Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

MOROGORO YAJIKITA KATIKA KILIMO KUONGEZA MAPATO

Imewekwa: 16 Feb, 2025
MOROGORO YAJIKITA KATIKA KILIMO KUONGEZA MAPATO

Mkoa wa Morogoro umejipanga kukuza mapato yake ukichangiwa kwa kiasi kikubwa na Sekta ya Kilimo kutoka pato la shilingi milioni 800 hivi sasa hadi kufikia shilingi bilioni 2 na kuendelea kwa miaka mitatu hadi minne  ijayo.

Akizungumza mara baada ya kutembelewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara, Kilimo Mifugo na Uvuvi tarehe 15 Februari 2025 mkoani Morogoro, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amesema Mkoa huo umejikita katika kilimo cha kisasa cha mazao ambayo hayapewi kipaumbele na wakulima hasa parachichi, viazi mviringo, tumbaku na kahawa kama mazao ya kimkakati ya mkoa huo.

Jumla ya hekari 272 za parachichi zimekwisha pandwa katika mashamba ya wakulima, huku miche 120,000 ikiandaliwa.  Lengo likiwa ni kupanda zaidi ya hekari 1700 za zao hili katika wilaya ya Gairo, kata ya Nongwe, ifikapo mwezi Mei mwaka huu katika kuhakikisha kila kaya inakuwa na hekari moja ya parachichi.

Kwa upande wa viazi mviringo jumla ya tani tatu za viazi zimekwisha sambazwa katika vikundi vya wakulima katika Tarafa ya Nongwe ili kuwafundisha kilimo cha zao hilo na kuwaonesha namna wanavyoweza kujikwamua kiuchumi.

Aidha,  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara Kilimo Mifugo na Uvuvi ilipata nafasi ya kutembelea shamba la mfano la viazi mviringo katika kijiji cha Masenge kitongoji cha Nongwe pamoja na kitalu cha parachichi kilichopo katika kijiji cha Mkobwe katika kitongoji hicho na kuridhishwa na jitihada zinazofanyika katika kukuza Sekta ya Kilimo.