MWELI: MATUMIZI YA MBOLEA YAFIKIA TANI LAKI NANE NCHINI
MWELI: MATUMIZI YA MBOLEA YAFIKIA TANI LAKI NANE NCHINI
Imewekwa: 11 Nov, 2024
Wizara ya Kilimo kupitia Mamlaka ya udhibiti wa Mbolea Tanzania -TFRA imeongeza tija ya matumizi ya mbolea kwa wakulima nchini hadi kufikia tani 800,000.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli wakati akizindua Kongamano la Kwanza la Mbolea tarehe 11 Oktoba, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa JK Nyerere, uliopo Wizara ya Fedha, jijini Dodoma.
"Tumeongeza matumizi ya mbolea mpaka tani laki 800,000 kwa mwaka 2024 kutoka tani 360,000 mwaka 2021/2022 kipindi ambacho mpango wa utoaji wa mbolea ya ruzuku ulipoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hivyo tunavyoona maendelea haya hatuna budi kumpongeza Mhe. Rais kwa kuendelea kutoa ruzuku kwa wakulima ili wazalishe kwa tija,” amesema Karibu Mkuu Mweli.
Aidha, Katibu Mkuu Mweli amezipongeza kampuni za ndani zinazozalisha mbolea kuendelea kuzalisha mbolea kwa wingi na ametoa rai kwa wawekezaji mbalimbali kuja kuzalisha mbolea nchini na kuhakikisha matumizi ya mbolea yana akisi na afya ya udongo ili Tanzania ifikie malengo ya kuwa kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa mbolea katika Mataifa mengine Barani Afrika.
Kongamano hilo limehudhuriwa pia na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara Kilimo, Mifugo na Uvuvi; wakiwemo wadau wa maendeleo pamoja na wawakilishi kutoka Mataifa mbalimbali.
Kongamano hilo ni la siku mbili ambapo washiriki watajadili masuala mbalimbali ya uendelezaji wa tasnia ya mbolea nchini, chini ya kauli mbiu "Kilimo ni Mbolea".