PAC YARIDHISHWA NA UJENZI WA VIHENGE VINAVYOSIMAMIWA NA NFRA BABATI MANYARA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeridhishwa na ujenzi wa vihenge vya kuhifadhia mazao na maghala wilayani Babati, Mkoa wa Manyara ambavyo vinasimamiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).
PAC ilifanya ziara tarehe 18 Machi 2025, ambapo Makamu Mwenyekiti wa PAC, Mhe. Japhet Hasunga (Mb) amesema kuwa lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kukagua utekelezaji wa mradi huo na thamani ya fedha zilizotumika.
"Tumekuja kuona mradi wa vihenge ambapo Kamati imefurahishwa sana na namna vihenge vilivyojengwa, kwani vinaongeza uwezo wa kuhifadhi chakula kwa manufaa ya Taifa," amesema Mhe. Hasunga.
Vihenge hivyo kwa sasa vimehifadhi tani 776,000 za mazao, zikiwemo tani 32,000 za mpunga; tani 400 za mtama (tayari zimechukuliwa) ambapo lengo la Serikali kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 kuhifadhi tani milioni 3.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli amesema kuwa miradi hiyo awali ilikuwa imekwama, lakini Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alihakikisha inapata ufadhili ili kuendelea na utekelezaji wake.
"Tumepokea maelekezo ya Kamati na tutahakikisha kuwa vituo vitano vilivyosalia kati ya nane vinakamilika haraka ili wananchi wapate huduma," amesema Katibu Mkuu Mweli.