DKT. SERERA AZINDUA MRADI WA GROWING TOGETHER
DKT. SERERA AZINDUA MRADI WA GROWING TOGETHER
Imewekwa: 11 Nov, 2024
Dkt. Suleiman Serera, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo (Ushirika na Umwagiliaji) amezindua Mradi wa Growing Together unaofadhiliwa na Serikali ya Kifalme ya Norway kupitia Shirika la Maendeleo la Norway(Norad) wenye jumla ya thamani ya Euro Million 9.5 sawa na TShs. 27.8 Billion. Hafla hiyo imefanyika tarehe 6 Novemba 2024 katika Hoteli ya Four Points by Sheraton, jijini Dar es Salaam. Mradi ni wa miaka 5 na umelenga kusaidia wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs 10), wakulima wadogo 60,000 na wanunuzi wakubwa (Off Takers) 2 kwa mazao ya Mchele, Mahindi, Maharage na Alizeti katika Mikoa ya Dodoma, Iringa, Mbeya na Morogoro kwa kutatua changamoto ya tija ndogo, upatikanaji wa mikopo nafuu kwa wasindikaji na wakilima, mabadiliko ya tabianchi, ajira kwa vijana na wanawake. Mradi umelenga kuongeza tija, kuimarisha upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu, kuimarisha ushirika wa vijana na wanawake na utasaidia wasindikaji na wakulima kulifikia soko la ndani na nje ya nchi na utachangia kufikia malengo ya Ajenda 10/30. Mradi huo ni mafanikio yaliyotokana na Hati ya Makubaliano (MoU) iliyosainiwa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo na Serikali ya Kifalme ya Norway kupitia Wizara ya Mambo na Maendeleo ya Kimataifa ya Norway kufuatia ziara ya kikazi ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Norway tarehe 12-14 Februari 2024, ambapo Mhe. Rais alisisitiza utekelezaji wake uwaguse wakulima na wasindikaji nchini. Mradi huo unaendana na maeneo ya ushirikiano ambayo yapo kwenye MoU iliyosainiwa ikiwemo uwezeshaji wa Sekta Binafsi kuwekeza katika Sekta ya Kilimo kwa kupata mikopo yenye riba nafuu na kuimarisha ushirika wa vijana na wanawake katika Mifumo ya Uzalishaji wa Chakula nchini.