Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

KATIBU MKUU MWELI: WIZARA ITASHIRIKIANA NA WADAU KUTATUA CHANGAMOTO ZITOKANAZO NA ATHARI ZA VIUATILIFU

Imewekwa: 28 Jan, 2025
KATIBU MKUU MWELI: WIZARA ITASHIRIKIANA NA WADAU KUTATUA CHANGAMOTO ZITOKANAZO NA ATHARI ZA VIUATILIFU


Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli amesema Wizara ya Kilimo itashirikiana na wadau mbalimbali kama Wizara ya Afya, Jeshi la Polisi, Taasisi na Mashirika mbalimbali katika kutatua changamoto zinazotokana na athari za viuatilifu vinavyotumika katika shughuli za kilimo.

Katibu Mkuu Mweli ameshiriki kama mgeni rasmi katika Kikao cha Wadau wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kujadili matukio na madhara ya sumu za viuatilifu yaliyotokea nchini katika mwaka 2017-2024 kilichofanyika tarehe 28 Januari 2025, mkoani Dodoma.  Amesema kuwa miongoni mwa malengo ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2030 ni kuongeza uelewa wa matumizi sahihi ya viuatilifu kuanzia katika ngazi ya manunuzi, uhifadhi pamoja na matumizi.

Katibu Mkuu Mweli ameeleza zaidi kuwa Wizara ya Kilimo itaendelea na tafiti za kugundua viuatilifu bora zaidi na  kuhakikisha wauzaji wa maduka ya pembejeo wanakua na elimu ya kutosha katika kutoa ushauri kwa wakulima ili kukabiliana na changamoto za kilimo pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ya viuatilifu.