Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

SILINDE AIAGIZA TPHPA KUJENGA MAABARA ZA KISASA VITUO VYA UKAGUZI RUSUMO NA MUTUKULA

Imewekwa: 24 Jan, 2025
SILINDE AIAGIZA TPHPA KUJENGA MAABARA ZA KISASA VITUO VYA UKAGUZI RUSUMO NA MUTUKULA

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) ameiagiza Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kujenga maabara za kisasa katika vituo vya ukaguzi vya mpaka wa Rusumo Ngara (karibu na nchi ya Rwanda) na Mutukula (karibu na nchi ya Uganda) ifikapo Februari 2025, zitakazo rahisisha zaidi utendaji kazi wa vituo hivyo.

Mhe. Silinde amefanya ziara ya kikazi katika vituo vya ukaguzi vya TPHPA katika Mpaka wa Rusumo Ngara na Mutukula iliyopo Wilaya ya Missenyi katika mkoa wa Kagera, tarehe 23 Januari 2025.

Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Prof. Joseph Nduguru amesema atafanyia kazi agizo hilo na kuhakikisha vituo hivyo vinajengwa maabara za kisasa ili kuboresha zaidi huduma zinazotolewa.

Aidha, Kaimu Meneja wa TPHPA Kanda ya Ziwa, Bi. Mary Leina, ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024, vituo vya Rusumo na Mutukula vilifanya kazi nzuri kwa kukagua mazao yenye uzito wa tani 331,537. TPHPA ilikusanya zaidi ya shilingi milioni 374 kutokana na huduma za ukaguzi, na sehemu kubwa ya mazao hayo yalisafirishwa kwenda nchi za nje, hasa mchele, mtama, maharage, na molasses.

Bi. Leina ameongeza kuwa kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025, Mpaka wa Rusumo tayari umehakiki tani 98,275.67 za mazao, na kuingiza fedha zaidi ya shilingi milioni 140,000,000, huku Mpaka wa Mutukula ukikagua tani 51,692.003 za mazao na kupata kiasi cha shilingi milioni 101,718,772.

"Mpaka wa Rusumo na Mutukula ni muhimu sana katika biashara ya mazao ya kilimo, na kupitia ujenzi wa maabara za kisasa, tunaamini tutaongeza tija na kuhakikisha kuwa mazao yanayohitaji kusafirishwa nje ya nchi yanakaguliwa kwa ufanisi zaidi," amesema Bi. Leina.

Hii ni hatua kubwa kwa Tanzania, kwani inaonesha dhamira ya Serikali kuboresha mifumo ya ukaguzi wa mazao na kuhakikisha usalama wa afya ya mimea na viuatilifu katika biashara ya Kimataifa.