Dkt. Omar akagua Shamba la makaribio la TARI-Mkuranga
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulia Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Hussein Mohamed Omar amefanya ziara ya kikazi tarehe 20 Desemba 2024 kukagua shamba la majaribio ya tafiti za kilimo (TARI -Mkuranga) lenye ekari 2.6 na kujionea maendeleo ya uzalishaji wa miche ya nazi.
Amewaelekeza TARI - Mkuranga kuhakikisha wanaweka mfumo wa kuvuna maji ya mvua ili kukabiliana na changamoto ya kutegemea maji ya DAWASCO. Katika hatua hiyo, Naibu Katibu Mkuu pia amemuelekeza Dkt. Thomas Bwana, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kuhakikisha kuwa Shamba la TARI - Mkuranga linakuwa katika hali ya usafi pamoja na kuwalipa vibarua wanaolisafisha stahiki zao kwa wakati ili kuomgeza kasi ya kusafisha shamba na kupalilia.
Sambamba na hilo, Dkt. Hussein Mohamed Omar amekutana na uongozi wa TARI katika Kituo cha Mikocheni, jijini Dar es Salaam na kusikiliza changamoto mbalimbali za kiutendaji. Kituo cha TARI - Mikocheni kinahusika na tafiti za zao la nazi ambapo Naibu Katibu Mkuu ameelekeza Kituo hicho kuongeza wigo wa tafiti katika zao hilo; ikiwa ni pamoja na kuwa na aina za miche inayohimili ukame na magonjwa ili kuongeza thamani kwa kuzalisha bidhaa za aina mbalimbali pamoja na upatikanaji wa masoko ya bidhaa zinazotengezwa kwa kutumia nazi.
Kwa ujumla, TARI imeelekezwa kuandaa mpango wa usimamizi wa mashamba yake (Farm Management Plan) ili kuwa na ufuatiliaji mzuri wa tathmini za mashamba na kuhakikisha mashamba yanakuwa katika hali nzuri na ya usafi.