Dkt. Omar ashiriki Kongamano Miaka 63 ya Uhuru
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dkt. Hussein Mohamed Omar (anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula) ameshiriki katika Kongamano la Miaka 63 ya Uhuru lililoandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), mkoani Morogoro tarehe 6 Desemba 2024.
Katika Kongamo hilo, Dkt. Omar ameelezea maono na uthabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuibua fursa mpya kwenye Sekta ya Kilimo na kueleza kuwa mwelekeo huo umechochea Wizara ya Kilimo kutoa hamasa kwa kwa wakulima kujishughulisha na kilimo chenye mtazamo wa kibiashara ambapo fursa za kiuchumi zitapatikana kupitia mnyororo wa thamani katika kilimo.
Aidha, Dkt. Omar amefafanua kuwa Serikali imedhamiria kuhakikisha kilimo kinakuwa endelevu kwa kuongeza uzalishaji wa mazao, uongezaji thamani wa mazao na kuhakikisha usalama wa chakula kwa Taifa.
Dkt. Omar alibainisha kuwa Serikali imejidhatiti kufanikisha maono hayo kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji, kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji, kutoa elimu kwa wakulima, kuanzisha mashamba makubwa ya uzalishaji.
Kuhusu uwezeshaji wa vijana kupata fursa za ajira kupitia Sekta ya Kilimo, Dkt. Omar amesema Serikali inatoa fursa kwa vijana kupitia programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) kwa kuwaandalia na kuwamilikisha mashamba ya pamoja, kuweka miundombinu ya umwagiliaji na kuwatafutia masoko. Kadhalika, ameeleza kuwa Wizara ya Kilimo itaendelea kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) katika kupata wataalamu wa ugani kwa ajili ya programu ya BBT.
Kuhusu wakulima wadogo, Dkt. Omar ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuchimba visima ili kuwewezesha wakulima wadogo kuzalisha mazao kwa mwaka mzima bila kutegemea mvua.