BASHE: ATAJA UMUHIMU WA KUONGEZA THAMANI YA ZAO LA KAHAWA BARANI AFRIKA
Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amesema kuwa Afrika inawazalishaji wa zao la Kahawa ambao ni asilimia 50 kati ya wazalishaji wote Duniani, hata hivyo thamani ya mauzo yake ni Dola za Marekani Bilioni 2.5.
Amefafanua kuwa biashara ya Kahawa Duniani thamani yake ni Dola za Marekani Bilioni 500 katika nchi 50 zinazozalisha zao hilo, ambapo kati yake nchi 25 za Afrika ni Dola za Marekani Bilioni 2.5 huku asimilia 50 ya wazalishaji wote Duniani ni Bara la Afrika.
Mhe. Bashe amesema hayo tarehe 14 Januari 2025 wakati wa Mkutano wake na Waandishi wa habari kuhusu Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Tatu wa Nchi zinazozalisha Kahawa Afrika (G-25 African Coffee Summit) tarehe 21 na 22 Februari 2025, Dar es Salaam. Mkutano na Wanahabari umefanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Kilimo, jijini Dodoma.
“Kwenye mkutano huu wa G-25 African Coffee Summit tunataka tuwe na tamko la Dar es Salaam (Dar es Salaam Declaration) ikiwa ni mojawapo ya lengo kama nchi 25 za Afrika zinazozalisha Kahawa kuongeza thamani ya zao hilo kibiashara badala ya kuuza Kahawa ghafi katika soko la Dunia”, amesema Mhe. Bashe.
Aidha, Waziri Bashe ameeleza kuwa uzalishaji wa zao la Kahawa umeongezeka kutoka Tani elfu 34 hadi kufikia Tani elfu 85 kwa mwaka jana, huku mauzo ya Tanzania nje ya nchi kuongezeka kufika zaidi ya Dola za Marekani Milioni 230 kutoka Dola za Marekani Milioni 140.
Waziri Bashe amesema kuwa moja ya lengo walilojiwekea kama nchi 25 za Afrika zinazozalisha zao la kahawa, ni katika miaka 10 ijayo asilimia 50 ya zao hilo linalozalishwa Afrika liongezewe thamani katika nchi hizo na ifanyike biashara huru miongoni mwao ili kukuza uchumi.