Dkt. Omar akabidhi ekari 2,000 kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dkt. Hussein Mohamed Omar ambaye ni Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula amekagua shamba la BBT la Mlazo Ndogowe na kukabidhi jumla ya ekari 2000 kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino na Serikali za Vijiji vya Mlazo na Ndogowe, mkoani Dodoma tarehe 30 Novemba 2024.
Dkt. Omar amesema kati ya ekari 2000, ekari 1000 ni za vijiji vya Mlazo na Ndogowe ambapo tayari ekari 500 zimesafishwa na zinaweza kutumika kuzalisha kuanzia msimu huu na hivyo kuwafanya wananchi wa vijiji hivyo kuanza kunufaika na uwepo wa mradi wa Shamba la Mlazo Ndogowe chini ya programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT).
Katika ziara hiyo, Dkt Omar aliambatana na wawakilishi wa vijana wanufaika wa programu ya BBT waliopangiwa shamba la Ndogowe ambao wameshiriki kukagua hali ya maandalizi ya shamba kwa ajili ya kuanza uzalishaji msimu huu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Mhe. Edson Mdonondo ameishukuru Wizara ya Kilimo kwa kukabidhiwa mashamba hayo hususan kwa kutoa kipaumbele kwa wanakijiji walio jirani na mradi huo.
Mhe. Mdonondo amesema Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino italekeza miradi ya huduma muhimu za jamii katika eneo la mradi huo ili kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika katengeneza ajira zenye staha kwa vijana.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Bw. Titto Mganwa amesema ofisi yake itaendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo katika kuhakikisha mashamba ya vijana ya BBT (Chinangali na Mlazo/Ndogowe) yanakuwa kichocheo kikubwa cha uchumi.