Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) amekutana kwa mazungumzo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Bw. Peter Situmbeko Nalitolela, tarehe 9 Aprili 2026 katika ofisi za Wizara ya Kilimo zilizopo Jijini Dodoma.
Viongozi hao wamejadili fursa mbalimbali zinazoweza kunufaisha pande zote mbili za sekta, ikiwemo umuhimu wa kutumia masoko ya mitaji kama nyenzo ya kusaidia upatikanaji wa mitaji kwa wakulima na wawekezaji wa kilimo katika kuongeza tija na ushindani kwenye uzalishaji.
Majadiliano yao pia yamegusia kukuza Sekta ya Kilimo kwa kuongeza thamani ya mazao, kupunguza gharama za uzalishaji, na kumuwezesha mkulima kunufaika zaidi na shughuli zake katika kuleta maendeleo endelevu ya Taifa.
Wakulima wa Idofi, Wilaya ya Makambako wameishukuru Serikali kufuatia kusogezewa mradi mkubwa wa umwagiliaji unaotekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NiRC) utakaonufaisha ekari zaidi ya 1.300. Kwa mujibu wa tathmini ya awali ya wataalamu, mradi huo utahusisha ujenzi wa bwawa la umwagiliaji na uwekaji wa miundombinu ya kisasa itakayowezesha uzalishaji wa mazao mwaka mzima.
Wamesema hayo wakati wa mkutano wa hadhara wa Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) katika viwanja vya shule ya Msingi ya Idofi ambapo amewaelekeza kuwa mradi huo wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu ya Idofi, utawezesha kilimo chenye tija na kufungua fursa mbalimbali za maendeleo katika eneo hilo.