Dkt. Mpango: Dodoma ina fursa nyingi za kilimo
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amehitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Dodoma na kubaini kuwa mkoa una fursa nyingi za kilimo zinazoweza kuinua zaidi uchumi wa nchi kutokana na ardhi yake kukubali mazao mengi ya aina tofauti. Mhe. Dkt. Mpango amesema hayo katika Kijiji cha Mpwayungu, Wilaya ya Chamwino, Mkoani Dodoma baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Mashamba ya Pamoja na Skimu ya Umwagiliaji ya BBT Ndogowe tarehe 22 Agosti 2024. Makamu wa Rais Dkt. Mpango ameeleza kuwa hapo awali jamii iliaminishwa kuwa mkoa wa Dodoma ni jangwa ambalo linaweza kuzalisha mazao machache jambo ambalo siyo sahihi. Amefafanua kuwa Dodoma inaweza kuzalisha mazao mengi yakiwemo mitende, mizaituni, mipera, parachichi, mikomamanga; hivyo wakulima wachangamkie fursa ya kufanya kilimo cha mazao hayo ili waweze kujiongezea kipato. Kuhusu mkoa kupata kiwango kidogo cha mvua, Mhe. Dkt. Mpango amesema mkoa wa Dodoma una maji mengi chini ya ardhi yanayokidhi kilimo cha umwagiliaji. Hivyo, amesema kuwa Serikali imewekeza kwenye miundombinu ya umwagiliaji ili kuwawezesha wakulima wa mkoa wa Dodoma kuzalisha katika vipindi vyote vya mwaka pasipo kutegemea mvua.