MRADI WA UMWAGILIAJI KULETA KILIMO CHA UHAKIKA KWA MISIMU YOTE

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo (anayesimamia Ushirika na Umwagiliaji), Dkt. Stephen Nindi ameieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuwa mradi wa umwagiliaji unaogharimu shilingi bilioni 13.6 wa Bwawa la Nyida umefikia hatua ya utekelezaji wa asilimia 75% kukamilika kwake.
Dkt. Nindi amesema hayo wakati wa ziara hiyo tarehe 13 Machi 2025 mkoani Shinyanga na kueleza kuwa mradi huo wa bwawa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha kilimo cha umwagiliaji nchini, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji wa mazao na kupunguza utegemezi wa mvua.
“Hadi kufikia hatua hii tunaimani kuwa wakulima sasa wataanza kunufaika na miradi kama hii ya umwagiliaji ili kilimo chao kiwe cha uhakika kwa misimu yote. Tayari sehemu ya ujenzi ukuta umekamilika, huku baadhi ya mashamba yameanza kutengenezewa mifereji ya kupitisha maji,” amesema Dkt. Nindi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Umwagiliaji, Bw. Raymond Mndolwa amesema mradi huo wa ujenzi utahusisha miundombinu ya bwawa, ukarabati wa mifereji ya skimu pamoja na ofisi ndogo ya Tume ya Umwagiliaji (NIRC).
Aidha, Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Deodatus Mnyika (Mb) ameishukuru NIRC na Wizara ya Kilimo kwa ujumla katika kutekeleza ujenzi wa miradi ya maendeleo, pia alisisitiza kuwa waongeze juhudi kwani muda mchache umebakia kukamilisha bwawa hilo.
Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huo kwa kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kuwanufaisha wakulima kwa kuboresha upatikanaji wa maji kwa shughuli za kilimo.