KITUO CHA UKAGUZI TPHPA MPAKA WA SIRARI KUJENGEWA MAABARA YA KISASA

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) ametembelea Kituo cha Ukaguzi cha Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kilichopo katika mpaka wa Tanzania na Kenya (Sirari) mkoa wa Mara na kueleza kuwa maabara ya kisasa itajengwa kwenye kituo hicho ili kuongeza kasi ya utendaji kazi.
Mhe. Silinde ametembelea kituo hicho tarehe 24 Januari 2025 wakati anahitimisha ziara yake ya kikazi iliyofanyika kanda ya ziwa katika vituo vya TPHPA mpaka wa Rusumo, Mutukula pamoja na Sirari na
kusema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo itawezesha Taasisi hiyo kujenga maabara za kisasa ifikapo Februari 2025.
Ziara hiyo pia imemhusisha Mkurugenzi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Prof. Joseph Ndunguru na Kaimu Meneja wa TPHPA kanda ya ziwa, Bi. Mary Leina ambapo wameeleza ujenzi wa maabara hizo na kuongeza kuwa kuwa kituo cha TPHPA mpaka wa Sirari kwa mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya tani 116,621.70 za mazao zilikaguliwa na kukidhi vigezo vya kusafirishwa nje ya nchi na jumla ya tani 18,564.97 zilikaguliwa na kuruhusiwa kuingia Tanzania na kupelekea nchi kupata kiasi cha fedha cha shilingi 263,496,501.45/=.
Aidha, Bi. Leina amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 hadi kufikia tarehe 15 Januari 2025 kiasi cha tani 51,639 za mazao zimekaguliwa na kuruhusiwa kwenda nje ya Tanzania na jumla ya tani 5,912.27 zimekaguliwa na kuruhusiwa kuingia nchini na kiasi cha shilingi 142,337,543.00/= zimekusanywa.
Mazao yanayosafirishwa kwa wingi kutoka Tanzania kwenda Kenya kupitia kituo cha TPHPA mpaka wa Sirari ni mahindi, mchele, mtama, nyanya, tangerine, tikiti maji na mazao yanayosafirishwa kutoka Kenya kuingia Tanzania ni viazi mviringo na karoti. Bi. Leona ameeleza kuwa kwa mwaka huu wa fedha zinatarajiwa kukusanywa ni zaidi ya shilingi 250,000,000/=.