata hifadhi ya kisheria. Sehemu hii vilevile ina vipengele vinavyohusu usajili kwa madhumuni maalum.

 

6.0              Sehemu ya Nne

 

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu ya nne ina vipengele vinavyoelezea utaratibu wa kuomba usajili wa haki miliki. Vipengele hivi ni pamoja na:-

 

a)                  Vipengele vinavyoainisha mambo yanayopaswa yaonekane kwenye hati za maombi; na

b)                  Vipengele vinavyohusu mapendekezo ya jina la haki miliki inayoombwa.

 

 

 

 

7.0              Sehemu ya Tano

 

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu ya tano inahusu utaratibu utakaofuatwa na wazalishaji na waendelezaji wa mbegu na mimea mipya katika kuomba usajili.

 

Sehemu hii inaainisha mabadiliko katika hati za maombi anayoweza kufanya muombaji. Pia Sehemu hii  ina vipengele vinavyoonyesha utaratibu utakaotumika katika kutoa haki miliki, ikiwa ni pamoja na utaratibu na vigezo vitakavyotumika kupinga usajili wa muombaji na namna ya kutolea uamuzi pingamizi hilo.

 

8.0              Sehemu ya Sita

 

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu hii ina vipengele kuhusu kuendelea kwa majukumu ya kisheria yaliyotolewa chini ya Sheria ya Mbegu ya mwaka wa 1973 kuhusu biashara ya mbegu hapa nchini. Aidha, sehemu hii inaainisha mambo yafuatayo:

a) haki za msingi wanazostahili kupewa waombaji;

b) muda  wa kunufaika na haki hizi, ambao utakuwa miaka ishirini; na,

c) ada ya lazima itakayowawezesha wenye haki miliki kuendelea kunufaika na haki miliki walizopewa.

 

9.0              Sehemu ya Saba

 

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu ya saba inatoa madaraka kwa Msajili kubatilisha haki miliki kama mwenye haki miliki atashindwa kutunza na kuendeleza sifa za mbegu husika. Aidha, sehemu hii inamlazimisha mwenye haki miliki kuirejesha haki hiyo, kama atashindwa kuendeleza mbegu husika.

 

10.      Sehemu ya Nane

 

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu ya nane inatoa madaraka kwa wenye haki miliki kutoa leseni za uendelezaji wa mbegu au mimea mipya  kwa waendelezaji wa kibiashara. Aidha, sehemu hii inampa uwezo Msajili kumlazimisha mwenye haki miliki kutoa leseni hiyo kama mhusika atakataa kuitoa bila sababu  za msingi. Sehemu hii vilevile inawataka wahusika kutoa taarifa za leseni zilizotolewa kwa Msajili.

 

11.      Sehemu ya Tisa

 

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu ya tisa inahusu utaratibu wa kusikiliza malalamiko ya mtu yeyote atakayeona kuwa uamuzi uliofanywa chini ya sheria hii sio wa haki. Sehemu hii pia inampa madaraka Waziri kuteua wajumbe wa Bodi ya Rufaa Bodi hiyo imeanzishwa chini ya sehemu hii ili kusikiliza na kutoa uamuzi juu ya malamiko mbalimbali, bila kuathiri haki ya mhusika kukata rufaa mahakamani juu ya uamuzi utakaotolewa na Bodi.

 

12.      Sehemu ya Kumi

 

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu ya kumi inaanzisha Mfuko utakaotumika katika kusimimia maendeleo ya utoaji haki miliki. Matumizi ya Mfuko yatakuwa ni pamoja na:

 

(a)                kulipia gharama za kuanzisha na kuendeleza benki ya mimea na mbegu mpya zitakazosajiliwa chini ya sheria hii;

(b)               kulipia gharama za kuendesha ofisi ya Msajili na kulipia utoaji wa taarifa kwa watafiti kuhusu haki miliki zilizosajiliwa au zinazotarajiwa kusajiliwa;

(c)                kusaidia katika kusimamia utekelezaji wa sheria kwa ujumla.

 

Mapato ya Mfuko huu yatatokana na;

§         ada zitakazokusanywa chini ya sheria hii; na,

§         mikopo au misaada itakayotolewa na watu au taasisi mbalimbali.

 

13.      Sehemu ya kumi na moja

 

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu ya kumi na moja ina vifungu vinavyoainisha makosa  na adhabu kwa makosa hayo.

 

14.      Sehemu ya Kumi na Mbili

 

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu ya kumi na mbili inahusu vipengele mbalimbali vinavyohitajika katika kutekeleza sheria hii. Vipengele hivi ni pamoja na vifuatavyo:

(a) kipengele kinachotoa madaraka kwa Msajili kutathmini na kukusanya ada kutoka kwa waombaji;

(b) kipengele kinachowataka wahusika katika utekelezaji wa sheria kutunza siri za maelezo na nyaraka wanazozipata au watakazozitoa;

(c) kipengele kinachompa mamlaka Msajili kusajili haki miliki za mimea na mbegu mpya zilizozalishwa kabla ya kuanza kwa sheria hii, zikiwemo mbegu na mimea inayomilikiwa na Serikali;

(d) kipengele kinachompa uwezo Waziri kuweka utaratibu wa kuhakikisha kuwa wakulima wananufaika na uendelezaji wa mimea na mbegu zitakayosajiliwa chini ya sheria hii;

(e) kipengele kinachompa uwezo Waziri kutengeneza Kanuni za kusimamia utekelezaji wa sheria hii.

 

 

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.

 

 

 

 

CHARLES N. KEENJA

WAZIRI WA KILIMO NA CHAKULA

OCTOBA, 2002