Dkt. Serera - TBT fanyeni kazi kwa ufanisi zaidi
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Ushirika na Umwagiliaji, Dkt. Suleiman Serera amewataka wafanyakazi wa Bodi ya Chai Tanzania (TBT) kufanya kazi kwa ufanisi na uwajibikaji ili kuongeza tija katika tasnia ya Chai nchini.
Dkt. Serera ametoa rai hiyo wakati akizungumza na wafanyakazi wa TBT katika Makao Makuu yake jijini Dar es Salaam tarehe 4 Desemba 2024.
Aidha, ameitaka TBT kuwatafutia wafanyakazi mafunzo mbalimbali kutoka katika nchi zilizoendelea kwa lengo la kuwaongezea uwezo kazini ili waweze kutumia uzoefu kutoka nchi hizo na kuutumia hapa nchini katika tasnia ya Chai.
“Ili sekta yoyote ikue ni lazima uwepo uwajibikaji kwa watendaji kazi kwenye sekta husika, yani kila mtu awe mbunifu kwa nafasi yake na afanye kazi kwa ufanisi na nawasihi kuwekeza sana katika mafunzo mbalimbali ambayo yanachagiza ukuaji wa sekta hii ya chai."
Kwa upande wake, Bi. Beatrice Banzi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai amemhakikishia Dkt. Serera kuwa TBT itazidi kujiimarisha katika utendaji wake wa kazi kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa.