Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

MHE. MAKONDA:  PIMENI UDONGO KWA AJILI YA KUPATA USHAURI ELEKEZI WA KILIMO

Imewekwa: 07 Mar, 2025
MHE. MAKONDA:  PIMENI UDONGO KWA AJILI YA KUPATA USHAURI ELEKEZI WA KILIMO

Katika hamasa za maonesho ya wiki ya wanawake Duniani zinazoendelea Mkoani Arusha wananchi wa Mkoa huo na maeneo ya jiran wamehimizwa kujitokeza kwa wingi ili kupata huduma ya kupimiwa afya ya udongo bure na kupatiwa ushauri elekezi.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda alipotembelea Maabara ya Wizara ya kilimo na kuzungumza na wanahabari huku akisema kuwa huduma hiyo inatolewa bure na kwa haraka.

“Niwasihi wananchi wote wa Mkoa wa Arusha kwa pande zote waliopo beba udongo wako njoo nao, hapa nilipo kuna Maabara iliyo kamilika yenye kusaidia kupima aina ya udongo wako na wataalam watakushauri matumizi sahihi ya mbolea na mazao husika unayopaswa kulima kwa aina ya udongo wa shamba lako,” amesema Mhe. Paul Makonda.

Aidha, ameeleza kuwa upimaji wa Afya ya Udongo utamsaidia mkulima kujua aina sahihi ya matumizi ya Mbolea na hata kupatiwa ushauri wa kulima mazao husika yanayofaa kulimwa kutokana na majibu ya udongo uliopimwa kutoka kwa wataalam.

Kilele cha Maonesho ya Siku ya Wanawake Duniani itafanyika tarehe 8 Machi 2025 ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kauli mbiu ni “Wanawake na Wasichana 2025; Imarisha Usawa Haki na Uwezeshwaji”.