USHIRIKA WAASWA KUWA NA MIFUMO,TARATIBU NA KANUNI IMARA WA KUENDELEZA VYAMA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Ushirika na Umwagiliaji, Dkt. Stephen Nindi amezitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TFC) na Muungano wa Vyama vya Ushirika (SCCULT) kuhakikisha kuwa wanatengeneza Mifumo, Taratibu na Kanuni imara ili kuendeleza Vyama vya Ushirika vilivyo imara.
Ametoa rai hiyo tarehe 10 Januari 2025 katika kikao kazi cha kujadili mwelekeo wa Serikali kuhusu Maendeleo ya Ushirika nchini kilichowashirikisha Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TFC) na Muungano wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SCCULT) kilichofanyika jijini Dodoma.
"Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika katika kuhakikisha inasimamia vyema Vyama vya Ushirika ila jambo la muhimu serikali inalolitaka kwenu TCDC, TFC na SCCULT, tengenezeni Mifumo, taratibu na Kanuni imara ili kuendeleza Vyama na kuwa na Ushirika imara na wenye nguvu," amesema Dkt. Nindi.
Aidha, ameongeza kuwa hakuna haja ya kuwa na utitiri wa Vyama vya Ushirika badala yake kuwe na Vyama vichache ambavyo vitasimama imara na kuweza kuwatetea Wanachama hasa Wakulima ambao ndio wazalishaji wakubwa wa mazao ya kibiashara na hivyo kuimarisha Sekta ya Kilimo hapa nchini.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Ushirika, Bi. Irene Madeje amesema kuwa ili kujenga taswira ya Ushirika iliyosimama kibiashara na Ushirika imara na wenye nguvu ni lazima Vyama vizingatie maelekezo ya Serikali na kutekeleza Vipaumbele vya Ushirika vilivyotolewa na Kamisheni na Wanaushirika.
Vipaumbele hivyo ni pamoja na Uwekezaji katika Mifumo ya kisasa ya kidigitali, Kuimarisha Maendeleo ya Benki ya Ushirika, Kuhamsisha Mfumo wa Ushirika kujiendesha kibiashara, Kuboresha Sera, Sheria na Usimamizi wa Ushirika, Kuhamasisha Ushirika kwenye Sekta mbalimbali na Makundi maalumu, n.k.
Kwa upande wake, Mrajis na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege ametoa rai kwa Bodi za TFC na SCCULT kuhakikisha kuwa Ushirika unamnufaisha kwanza Mwanaushirika mwenyewe na si vinginevyo.