BASHE ATAJA FURSA KWA TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA TATU WA G-25 AFRICAN COFFEE SUMMIT
Tanzania inatarajia kunufaika na Mkutano wa Tatu wa Nchi Zinazozalisha Kahawa Afrika (G-25 African Coffee Summit) kwa kuwa na Kituo kikubwa cha Utafiti wa Kahawa Afrika (Center of Excellence and Research Center for Africa) kitakachojengwa katika Kituo cha Utafiti wa Kahawa nchini (TACRI) kilichopo mkoani Kilimanjaro. Kituo hicho kitalihudumia Bara la Afrika katika masuala ya uzalishaji wa miche na tafiti za Kahawa.
Aidha, Tanzania inatarajia kunufaika kwa kuwa mwenyeji wa Kituo Mahiri cha Mafunzo ya Uzalishaji wa Kahawa (Center of Excellency for Coffee) kitakachojengwa mkoani Dodoma ambacho kitatoa mafunzo muhimu ya masuala ya zao la Kahawa.
Akizungumza na waandishi wa habari tarehe 14 Januari 2025, Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (Mb) amesema kuwa katika mkutano huo, Tanzania kwa pamoja na nchi zinazozalisha Kahawa Barani Afrika zinatarajia kuwa na tamko la pamoja la Dar es Salaam (Dar es Salaam Declaration) lenye kulenga kukuza thamani ya zao la Kahawa.
“Tunataka thamani ya zao la Kahawa katika kipindi cha miaka 10 ijayo iongezwe ili asilimia 50 ya Kahawa inayozalishwa barani Afrika iwe na thamani zaidi kwa kuwa na biashara huru miongoni mwetu ndani ya Afrika. Thamani ya biashara ya Kahawa Duniani ni Dola za Marekani billioni 500, huku Afrika yenye asillimia hamsini ya wazalishaji inapata Dola za Marekani billioni 2.5,” amefafanua Waziri Bashe.
Mhe. Bashe amehitimisha kwa kusema zao la Kahawa si zao la Afrika tu bali ni zao la Dunia akisema kuwa nchi za Afrika hazipaswi kushindana katika zao hilo bali zinapaswa kushirikiana katika kuhakikisha zinazalisha na kuuza Kahawa iliyochakatwa katika masoko ya Kimataifa.
Tanzania ambayo ni mwanachama wa Inter- African Coffee Organization (IACO), imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa G-25 African Coffee Summit tarehe 21-22 Februari 2025, jijini Dar es Salaam kufuatia mkutano huo awali kufanyika katika nchi za Kenya na Uganda. Mgeni rasmi na mwenyeji Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.