SHAMBA LA MBEGU MSIMBA KURAHISISHA UPATIKANAJI MBEGU

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi tarehe 18 Februari 2025 imetembelea shamba la mbegu Msimba lililopo chini ya Wakala wa Mbegu za Kilimo nchini (ASA) na kupata taarifa ya utekelezaji wa Wakala wa Mbegu za Kilimo, kutembelea ghala pamoja na karakana.
Kamati ilipata elimu na kukagua miundombinu ya uzalishaji katika shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 2,000 ambapo hadi kufikia Februari 14 hekta 665 zimelimwa na upandaji unaendelea lengo likawa ni kuvuna tani 1,056 za mbegu kwa msimu huu.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa ASA, Bw. Leo Mavika amesema uzalishaji huu unalenga kuwezesha upatikanaji wa mbegu kwa wakulima kwa bei nafuu na kukabiliana na changamoto ya uagizaji wa mbegu toka nje ya nchi, ambapo hadi kufikia mwaka 2023/2024 jumla ya tani 4,510.0 za mbegu zimezalishwa nchini toka tani 3,034.4 kwa 2020/2021 likiwa ni ongekezo la 48.3%.
Shamba hili lipo katika Tarafa ya Kimamba, kata ya Chanzuru, kijiji cha Ilonga wilayani Kilosa Mkoani Morogoro likitumika kuzalisha mbegu za mazao ya alizeti, mbaazi ufuta na choroko.
Naye Mwenyekiti wa Kamati, Mhe.Deodatus Mwanyika (Mb) ameitaka Serikali kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya kutosha katika shughuli za uzalishaji wa mbegu ikiwemo zana za kilimo, miundombinu ya umwagiliaji pamoja na magari.
Kamati hiyo pia iliambatana na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe David Silinde (Mb) pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo (anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula), Dkt. Hussein Mohamed Omar ilihitimisha kwa kutembelea Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI -ilonga na kuzindua miundombinu ya umwagiliaji katika shamba la hekta 15.