Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

MAJUMUISHO YA MATUKIO YA WIKI

Imewekwa: 17 Feb, 2025
MAJUMUISHO YA MATUKIO YA WIKI

Ushiriki wa Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) aliyemwakilisha Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa 48 wa Magavana wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) uliofanyika tarehe 12-13 Februari, 2025 mjini Roma, nchini Italia.

Mapendekezo ya Tanzania ni kuwa na mfumo wa upatikanaji wa mitaji sawia Duniani wa kutambua kuwa wakulima wadogo nao ni wafanyabiashara wadogo kama walivyo wafanyabiashara wengine.

Pia Mhe. Waziri Bashe alikutana na viongozi wafuatao katika mikutano ya uwili (bilateral meetings):

i.    Mhe. Edmondo Cirielli, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Italia kuhusu kukuza ushirikiano katika kilimo;

ii.    Mhe. Luigi D’eilamo, Waziri wa Utawala wa Chakula na Misitu wa Italia kuhusu ununuzi wa Kahawa moja kwa moja kutoka Tanzania; na mwaliko kushiriki maonesho ya kilimo ya Mei 2025 nchini Italia;

iii.    Bw. Donald Brown, Makamu wa Rais wa IFAD kuhusu kuimarisha utendaji kazi wa IFAD Tanzania na kuijengea uwezo zaidi Ofisi ya Mageuzi ya Kilimo (Agriculture Transformation Office - ATO); 

iv.    Mhe. Mutahi Kagwe, Waziri wa Kilimo wa Kenya kuhusu kuimarisha ushirikiano Sekta ya Kilimo.  Mhe. Waziri Bashe pia alimkaribisha Waziri Kagwe kushiriki katika Mkutano wa Tatu wa Nchi Zinazozalisha Kahawa Barani Afrika ambao Tanzania ni mwenyeji, tarehe 21-22 Februari 2025 JNICC Jijini Dar es Saaam;

v.    Mhe. Dkt. Alexander Nuetah, Waziri wa Kilimo wa Liberia; aliomba kuja Tanzania kujifunza namna Tanzania inavyofanya vizuri katika Sekta ya Kilimo ikiwemo programu ya vijana ya BBT.  Waziri huyo pia alialikwa kushiriki Mkutano wa Kahawa ambao Tanzania ni mwenyeji;

vi.    Dkt. Alvaro Lario, Rais wa Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kuhusu kuujengea uwezo Mfuko wa Pembejeo (AGITF) ili kutoa mikopo kwa gharama nafuu kwa wakulima;

vii.    Mkutano na Rais wa Shirikisho la Wazalishaji, Wachakataji na Wanunuzi wa mazao na bidhaa za kilimo nchini Italia kuhusu kushirikiana kukuza na kuendeleza Ushirika nchini.