BILIONI 15.7 ZAKAMILISHA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIJI MASHAMBA YA ASA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali imeridhishwa na matumizi ya Shilingi Bilioni 15.7 kwa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji hekta 800 katika mashamba ya Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA).
Amesema hayo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Mhe. Japhet Hasunga (Mb) wakati wa ziara ya Kamati jijini Arusha tarehe 20-22 Machi 2025. Kazi ya kuweka miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba ya uzalishaji wa mbegu inatekelezwa katika shamba la Msimba lililopo Kilosa Mkoani Morogoro na Shamba la Mbegu Kilimi, lililopo Nzega Tabora.
Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) Bw. Leo Mavika ameeleza kuwa ASA itaendelea kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Kamati hiyo ili azma ya Serikali katika kuongeza uzalishaji wa mbegu bora nchini iweze kutimia.
Ziara hiyo pia ilimhusisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dkt. Hussein Mohamed Omar ambaye amesema kuwa Wizara itaendelea kusimamia maelekezo yote yaliyotolewa na Kamati ili kuhakikisha Taasisi zake zinatekeleza ipasavyo. Amefafanua zaidi kuwa ukamilishaji wa miradi hiyo mikubwa ya umwagiliaji utaongeza tija ya uzalishaji wa mbegu nchini na kupunguza uagizaji wa mbegu kutoka nchi za nje.