Silinde - Waliofanya Uharibifu katika Shamba la Msimba Wachukuliwe hatua kali
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) ameiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro kuwachukulia hatua kali za kisheria baadhi ya wafugaji waliofanya uharibifu wa kukata uzio wa waya katika Shamba la Mbegu Msimba kisha kuingiza mifugo kwa ajili ya malisho na kusababisha hasara kwa Serikali.
Mhe. Silinde amesema hayo tarehe 7 Desemba 2024, mara baada ya kutembelea na kushuhudia eneo lililokatwa uzio wakati akiendelea na ziara ya kikazi katika Mkoa huo.
“Tukio lililofanyika ni uhujumu uchumi maana limefanyika kwa kusudi na baadhi ya wafugaji, hivyo wachukuliwe hatua kali za kisheria ili iwe funzo kwa watu wengine maana mbegu ndizo zinazoleta usalama wa chakula na Serikali imewekeza fedha nyingi kwa Wakala wa Mbegu za Kilimo Nchini (ASA)”, ameeleza Mhe. Silinde.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo Nchini (ASA) Bw. Leo Justine Mavika ameishukuru Serikali na Jeshi la Ulinzi na Usalama kwa kushirikiana na ASA kukamata mifugo iliyopitishwa kwenye uzio na wafugaji na kusema atahakikisha waliofanya tukio hilo wanachukuliwa hatua.
Aidha, Meneja wa Shamba la Mbegu Msimba, Bw. Samson Mollel amesema tukio hilo limefanyika usiku wa kuamkia tarehe 6 Desemba 2024 ambapo alipokea taarifa kwa walinzi wa eneo hilo na kuzipeleka kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambapo walifika katika eneo la tukio na kushuhudia uzio uliokatwa wenye urefu wa mita 11 na kuona nyaya na sehemu zingine za shamba hilo zilizoharibiwa na kufanikiwa kukamata ng’ombe 576.
Baada ya kutembelea shamba hilo, Mhe. Silinde aliongea na watumishi wa Taasisi ya ASA na kuwahimiza wafanye kazi kwa kusaidiana na kwa kujituma ili kuweza kufikia lengo la Serikali la kuongeza uzalishaji wa mbegu bora nchini.