Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

SERIKALI YAWEKA MSISITIZO UZALISHAJI MAZAO YA VIUNGO

Imewekwa: 18 Feb, 2025
SERIKALI YAWEKA MSISITIZO UZALISHAJI MAZAO YA VIUNGO

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe David Silinde (Mb) amesema Serikali imeendelea kuwainua wakulima kupitia mpango wa ruzuku za pembejeo za mbegu pamoja na mbolea akiwataka wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha miradi yote ya kilimo inatekelezwa kwa ufasaha.

Akiwa mkoani Morogoro, Mhe.Silinde ameshiriki katika uzinduzi wa kampeni ya "Jisomeshe na Mkarafuu Mkoa wa Morogoro" tarehe 17 Februari 2025 ambapo miche 10 ya Mikarafuu iligaiwa kwa kila mwanafunzi wa shule za Sekondari ili waweze kujiendeleza kimasomo kupitia kilimo cha zao hilo.

Mhe. Silinde amesema Wizara ya Kilimo itashirikiana na wakulima katika kufanikisha kampeni hiyo na kuhakikisha rasilimali zinazopatikana zinatumika ipasavyo katika kuendeleza malengo ya kampeni hiyo. 

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo (anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula), Dkt. Hussein Mohamed Omar amesema Wizara itahakikisha inatekeleza Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo kwa mwaka 2025/2050 unaotoa pia kipaumbele kwa mazao ya viungo kwa kuhakikisha upatikanaji wa fedha na utekelezaji wa vipaumbele unajumuisha mkoa wa Morogoro katika kuendeleza zao hilo.  

Jumla ya miche ya Mikarafuu 8000 inatarajiwa kugawiwa katika hatua ya awali kwa wanafunzi 796 katika kata 5 za Wilaya ya Morogoro vijijini lengo likiwa ni kuongeza miche zaidi katika maeneo mengine Mkoa wa Morogoro.

Miche Mkarafuu inakomaa kwa wastani wa miaka 5 hadi 6, ikizalisha mazao kwa muda wa miaka 50 kwa wastani wa kilogramu 15000 kwa mti mmoja iwapo utatunzwa vyema. Wastani wa  bei kwa kilogramu moja ni shilingi 18000 hadi 20000.