Dkt. Omar aipongeza TTB kwa kuongeza uzalishaji na masoko
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dkt. Hussein Mohamed Omar (anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula) ameipongeza Bodi ya Tumbaku Tanzania kutokana na mwenendo wa uzalishaji, masoko na kuongezeka kwa wastani wa bei ya Tumbaku kwa wakulima kutoka wastani wa Dola za Marekani 1.42 kwa kilo moja katika mwaka 2019/2020 hadi kufikia Dola 2.29 kwa kilo kwa mwaka 2023/2024.
Dkt. Omar ametoa pongezi hizo tarehe 7 Desemba 2024 alipofanya ziara ya kikazi katika ofisi za Bodi ya Tumbaku, mkoani Morogoro ambapo amemuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku Tanzania, Bw. Stanley Mnozya kushirikiana na wadau wa tasnia ya Tumbaku kuhakikisha kuwa vijana wenye taaluma ya ugani wanapatiwa fursa za ajira kupitia BBT Ugani ambayo ni moja ya miradi inayotoa ajira kwa vijana kupitia programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) kama ilivyofanyika kwenye mazao ya Korosho na Pamba.
Awali akiwasilisha taarifa ya mafanikio ya zao la Tumbaku, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku Tanzania, Bw. Stanley Mnozya amemueleza Naibu Katibu Mkuu Dkt. Omar kuwa uzalishaji wa Tumbaku umeongezeka kutoka tani 37,550 mwaka 2019/2020 hadi tani tani 122.858 mwaka 2022/2023.
Bw. Mnozya ameongeza kuwa wanunuzi wapya wa Tumbaku wameongezeka kutoka 3 hadi 21 kufikia mwaka 2024/2025 pamoja na kufufua kilimo cha tumbaku katika mikoa ya Singida, Iringa, Kigoma, Geita, Kagera, Mara na Ruvuma.