Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

Mhe. Bashe azungumza na Wawakilishi kutoka Kampuni ya Nasa Corporation na Kawasaki Kiko

Imewekwa: 11 Dec, 2024
Mhe. Bashe azungumza na Wawakilishi kutoka Kampuni ya Nasa Corporation na Kawasaki Kiko

Waziri wa Kilimo, Mhe.Hussein Bashe (Mb) amekutana kwa mazungumzo tarehe 10 Desemba 2024 na wawakilishi kutoka Kampuni ya Nasa Corporation inayojishughulisha na  utengenezaji wa mashine za kufungasha chai na wawakilishi kutoka Kampuni ya  Kawasaki Kiko inayojishughulisha na utengenezaji wa mashine za kuchakata chai kutoka nchini Japan. 

Waziri Bashe ameeleza ujumbe huo kuwa miongoni mwa malengo ya Serikali ni  kuwawezesha wakulima wadogo wa zao la chai nchini kutoka katika kuuza majani pindi wanapovuna hadi kuuza chai iliyochakatwa ili kunufaika na fursa za masoko ya kimataifa.

Amewahakikishia zaidi kuwa kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Japan pamoja Kampuni za nchi hiyo ili kuhakikisha chai yenye ubora kutoka Tanzania inauzwa nchini Japan.

Ujumbe huo utatembelea pia mashamba ya chai yaliyopo mkoani Iringa, Njombe na maeneo mengine nchini ili kujionea uzalishaji wa zao la chai ili kukuza  ushirikiano katika tasnia ya chai.

Ujumbe wa Kampuni hizo uliofika Wizara ya Kilimo, jijini Dodoma umeongozwa na Bw. Daniel Nganga ambaye ni Msimamizi Mauzo Kanda ya Afrika wa Kampuni ya Nasa Corporation; Bi. Gaelle Lagrouas, Gaelle Lagrouas kutoka Idara ya Uzalishaji (Vifungashio na Mauzo Kanda ya Afrika); na Bw. Motohiro Handa, Meneja wa Kitengo cha Usimamizi katika Kampuni ya Kawasaki Kiko.