SERIKALI YAKAMILISHA UJENZI BWAWA LA KASORI KWA BILIONI 11.4

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Kenani Kihongosi amesema kuwa Serikali imekamilisha ujenzi wa Bwawa la Kasori kwa gharama ya shilingi bilioni 11.4 ambazo ni fedha zilizotolewa na Wizara ya Kilimo. Bwawa hilo linatarajiwa kuwa msaada mkubwa kwa wakulima wa Mkoa huo, hususan katika umwagiliaji na uhifadhi wa maji kwa ajili ya kilimo cha pamba na mazao mengine.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi iliyoambatana pia na Dkt. Stephen Nindi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo (anayesimamia Ushirika na Umwagiliaji) tarehe 12 Machi 2025 amesema kuwa Mkoa wa Simiyu unaendelea kuwa kinara wa uzalishaji wa pamba nchini Tanzania.
“Katika msimu uliopita, tulizalisha tani 70,000 za pamba, lakini kwa msimu ujao tuna mpango wa kuzalisha tani 200,000. Hili litawezekana kupitia upanuzi wa eneo la kilimo hadi hekta 278,000,” ameeleza Mhe. Kihongosi.
Ameongeza kuwa Mkoa huo pia unazalisha mazao mengine ya biashara na chakula. Kwa mfano, mnamo Februari 2025, zaidi ya tani 2,905 za choroko ziliuzwa, hatua inayothibitisha ukuaji wa Sekta ya Kilimo katika Mkoa wa Simiyu.
Mkuu wa Mkoa pia ameeleza kuwa Serikali imeanza ujenzi wa nyumba sita za maafisa ugani katika wilaya za Bariadi na Meatu kwa ufadhili wa Wizara ya Kilimo katika kuhakikisha kuwa wataalamu wa kilimo wanakuwa karibu na wakulima kwa ajili ya kuwapa ushauri na msaada wa kitaalamu.
Mkoa wa Simiyu unaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza uzalishaji wa mazao na kuboresha maisha ya wakulima, huku ukitumia rasilimali zilizopo kwa manufaa ya wananchi wake.