KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UWEKEZAJI WA MITAJI YA UMMA YATEMBELEA MAKAO MAKUU YA ASA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imetembelea Makao Makuu ya Wakala wa Mbegu (ASA) na kujionea kazi mbalimbali zinazofanywa na Wakala huo katika kuleta mageuzi ya kilimo nchini.
Ziara hiyo imefanyika tarehe 11 Januari Mkoani Morogoro kutokana na kikao cha Kamati kilichofanyika tarehe 08 Januari 2025 Bungeni jijini Dodoma. Aidha, Kamati pia imetembelea maghala ya Kiwanda cha Mafuta cha Moprocc ambayo kwa muda mrefu yamekuwa hayatumiki.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Augustine Vuma Holle, Mbunge wa Kasulu Vijijini amesema Serikali inapaswa kukaa na mwekezaji ili kumaliza mgogoro uliopo dhidi ya mwekezaji na maghala hayo yaanze kutumika kuhifadhia mbegu za Wakala wa Mbegu za kilimo ASA.
“Ni lazima Serikali ihakikishe Wakala wa Mbegu ASA anapata maghala makubwa zaidi kwa ajili ya kuhifadhia mbegu wanazozalisha lakini jambo la pili Serikali ihakikishe ASA anapata mitambo mizuri ya kisasa ili aweze kuzalisha mbegu kwa kasi kubwa zaidi,” ameeleza Mhe.Augustine Vuma Holle.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Bw. Nyasebwa Chimagu akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo ameeleza kuwa Wakala wetu wa Mbegu za Kilimo ASA imeendelea kufanya vizuri katika uzalishaji wa mbegu bora kwa kushirikiana na Sekta Binafsi.
“Katika Mkoa wa Morogoro kutokana na fursa zilizopo kuna miundombinu muhimu mojawapo ni viwanda ambavyo vilikuwepo ambavyo vinaweza kutumika katika shughuli za kilimo lakini pia yapo maghala ambayo yanaweza kutumika kutumika kwa ajili ya uhifadhi wa mbegu na mazao ili kufikia lengo la kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani million tatu za mazao ifikapo mwaka 2030,” ameongeza Bw. Nyasebwa.
Akizungumza kwa Niaba ya Msajili wa Hazina, Bi. Lightness Mauki ambaye ni ambaye ni Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina amesema Ofisi ya Hazina itaendelea na mazungumzo hayo kama Kamati ya kudumu ilivyo shauri ili maghala hayo yaweze kuanza kutumika.