Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

TFC kuharakisha usambazaji wa Mbolea ya Ruzuku

Imewekwa: 10 Dec, 2024
TFC kuharakisha usambazaji wa Mbolea ya Ruzuku

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) ameiagiza Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC ) kuharakisha usambazaji wa mbolea ya ruzuku kwa wakulima wote nchini kwani tayari msimu wa kilimo umeanza.

Akizungumza mara baada ya kutembelea ghala la kuhifadhi mbolea lililopo eneo la Chuo cha Magereza, Ukonga, jijini Dar es Salaam tarehe 9 Desemba 2024, Mhe. Silinde amesema ameridhishwa na kasi ya kazi inayofanyika huku akiagiza ndani ya siku 10 kazi hiyo iwe imekamilika na mbolea yote ikiwemo tani 2,000 za Urea zisambazwe kwa wakulima wa Tumbaku.

“Moja ya maelekezo ya Serikali ni kusambaza tani 61,000 za mbolea kwa wakulima wa zao la Tumbaku na jukumu hili ilipewa TFC, ambapo hadi sasa tani hizo zimeshasafirishwa kutoka Mkoa wa Mbeya na kusambazwa kwa wakulima wa zao hilo.  Mbolea aina ya Urea na CAN zaidi ya tani 10,700 nazo zinaendelea kusambazwa”, ameeleza Mhe. Silinde.

Ametoa rai kwa waagizaji wengine wa mbolea nchini kuhakikisha wanasambaza kwa wakati kama lilivyo lengo la Serikali ili msimu wa kilimo uende sambamba na mbolea itakayotumika kwenye mazao na kuweza kuongeza tija kwa wakulima nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Bw. Samuel Mshote ameeleza kuwa kazi ya upakiaji wa mbolea unaendelea
katika eneo la Chuo cha Magereza, Ukonga na ghala lililoko Mbagala, jijini Dar es Salaam; huku akibainisha kuwa mchakato wa mbolea tani 15,000 unaendelea.