HOTUBA YA WAZIRI WA KILIMO NA CHAKULA MHE. CHARLES N. KEENJA (MB.) KATIKA SHEREHE YA UZINDUZI WA MBEGU MPYA DAR ES SALAAM, JANUARI 8, 2002

 

 

Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo na Chakula,

Mhe. Katibu Mkuu wa Wizara,

Waheshimiwa Wataalam wetu wa Utafiti,

Waheshimiwa Wageni Waalikwa,

Waheshimiwa Wafanyakazi Wote,

Mabibi na Mabwana.

 

          Waheshimiwa Wageni Waalikwa na Watumishi wa Wizara ya Kilimo na Chakula, napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha kwenye Wizara hii na katika sherehe hii fupi ya kuzindua mbegu mpya za mahindi na mpunga.  Kwa Wakulima na kwa Wizara hii, kuzalishwa kwa mbegu hizi mpya zenye sifa bora za kutoa mazao mengi kwa eneo, ukinzani dhidi ya magonjwa na yanayopendwa na walaji, ni kitendo kinachotupa matumaini kwamba uzalishaji wa chakula nchini utaongezeka na kuihakikishia familia upatikanaji wa chakula na kuiongezea mapato.  Kwa kifupi, kuzinduliwa kwa mbegu hizi mpya ni kitendo cha maendeleo katika kilimo.  Natanguliza shukrani na pongezi kwa watafiti wote waliowezesha kuzalishwa kwa mbegu hizi.  Ahsanteni sana.

2.          Mbegu ni moja ya pembejeo muhimu sana katika kilimo.  Kwa bahati mbaya sana, matumizi ya mbegu bora katika nchi hii ni madogo sana, yanakisiwa kuwa chini ya asilimia kumi tu yakilinganishwa na asilimia 85 Zimbabwe na 62 Kenya.  Wakulima wetu wanatumia mbegu za asili ambazo zinatoa mazao kidogo kwa hekta na huenda zina ukinzani mdogo.  Kuna sababu nyingi zinazowafanya wakulima waendelee kutegemea mbegu zao za asili badala ya mbegu bora.

3.          Sababu za Wakulima kutegemea mbegu zao za asili ni pamoja na mbegu bora kutokupatikana kwa urahisi, kuwa na bei kubwa sana na kutokuwa na baadhi ya sifa zinazopendelewa na walaji kama ladha, raha na kadhalika.  Hali ya upatikanaji wa mbegu bora hivi sasa ni mbaya kuliko ilivyokuwa kabla ya kuanzishwa kwa soko huria.  Shirika la TANSEED ambalo lilikuwa na wajibu wa kuzalisha na kusambaza mbegu bora na zilizodhibitishwa liko katika hali mbaya kifedha na haliwezi kutekeleza majukumu yake hata kwa kiwango kidogo.  Mfumo wa kuzalisha na kusambaza mbegu bora kwa hiyo, umevurugika na Wizara ya Kilimo na Chakula iko mbioni kubuni mfumo mpya ambao utategemea zaidi ushirikiano kati ya vituo vya utafiti, ambavyo vitazalisha mbegu ya watafiti, mashamba ya mbegu ambayo yatazalisha mbegu za msingi (foundation seed) na wakulima binafsi, ambao watasimamiwa kuzalisha mbegu bora zilizothibitishwa (certified seed). Wote wanaohusika wanaagizwa kuharakisha kazi hii ili ikamilike mapema, kwa vyovyote vile, kabla ya mwisho wa mwezi Machi, 2002.

4.          Mbegu tunazozindua leo zina sifa bora ambazo amezieleza Katibu Mkuu na ambazo nitazirudia baadaye kidogo.  Tumekuwa tukiziona mbegu hizi katika vituo vya utafiti na katika maonyesho mbali mbali yakiwamo yale ya Nane Nane 2001, na ya Sayansi na Teknolojia yaliyofanyika Dodoma mwaka jana .  Tunalofanya leo ni kuziondoa mbegu hizo kutoka kuwa za maonyesho na kuzifikisha katika hatua ambapo zitazalishwa kwa wingi na kusambazwa kwa wakulima.

5.          Ningependa kurudia hapa kwamba Wizara ya Kilimo na Chakula inachukua hatua za makusudi kuhakikisha kwamba mbegu bora zinapatikana kwa wingi na kwa bei ambazo mkulima atazimudu.  Kwa muda sasa, wakulima wamekuwa wakiwezeshwa kuzalisha mbegu bora kwenye vijiji vyao chini ya mpango wa Agricultural Sector Programme Support unaohisaniwa na DANIDA.  Utaratibu huo utaendelezwa na kupanuliwa.  Sambamba na mpango wa wakulima kuzalisha mbegu vijijini, tunao wakulima wa kati na wakubwa nao waanzishe kilimo cha mbegu bora na tunawaahidi mbegu za msingi (foundation seed) na ushauri wa kitaalam ili kuwawezesha kufanya kazi hii kwa misingi sahihi na kwa ufanisi.

6.          Mashamba ya mbegu yaliyoko Arusha, Ilonga - Kilosa, Msimba - Kilosa, Mwele - Tanga, Kilangali - Kilosa, Dabaga - Iringa, yataendelea kutumiwa kuzalisha mbegu za msingi na kwa sababu hiyo, hayatabinafsishwa au kuuzwa.  Mashamba hayo yatakuwa sehemu muhimu ya mfumo wa uzalishaji mbegu ambao utaanzia kwenye vituo vya utafiti, mashamba ya mbegu na kuishia na uzalishaji wa mbegu zilizothibitishwa ambao utafanywa na wakulima vijijini, shule za msingi na sekondari, NGO, vikundi vya dini na wakulima wa kati na wakubwa wa mbegu.  Uzinduzi wa mbegu hizi mpya leo, ni sehemu muhimu ya mfumo huo wa kuzalisha mbegu nchini.

7.          Mbegu bora ni pembejeo muhimu ya kilimo lakini peke yake, mbegu bora haitamhakikishia mkulima mazao mengi.  Tunahitaji kuwa na utaratibu mzuri wa kumpatia mkulima mahitaji yake ya mbolea na madawa ya kuulia wadudu kwa wingi, kwa wakati na kwa utaratibu utakaomwezesha kuyapata kwa urahisi karibu na shamba lake.  Kwa wakati huu, mfumo wa kuingiza mbolea na madawa nchini, kama ule wa mbegu, umevurugika na unategemea soko huria.  Tumeanza kuweka utaratibu wa kushauriana mara kwa mara na waagizaji na wasambazaji wa mbolea na madawa ili kuhakikisha kwamba wanaingiza nchini pembejeo hizo za kutosha na wanazifikisha mikoani.  Aidha, tunahimiza kusambazwa kwa mbolea ya Minjingu Phosphate ambayo ina sifa bora sana za kuipatia mimea mahitaji yake ya virutubisho na wakati huo huo kupunguza tindi kali kwenye udongo.  Wizara inashirikiana na sekta binafsi kuweka utaratibu wa uhakika wa kuingiza mbolea na madawa nchini na kuyasambaza.

8.       Tatizo kubwa sana linalotukabili ni uwezo mdogo wa wakulima wa kununua mahitaji yao ya mbegu, mbolea na madawa kwa fedha taslimu.  Tunahitaji utaratibu utakaomwezesha mkulima kupata mahitaji yake ya pembejeo kwa mikopo yenye masharti nafuu.  Aidha, kadri uchumi wetu utakavyozidi kukua, itabidi tuangalie jinsi Serikali itakavyoweza kumsaidia kubeba mzigo wa gharama hizo.  Kwa ufupi, mfumo wote wa kilimo unatazamwa upya kwa lengo la kuwezesha kukua kwa uzalishaji, kupunguza umaskini miongoni mwa wananchi na kuongeza mchango wa kilimo katika uchumi wa Taifa.

9.       Ili kilimo chetu ambacho kinategemea wakulima wadogo wadogo wanaoishi vijijini kikue, ni sharti mipango ya kilimo ya vijijji iwe inaandaliwa na kusimamiwa kwa umakini kuliko ilivyo sasa, vinginevyo vijiji vyetu vitakuwa maskani yanayolea umaskini tu.  Vijiji ni sharti view vituo vya uzalishaji katika kilimo, viwanda vidogo vya kusindika mazao na kutengeneza mahitaji ya wana vijiji na kadhalika.  Mipango ya kilimo ya vijiji ikiandaliwa vizuri, ndipo wakulima watakapoweza kufaidika na mbegu bora, matumizi ya mbolea na madawa n.k.

10.     Ni muhimu sana kwa wakulima kuanzisha na kujiunga na vyama vya ushirika na vyama vya kuweka na kukopa.  Ipo mifano mingi ya mafanikio ambayo wananchi wamepata kwa kujiunga na vyama vya uzalishaji wa mazao na vya kuweka na kukopa.

11.          Pamoja na kuzindua mbegu mpya, mwaka huu Wizara itaanza kuzalisha kwa wingi na kusambaza aina nane za mbegu kama ifuatavyo:

1.                 PAMBA (uk. 91) kuzalishwa kwa wingi ili ziweze kutosheleza mahitaji ukanda wote wa Magharibi.

2.              MTAMA (PATO na MACIA), kuzalishwa na vikundi vya wakulima Mikoa ya Dodoma na Singida

 3.                 MAHINDI (KILIMA ST) Kuzalishwa na vikundi vya wakulima mikoa ya Mara na Mwanza chini ya usimamizi wa Kituo cha Ukiriguru tani 300 zinatarajiwa kuzalishwa.

 UYOLE HYBRID 615 – mbegu hii itazalishwa tena chini ya usimamizi wa Kituo cha Uyole.  Tani 200 zinatarajiwa kuzalishwa.

 4.        MBAAZI          KOMBOA Tani 5 za mbegu hii zitazalishwa na vikundi vya wakulima mkoani Morogoro chini ya usimamizi wa kituo cha Ilonga.

 5.        MAHARAGE      (LYAMUNGU 90, UYOLE 98). Vikundi vya Wakulima vitazalisha mbegu hizi kiasi cha tani 20 kando za Kaskazini na Nyanda za Juu kusini chini ya usimamizi wa vituo vya Selian na Uyole.

6.          Mahindi yenye proteini nyingi (High Protein Quality Maize) ambayo itazalishwa Arusha.

7.                 Low nitrogen draught tolerant Maize nayo yatazalishwa kwenye shamba la mbegu la Arusha.

11.    Baada ya maelezo hayo ya utangulizi sasa natamka rasmi kuzinduliwa kwa mbegu zifuatazo:    

 

MBEGU MPYA ZILIZOTOLEWA NA WATAFITI WA WIZARA MWAKA WA 2001

 

MAHINDI

 

(1).   Uyole Hybrid 615 (UH 615)

KITUO:               ARI Uyole

KIONGOZI WA UTAFITI:- DR. NICK LYIMO

Sifa:             Inavumilia ugonjwa wa ukungu wa Mahindi, “Grey Leaf Spot (GLS) na kutoa mavuno mengi ya tani 8 – 10 kwa hekta

 

(2).  LISHE 1)

(3). LISHE 2) - Quality Protein Maize (QPM)

KITUO:                ARI SELIAN

KIONGOZI WA UTAFITI:- DR. ZUBEDA MDURUMA

SIFA:          Zina virutubisho bora zaidi vya lishe vitakavyoweza kupunguza utapiamlo nchini.

 

 (4).  SITUKA 1

(5).  SITUKA 2

KITUO:       ARI SELIAN

 

KIONGOZI WA UTAFITI: DR. ZUBEDA MDURUMA

SIFA:          Z|inavumilia ukame na pia husitawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ndogo na kuweza kutoa mavuno ya tani 3-4 kwa hekta     

 

(6).  KILIMA – ST

KITUO:       ARI SELIAN

KIONGOZI WA UTAFITI: DR. ZUBEDA MDURUMA

 SIFA:          Hustawi kwenye mazingira mengi tofauti na kustahimili ugonjwa wa melea ya mahindi (streak virus).  In uwezo wa kutoa mavuno tani 6 kwa hekta.

 

(7).  TMV 1 – ST

KITUO:       ARI SELIAN

KIONGOZI WA UTAFITI: DR. ZUBEDA MDURUMA

SIFA:          Inastahimili sana ugonjwa wa melea ya mahindi (maize streak virus) na kutoa mavuno ya tani 5 – 6 kwa hekta.

 

 MPUNGA

(8).  TXD 85

(9).  TXD 88

KITUO:       ARI DAKAWA/ ARI IFAKARA

KIONGOZI WA UTAFITI:         DR. Z. KANYEKA/MR. MSOMBA

 SIFA:          Ni mbegu za kwanza kutolewa nchini zilizo na uwezo wa kutoa mavuno mengi kwa ekari (tani 6-8) na pia kuwa na ladha nzuri.

12.    Baada ya kufanya hivyo napenda niungane na Katibu Mkuu kuwapongeza watafiti wote mliofanyakazi hii chini ya mazingira ambayo mara nyingi yalikuwa magumu.  Mchango wenu katika kuchangia kupunguza umasikini nchini unatambuliwa.  Wizara itajitahidi kuwaongezea uwezo na kuboresha mazingira yenu ya kazi kadi uwezo utakavyoruhusu.

13.    Katika miaka hii, tumeona bei za mazao yetu ya biashara zikiporomoka kwa viwango vya kutisha.  Vituo vyetu vya Utafiti na Watafiti wetu wanakabiliwa na changamoto la kuzalisha mbegu za mazao yatakayolimwa badala ya yale ambayo bei zake zimeshuka sana.  Kituo cha Utafiti cha Katrin kimeagizwa kuzamia katika kukusanya mbegu za aina nyingi ya spices kama  uwezekano na kufanya utafiti wa njia bora za kuzizalisha kwa wingi.  Tunahitaji aina nyingine nyingi za mbegu za mazao mapya na kazi hii ni ya haraka sana.  Ianze mara moja bila kusubiri.

14.        Mwisho, nawatakia heri na fanaka ya mwaka mpya, mwaka wa 2002.  Kwetu katika wizara ya Kilimo na Chakula, huu ni mwaka wa kazi nyingi na ngumu za kufafanua matatizo yanayokabili kilimo na kubuni njia za kuyapatia ufumbuzi.  Mafanikio yetu yatapimwa kwa viwango vya kuongezeka kwa uzalishaji, vya kupungua kwa umaskini na mchango katika Uchumi wa Taifa.  Tunatambua kwamba shughuli za kilimo zinahusu wakulima na taasisi nyingi na Wizara na idara ya Serikali na Washiriki wetu katika maendeleo.  Aidha, kilimo ni shughuli inayoongozwa na sekta ya watu binafsi.  Tutashirikiana na kuwashirikisha washikadau wote wa kilimo katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ya kilimo nchini.  Tungependa kuona mapinduzi katika kilimo chetu na tunaamini kwamba uwezo tunao na nia tunayo. Tunachohitaji ni kuweka mifumo itakayomwezesha mkulima kupata mahitaji yake ya kilimo ya kuyafikia masoko yenye bei nzuri.